Kipindi
cha nyuma kidogo niliwahi kuandika makala juu ya umuhimu wa kila mmoja
kuwa na marafiki. Katika makala hayo nilisema wazi kwamba, kuishi bila
marafiki ni tatizo na ukijaribu kufuatilia wale ambao hawana marafiki,
maisha yao yana upungufu.
Nikashauri kwamba, ili maisha yako
yakamilike ni vyema ukachagua marafiki ambao watakuwa ni wenye faida
kwako. Lakini wakati nikishauri hivyo, wapo watu ambao naona wazi maisha
yao hayana dira, wapo wapo tu kwa sababu ya aina ya watu ambao
wamechagua wawe marafiki zao.
Unapochagua mtu wa kumfanya awe rafiki
yako, ina maana umeona mnaendana katika mambo mbalimbali. Huwezi
kumfanya mtu f’lani awe rafiki yako wakati unajua yeye ni mlevi na wewe
si mlevi. Yeye ni mwizi, wewe hupendi kuwa hivyo! Ukiwa karibu na mtu
huyo, ni rahisi sana kujiingiza huko.
Ndiyo maana ukifuatilia sana utagundua
vijana wengi wanaojifundisha tabia za wizi na uvutaji bangi walianza kwa
kujiweka karibu na marafiki wenye tabia hizo. Hiyo ni ishara tosha
kwamba, usipokuwa makini kwenye kuchagua rafiki, usishangae maisha yako
yakawa mabaya, tofauti na vile ulivyokuwa unafikiri.
Nimelazimika kulizungumzia hili kwa
sababu nimegundua wengi wetu tunashindwa kuyafikia mafanikio
tunayotakiwa kuwa nayo kwa kuwa na marafiki wabaya ambao hugeuka kuwa
vikwazo.
Hebu fikiria, unakuwa na rafiki ambaye
siku zote pesa zake zinaishia kwenye anasa. Yaani kila ikifika mwisho wa
mwezi anakushawishi muende kwenye kumbi za starehe, kunywa pombe kwa
sana na mambo mengine ambayo yamekuwa yakiwarudisha nyuma wengi.
Kama ulikuwa hujui, rafiki uliyenaye
ambaye hawazi mambo ya kimaendeleo anakuathiri kwa kiwango kikubwa sana.
Yawezekana mafanikio uliyonayo leo yangekuwa mara mbili yake kama
ungechagua marafiki wengine tofauti na hao ulionao sasa!
Ni wangapi unaowajua wewe ambao walikuwa
si walevi kivile lakini baada ya kuwa na marafiki wenye hulka hiyo nao
wakatopea huko? Ni wanawake wangapi unaowajua ambao huko nyuma walikuwa
wametulia lakini baada ya kuwa na marafiki micharuko nao wakawa
walewale?
Ni wengi sana ambao wameathiriwa na marafiki zao na hili linatokana na kutokuwa makini na aina ya watu wa kuwa nao karibu.
Wapo watu ambao wana aleji na mafanikio,
wakipata pesa wao wanatumbua tu, wala hawafikirii kwamba kuna kesho.
Hawa ni wale wanaoishi kwa kufuata ile misemo ya kijinga kama vile,
tumia pesa ikuzoee au wale ambao kila siku wanafikiria kujenga heshima
baa.
Hivi wewe ambaye unasoma makala haya
unadhani ukiwa na rafiki wa dizaini hiyo utaweza kujitoa kwenye mawazo
hayo? Hakika ni ngumu, labda Mungu akupe ujasiri wa kujinasua kutoka kwa
marafiki wenye akili hizo finyu.
Ndiyo maana nasema, marafiki ni muhimu
sana kwenye maisha yako lakini uangalie yupi anafaa na yupi ambaye ukiwa
naye karibu atakulostisha!
Ni vyema leo hii ukawafanyia uchambuzi
marafiki zako ulionao na kuangalia kama wamekuwa na faida au wamekuwa
chanzo ya kuyafanya maisha yako yawe hayana mbele wala nyuma.
0 comments:
Post a Comment