JUA lilikuwa linakuchwa taratibu katika maeneo haya ya milima ya
Uluguru pande za Mgeta. Maeneo ya Lukwangule tayari yalishapoteza nuru
yake ya mchana na kiza kilikuwa kimejivuta kama bibi kizee.
Wakati maeneo hayo kiza kinajivuta maeneo ya kijiji cha lusungi yalikuwa bado yanachechemea na mwanga kidogo uliokuwa unavuka.
kuku
wote walishaingia katika mabanda yao, wakiwa wametulia tayari kupitisha
usiku mwingine tulivu. wanyama wa usiku taratibu walianza kutoka katika
maficho yao, bundi mmoja akaanza kulia.
Katika nyumba moja
mama kuku alikuwa anahesabu watoto wake huku analia,mbuzi katika mabanda
walikuwa wanacheua na kondoo nao pia, walikuwa wameshafunguliwa makopo
midomoni mwao na wametulia huku beberu mmoja mgomvi akiwa ametiwa kamba
sawia.
Msichana mmoja mweusi wa wastani, mrefu na ambaye
alikuwa na umbile la nane, akiwa na mfuko wake mgongoni alikuwa
anatembea taratibu katika barabara inayoelekea Bumu. Njiani alikuwa peke
yake, lakini alikuwa anashika kasi ya mtu ambaye hakuwa na mazoea ya
milima au ambaye ni mgonjwa.
Mwenda binti pekee kwa baba na
mama Mwenda alikuwa ameondoka nchini miaka saba iliyopita kwenda kusomea
udaktari nchini Russia. Baada ya kupata vyeti vyake alikuwa na kila
sababu ya kurejea nyumbani na kuungana na watu wake. Alikuwa amewamisi
wazazi wake ambao alikuwa na mazoea ya kuwaandikia barua lakini wenyewe
walikuwa na mazoea ya kutomjibu.
Alijua kwanini hawataki
kumjibu. Walimweleza mapema kwamba wanaomba awatumie salamu kila mara
lakini wao hawataweza kujibu kwa sababu za kiusalama.Walimwambia kwamba
baba yake mdogo alikufa kwa namna ya ajabu nchini Canada baada ya kusoma
barua iliyotoka nyumbani akidhani inatoka kwa ndugu zake.
Mzee mmoja mchawi alimuua ndugu yao na akatamba kijiji kizima kwamba amewapatia na hilo hawatakaa walisahau maisha yao yote.
Aliingia
Dar es salaam saa nne akitokea Nairobi, Kenya ambako aliunga ndege
yake. Aliunga mara nyingi sana usafiri wake kwani alipotoka Moscow,
alifika Addis Ababa, Ethiopia ambako alikaa kwa siku nzima kabla ya
kusafirishwa na Ethiopia Airline na kushushwa Nairobi kenya ambako
alichukua Kenya Airways na kutua uwanja wa ndege wa Dar es salaam saa
nne asubuhi.
Mpaka saa saba alikuwa amefika kwa ndugu yake
Magomeni Mikumi katika nyumba ya Uyeka. Aliketi kwa muda kabla ya
kuondoka kwenda kutafuta usafiri wa Morogoro . Pale kwa shangazi yake
Magomeni nusura asiondoke baada ya kukutana na wadogo zake ambao
walishakua wakubwa wakimshangaashangaa.Lakini alipiga moyo konde hasa
baada ya kuelezwa kuwa wazazi wake hawakuwa katika hali nzuri sana
inafaa kwenda kuwaona.
Saba nusu, pale Magomeni mapipa alikuwa
abiria wa mwisho katika Double Coaster moja ambayo haikubeba abiria
tena mpaka inaingia morogoro saa kumi na nusu. Alifikiria sana kwenda
gesti kulala lakini aliamua kufanya kitu kimoja cha maana cha kwenda
katika soko la Morogoro kuona kama hakuna lori linalopandisha kwenda
kwao Mgeta.
Binti huyu bahati ilikuwa kwake, kwani anatia mguu
tu akaliona lori ambalo lilikwishapakia pumba na mabati likiwa tayari
kuondoka.
"Vipi mnapanda mlimani?"
"Ndio bibiye unataka usafiri?"
