Tuesday, June 30


Hatimaye marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa wameungana na wajumbe wenzao wa Baraza la Ushauri la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanza kuwajadili makada waliojitokeza kuwania urais na kutoa ushauri utakaowezesha kupatikana kwa njia bora za kumpata mgombea wa chama hicho.

Tayari vikao vya baraza hilo vilivyokuwa vikisubiriwa kwa hamu vimeshaanza na leo vinaingia katika siku yake ya tatu, kwenye ofisi moja nyeti jijini Dar es Salaam.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya baraza la wazee hao zinaarifu kuwa vikao hivyo vina umuhimu wa pekee katika mchakato huo na kwamba vimepewa eneo tulivu na lenye usalama wa hali ya juu.

"Kikao kimeanza hapa (anataja ofisi) tangu juzi (Jumamosi) na hivi sasa bado tunaendelea,” kilieleza chanzo  kimoja  toka  ndani  ya  kikao  hicho.

Katika hali inayoonyesha umuhimu wa ushauri wa baraza hilo, chanzo hicho kinasema, “tuombe Mungu ili yanayoazimiwa na wazee wetu yakamilike na kuweza kukipa sura mpya chama chetu (CCM).”

Hata hivyo, taarifa nyingine kutoka ndani ya CCM zinaeleza kuwa hivi sasa baraza hilo linapewa umuhimu mkubwa kutokana na hali ya ‘mnyukano’ unaowahusisha wanasiasa wakongwe wakiwamo waliotegemewa kutoa ushauri ili kivuke salama katika mchakato unaohusu Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25 ili hatimaye apatikane mrithi wa Rais Jakaya Kikwete kwa nafasi ya urais na uenyekiti wa CCM.

Awali, kikao cha wazee hao kilikuwa kifanyike Jumatano iliyopita lakini kiliahirishwa na katibu wake, Pius Msekwa, kutokana na kile alichokieleza kuwa ni baadhi ya wajumbe kuwa safarini.

Wazee hao, pamoja na mambo mengine kuhusiana na uchaguzi, wanakutana kujadili mwenendo wa mbio za urais ndani ya CCM ikiwa ni siku chache kabla ya kufikia Julai 2, mwaka huu, ikiwa ni siku ya mwisho ya kurejesha fomu kwa wanaowania urais kupitia chama hicho. 
 
Hadi kufikia jana, makada 42 wa chama hicho walijitokeza na kuchukua fomu za kuwania kuteuliwa kuwa wagombea urais wa CCM katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25.

Mbali na marais wastaafu Mwinyi na Mkapa, wengine wanaounda Baraza la Ushauri la Wazee kwa mujibu wa mabadiliko yaliyofanywa na CCM mwaka 2012 katika katiba yake ni marais wastaafu Mwinyi (Mwenyekiti), Mkapa (Mjumbe), Amani Abeid Karume (Mjumbe) na Dk. Salmin Amour (Mjumbe).

Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais, John Malecela (mjumbe) na Pius Msekwa (Katibu).
Credit: Nipashe
Mpekuzi blog

0 comments:

-