WAMILIKI
wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali wameiomba Serikali kufuta mfumo
wa GPA unaotumiwa na Baraza la Mitihani (Necta) kupanga madaraja ya
mitihani ya sekondari, kwa maelezo kuwa haufai kwa kuwa unahalalisha
watahiniwa waliofeli waonekane wamefaulu.
Akizungumza
jana Dar es Salaam kuhusu matokeo ya kidato cha pili ambayo
yametangazwa na Necta hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi (TAMONGSCO), Benjamin Nkonya alisema
matokeo hayo hayaeleweki kwani wameshuhudia baadhi ya wanafunzi
wanaoonekana kufanya vizuri chini ya mfumo wa GPA wakati katika mfumo wa
madaraja (division) wanaonekana wamefanya vibaya.
Kwa
hali hiyo, Nkonya amemwomba Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kufuta mfumo huo hadi pale Necta
itakapokuwa tayari kujibu maswali kadhaa ya wadau wa elimu ambao wanaona
mfumo huo hauna tija katika kuboresha elimu.
Baadhi
ya hoja ambazo zilihojiwa na Nkonya ni kwamba kulikuwa na kasoro gani
katika mfumo wa madaraja mpaka ukaja huo wa GPA na akataka kujua ni nani
alilalamikia mfumo wa division mpaka ukaondolewa? Alihoji kabla ya
mfumo huo kuletwa, ni wadau wapi walishirikishwa?
Alisema
TAMONGSCO ilipata taarifa za kuwepo kwa mfumo huo wa GPA kupitia vyombo
vya habari na hawakushiriki katika ngazi yoyote ya mijadala ya kisera
kama sheria inavyoelekeza.
Katibu Mkuu huyo wa TAMONGSCO alihoji, “Je,
alama za chini za gredi D, C,B na A zilibaki kama zilivyokuwa wakati wa
mfumo wa division au kuongeza gredi E na B+ ilikuwa mbinu ya kushusha
alama za ufaulu na matumizi ya GPA yakaanzishwa kwa lengo la kuficha
ukweli kuwa viwango vimeshushwa kwa kiasi kikubwa??
Nkonya
pia alihoji mfumo huo una faida zipi na unasaidiaje katika kuhakikisha
kuwa wanafunzi wanaomaliza wanakuwa na ujuzi stahiki utakaowawezesha
kuhimili changamoto za soko la ajira na utandawazi?
“Kwa hali hii bado tunaishauri Serikali isitishe matumizi ya mfumo wa GPA hadi pale hoja zetu zitakapopatiwa ufumbuzi,” alisema Nkonya.
0 comments:
Post a Comment