"Ndio kama inawezekana"
"Utakuwa mwanamke peke yako huko nyuma manake mbele kumejaa."
"Wala usijali, mpaka Lolo bei gani?"
"Mpaka Lolo? Lolo ndio wapi Hading'oka"
"Ndio Madukani kwani wewe hupajui?"
"Nimechemsha kila mara inakuwa taabu kukumbuka.mama wewe ingia tu tutaelewana sisi binadamu."
"Ninaweza kuwa sina hela hiyo?"
"Huonekani
kama huna hiyo hela nitakayoihitaji. nataka shilingi 1,500 tu"alisema
dereva na kisha akamhimiza apande kwani anataka kuingia bado kweupe.
Alifika
Lolo lakini hakushuka, kwa kuwa lori lilikuwa alinaelekea Tchenzema,
akashukia visomoro ndipo alipoanza taratibu hatua za kurejea kwao, huku
fikira zikimuumiza.
Atawakuta namna gani watu wake na watakuwa vipi. Alikumbuka wadogo zake kutoka kwa mama mdogo wake hakujua atawakuta vipi.
Lakini
kule nyumbani Baba yake alikuwa amelala akiwa mgonjwa na mama yake
alikuwa anahangaika kufanya hiki na kile ili kusawazisha mambo kabla ya
kuanza kumhudumia mgonjwa wake.
kama vile mtu aliyekwisha
choka mawazo ya mtoto wake wa pekee yalikuwa yakimjia. Alifikiria mtoto
wake kwa miaka saba hajawahi kumtia machoni, watu walikuwa wanamdhihaki
na ndugu wa mume walikuwa wameacha kumsaidia ndugu yao zamani kabisa na
juhudi kubwa ilibaki kwake yeye ambaye ndiye mke.
Kazi za
shamba, kazi za kilimo, kazi za kutunza mifugo hazikuwa na msaidizi
kwani hata wale walio wadogo wanaonekana kama wameambiwa wasifike pale,
alikuwa anaonekana mchawi anamloga mume wake.
Mama Mwenda
hakuwa na muda wa kumsaida mume wake kwa kipindi kile cha jioni ilikuwa
lazima akimbizane na kutwanga kwanza kabla hajampatia chakula mgonjwa
wake ambaye hakuonyesha hata dalili za kupona katika ugonjwa wake.
Siku
ile alimaliza kutwanga mapema akampikia mumewe na baada ya kumkanda kwa
maji ya uvuguvugu alimnyanyua na kumsaidia kumlisha. Alipoona mgonjwa
wake yupo safi naye akala na kisha kuanza kujiandaa kwa usiku.
Wakati anafunga mlango kwa kuweka michi na kinu alisikia hodi ambayo alidhani kwamba ni kichaa chake.
Hodi
ilirejewa tena na tena na mwisho wake akaamua kuchungulia hakuamini
aliyemuona pale ndani na badala ya kumfungulia mlango akakimbilia kwa
mume wake.
"Baba Mwenda, mwenda amerudi" alisema huku akiwa anashangilia.
"Yupo wapi?" aliuliza mzee kwa sauti ya taabu.
"Yupo nje"
"Sasa si kiza kimeingia unawezaje kumwacha nje"
"Ohh
Mungu ashukuriwe" alikimbilia nje na kuanza kutoa vifaa alivyoweka
mlangoni, akafungua mlango na kumkumbatia mwanawe kwa muda mrefu sana
kabla ya kumsalimia na kumtazmaa kila mahali katika mwili wake.
"Mhh mama hujaacha tu kunikagua kote huko?"
"Mwanangu sijakuona muda gani?"
"Si
hivi nipo mama." alisema akitabasamu alikuwa anamjua mama yake huwa
anamkagua hata akitoka shule.Alikuwa na kawaida hiyo kiasi ya kwamba
alikuwa wakati mwingine anamuona mama yake kuwa kero.
" Wooh
umekuwa na rangi gani sasa manake bluu si bluu , weusi si weusi rangi
gani hii" alisema huku akimpokea begi kubwa mgongoni na kwenda kuiweka
katika chanja ambayo ilitengenezwa vyema kwa ajili ya kuwekea
mizigo.
