Monday, January 18


Hatua Ambazo Zimechukuliwa Dhidi Ya Stanbic Bank Tanzania Limited Kuhusu Ushiriki Wake Kuwezesha Mkopo Wa Serikali Wa Dola Za Kimarekani Milioni 600
____________________

Utangulizi
Mwezi Julai 2013, Benki Kuu ya Tanzania kupitia ufuatiliaji wa kawaida wa shughuli za mabenki iligundua matatizo yaliyohusiana na hasara itokanayo na mikopo na pia kuacha na kuondolewa kazini kwa viongozi waandamizi wa Stanbic Bank Tanzania Limited (Stanbic) katika muda mfupi.
Kutokana na hilo, Benki Kuu iliamua kufanya ukaguzi wa kulenga (Targeted Examination) katika benki hiyo. 
Ukaguzi huo ni kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa Benki Kuu chini ya Kifungu 47 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 na Kifungu 31 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

Matokeo ya Ukaguzi wa Benki Kuu
Katika ukaguzi huo, wakaguzi wa Benki Kuu, pamoja na mambo mengine walibaini miamala ya kutia shaka iliyohusu malipo kwa kampuni ya kitanzania ya Enterprise Growth Market Advisors (EGMA). 
Kampuni ya EGMA ilihusika katika uwezeshaji wa upatikanaji wa Mkopo kwa Serikali ya Tanzania ambapo Standard Bank Plc (ambayo kwa sasa inajulikana kama ICBC Standard Bank) na Stanbic Bank Tanzania Limited kwa pamoja walikuwa “Mwezeshaji Mkuu” (Lead Arranger).
Malipo hayo kwa kampuni ya EGMA yalikuwa yamefanyika kinyume na taratibu za kibenki na yalihusisha uongozi wa benki ya Stanbic. 
Jumla ya malipo yalikuwa ni kiasi cha dola za kimarekani milioni 6, na zililipwa katika akaunti ya EGMA na kutolewa kwa muda mfupi kwa njia ya fedha taslimu (cash) ambayo ni nje ya taratibu za kibenki.

Taarifa ya ukaguzi huo iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic kwa mujibu wa taratibu, na Benki Kuu iliiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo kuchukua hatua stahiki za kurekebisha kasoro zilizoonekana.
Aidha, benki ya Stanbic iliagizwa kutoa taarifa kwa Kitengo cha Financial Intelligence Unit (FIU) kilichopo Wizara ya Fedha na Mipango kuhusiana na miamala hiyo yenye mashaka katika akaunti ya EGMA kama Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu ya mwaka 2006 (The Anti-Money Laundering Act, 2006) inavyoelekeza. Benki ya Stanbic ilitekeleza maagizo na kutoa taarifa FIU kuhusu miamala inayotiliwa shaka.

Mnamo 29 Septemba 2015, Benki Kuu ilipokea barua toka Idara ya Serikali ya Uingereza inayohusika na Upelelezi wa Makosa ya Kugushi na Rushwa (Serious Fraud Office - SFO) ikiiomba Benki Kuu ruhusa ya kutumia ripoti yake ya ukaguzi kama ushahidi katika kesi dhidi ya Standard Bank Plc ambayo ilikuwa ni mshirika wa Stanbic Bank Tanzania Limited katika kuwezesha mkopo wa dola za kimarekani milioni 600 kwa Serikali na kwamba ripoti hiyo ingekuwa wazi kwa umma. 
Benki Kuu iliijibu SFO kuwa kwa mujibu wa Sheria ripoti za Benki Kuu zinatolewa tu kwa benki au taasisi ya fedha inayohusika, hata hivyo, Benki Kuu haikuwa na pingamizi kwa SFO kutumia taarifa za ripoti hiyo kwa kuzingatia chanzo cha ripoti hiyo.

Hatimaye, Standard Bank Plc ilikubali makosa na ilitozwa faini ya jumla ya dola za kimarekani milioni 32.20, ambapo kiasi cha dola za kimarekani milioni 7 zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania (dola za kimarekani milioni 6 zilikuwa ni fidia na dola za kimarekani milioni 1 ni riba).

Kwa kuzingatia mapungufu ya kufanya miamala iliyohusisha EGMA na pia kutokuweka taratibu madhubuti za udhibiti wa ndani, na kwa kuzingatia Kifungu 67 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu imeiandikia benki ya Stanbic barua ya kusudio la kuitoza faini ya shilingi bilioni 3. 
Sheria inaitaka benki ya Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha siku ishirini (20) ambacho kitaisha tarehe 30 Januari 2016. Endapo Benki Kuu haitaridhika na utetezi, benki ya Stanbic italazimika kulipa faini hiyo.

Hitimisho
Benki Kuu imechukua hatua hizo kama onyo kwa benki ya Stanbic na ili iweze kuwa makini katika kuhakikisha kuwa shughuli zake zinaendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kibenki na kuzingatia Sheria.

Aidha, hatua hii ni onyo kwa mabenki na taasisi za fedha zisijihusishe na makosa ya aina hii ambayo ni kinyume cha taratibu za kibenki na ni uvunjaji wa Sheria za nchi.
Hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa benki au taasisi ya fedha yoyote itakayobainika kwenda kinyume na taratibu za kibenki na Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

0 comments:

-