Aliitazama
nyumba yao, nyumba iliyomlea. Alitaka kuibadili kama watu wengine
walivyobadili nyumba za wazazi wao. Alikuwa ameona nyumba nyingi zikiwa
zimejengwa pau na wala si misonge kama ya kwao ingawa ilijengwa vyema.
Ilikuwa
nyumba ambayo ina chumba tatu, chumba cha ndani ambacho ni jiko ambako
kila mara alikuwa akihimizwa kulala humo kutokana na joto lake, chumba
cha wazazi wake ambacho kilikuwa karibu na zizi la kuku na mbuzi na
kondooo na kingine ambacho kilikuwa na mwanga na safi kwa ajili ya
wageni.
Alikumbuka kitanda chake cha teremka
tukaze ambacho baba yake alikuwa amemnunulia godoro la sufu baada ya
kupata nafasi ya kwenda shule ya sekondari ya Kilakala kutoka
Bumu.Ilikuwa taabu kidogo kukumbuka kama mto wake ulikuwa upo au la.
"Mhh
nambie hali ya baba mama" alisema huku akiwa amekaa katika kiti cha
fito kilichokuwa katika sebule ya nyumba yao hiyo ya msonge.Alikuwa ni
miongoni mwa watoto ambao hawakuwa wanadeka, alikuwa amechangamka na
mama yake lakini kitendo cha kutomuona baba yake pale akitoka kumuona
kilimpa shida kidogo, alitarajia habari mbaya manake miaka saba si
sawasawa.
"Baba yako yupo ndani hali yetu si sawasawa
mwanangu" alisema kwa huzuni kisha akaanza kumweleza taabu ilianza
kukohoa na ilipofika kukohoa damu wote waliwakimbia.
"Unaponiona
hapa sina la kufanya, hatuna hela, hatuna dawa nimekuwa nikihangaika na
mibaazi mpaka sasa tupo tu. baba zako wamenikimbia mimi sasa ndiye
muuguzaji." alisema huku anadondosha machozi.
Mwenda aliamka
na kwenda kumkumbatia mama yake na kisha akaongoza mahali ambapo alijua
lazima baba yake yupo, chumba cha kati ambacho huwashwa moto.Kweli
alimkuta baba yake.
Hali ya baba yake ilimtisha.
Alimsalimia na kumuitikia kwa taabu kubwa.
Haikuwa rahisi kuelewa kama anamsikia vyema baba yake au la. Akakimbilia kumbariki kisha akatulia sana.
"Mama ilianza lini?"
"Tunamwaka mmoja" alitulia.
Alimwangalia akatazama mapigo yake kisha akatoka na kukimbilia begi lake.
Ilikuwa taabu kubwa katika moyo wake, alijua baba yake ana kifua kikuu na huenda naye mama yake ana kifua kikuu pia.
Alienda kuchukua vidonge vya kutuliza maumivu na saplimenti za vitamini.
"Mama baba anakula?" alimuuliza mama yake wakati anaingia tena katika chumba kile.
"Bado anaweza kula japo kwa taabu."
"Basi mpe dawa hizi na kikopo hiki akikohoa tia mate yake." alisema.
"Yanini mama?" aliisikia sauti yake dhaifu.
"Kesho asubuhi asubuhi nataka kwenda kituo cha Afya Mgeta nijue nini."
"Mtaalamu amesema wamemroga kwa sababu wewe upo Ulaya" alisema mama mtu
"Inawezekana mama lakini pia inawezekana baba ana kifua kikuu ndio maana ukimpa mibaazi inatulia"
"Haya
mama" alisema mama yake na kisha akachukua vidonge vile na kuhangaika
kumpa mgonjwa na baada ya kumaliza kumpa alikohoa lakini hakutoa damu
badaaye alipokohoa alitwaa makohozi na kuona yanadamu na kohosi la
kawaida.
Bila hata kujiuliza swali mwenda alitambua kwamba
nafasi ya baba yake kupona ni hamsini hamsini, kifua kikuu kilikuwa
kimetafuna sana....
Kwa leo kwaheri tutaonana Jumatatu ijayo kwa mwendelezo
0 comments:
Post a Comment