Wednesday, August 13

LEO Agosti 13, ni siku ya Mashoto Duniani (International Lefthanders Day). Siku hii imekuwa ikisherehekewa kila mwaka toka Agosti 13, 1976 pale chama cha Mashoto (Lefthanders International) kilipoitangaza siku hii kuwa maalumu kuwathamini mashoto ambao wanatengeneza asilimia 10 hadi 15 ya idadi ya watu ulimwenguni huku idadi ya wanaume mashoto ikielezwa kuwa mara mbili ya idadi ya wanawake mashoto. Madhumuni ya siku hii ni kuwakutanisha mashoto sehemu mbalimbali duniani na kufurahia upekee wao. Lakini pia siku hii inalengwa kuifahamisha dunia juu ya ukweli kuhusu mashoto.

Kabla sijaendelea na makala haya, naomba kukiri (declaring interest) kuwa mimi ni mashoto pia. Ninajivunia kuwa mashoto. Lakini pamoja na kuwa kwangu mashoto, haya ninayoyaandika katika makala haya siyaandiki kwa ufahamu wangu, bali kutokana na maandiko kadha wa kadha ambayo nimeyasoma na kuyakusanya kutoka vyanzo mbalimbali.

Mila potofu kuhusu mashoto
Kwa miaka mingi, jamii nyingi zimekuwa na mila potofu kuhusiana na mashoto. Wengi wamekuwa wakiita mkono wa kushoto kama mkono wa shetani. Jamii nyingi zimekuwa na kawaida ya kulazimisha kuwabadili watoto wao mkono wa kutumia pindi wagunduapo watoto hao ni mashoto. Jamii hizo zimekuwa zikiamini kuwa mashoto ni ulemavu ama mkosi.

Majina mengi mabaya yamekuwa yakitumiwa kwa miaka mingi yakionesha kuwadharau mashoto. Kwa mfano, hapa Tanzania mkono huo umekuwa ukiitwa ‘kono la mavi’. Katika Kilatini, mkono wa kushoto umekuwa ukitwa ‘sinitra’ ambayo humaanisha kitu kiovu.

Kumekuwa na imani kuwa mashoto wengi hukumbwa na vifo vya ajali. Lakini watafiti wamesema kuhusu hilo. Wanakiri kuwa mashoto wengi hukumbwa na ajali kutokana na ukweli vitu vyote vimetengenezwa kwa ajili ya matumizi ya mkono wa kulia. Mathalani, vyombo vya moto na vyombo vingine vya matumizi ya kila siku vinawapa upendeleo wanaotumia mkono wa kulia. Kwa maana hiyo mashoto hulazimika kufoji matumizi.

Jamii zingine kwa miaka mingi zimekuwa zikiamini kuwa mashoto hukumbwa na vifo vya ajabu ajabu.

Mtazamo chanya kuhusu mashoto
Huko Peru, Amerika ya Kusini, kwenye jamii ya Inca, mashoto wanaaminiwa kuwa na uwezo mkubwa sana kiroho na uponyaji. Mtawala wa tatu wa jamii hiyo aliyekuwa mashoto alipewa jina la Lloque Yupanqui likiwa na maana ‘Mashoto aliyebarikiwa’.

Katika Ubudha, mashoto huhesabiwa ni wenye hekima zaidi.

Huko Urusi, mashoto ambao huitwa ‘Levsha’ huhesabiwa kuwa ni mafundi stadi zaidi wa kazi za mikono.

Uchina na Ujapani, mashoto huhesabiwa kuwa ni wabunifu na wachapa kazi zaidi.

Ukweli kuhusu mashoto
Sababu za msingi hasa kwa nini watu huzaliwa mashoto hazijawa wazi hadi sasa. Lakini watafiti wengi wanasema mashoto hutokana na vinasaba (genetics) na sababu za kimazingira. Inaelezwa kuwa wazazi wote wawili wakiwa mashoto, upo uwezekano wa asilimia 50 kuzaa mashoto, wakati wazazi wote wawili kama si mashoto, wana uwezekano wa asilimia 2 kuzaa mashoto.

Mashoto, kwa mujibu wa utafiti, huongozwa zaidi na upande wa kulia wa ubongo, wakati wanaotumia kulia huongozwa zaidi na upande wa kushoto wa ubongo. Kwa kuwa mashoto huongozwa na upande wa kulia, watafiti wanasema mashoto ni watu wenye uwezo mkubwa zaidi kiakili. Pia wana uwezo mkubwa zaidi katika sanaa, muziki na ubunifu kwa ujumla. Mashoto wanaelezwa kuwa na uwezo mkubwa sana wa utambuzi (perception). Watafiti wanaeleza pia kuwa mashoto wana mhemuko, mchomo wa moyo ama hisia (emotions) kwa kiasi kikubwa zaidi. Hivyo mashoto wanaelezwa ni watu wenye upendo na huruma kwa kiwango cha hali ya juu sana.

Kwa mujibu wa utafiti wa Dr. Alan Searleman wa Chuo Kikuu cha Mt. Lawrence huko New York, Marekani, mashoto wana uwezo mkubwa zaidi wa utatuzi (problem-solving skills).

Mashoto wana uwezo mkubwa sana wa kutunza kumbukumbu kiasi kwamba wengi wao hawatumii shajara (diary) na hawapendi kutumia notebooks wanapomsikiliza mtu akitoa mhadhara.

Mashoto wana mzio (allergies) zaidi.

Mashoto wana tatizo la kukosa usingizi (insomnia) zaidi.

Mashoto huchelewa kupevuka ama kubalehe kwa miezi 4 hadi 5 ukilinganisha na wanaotumia kulia.

Mashoto wana uwezo mkubwa zaidi wa kufikiria na kutambua mambo hususani katika teknolojia ya 3D. Wanao upeo mkubwa sana.

Mashoto wana uwezo mkubwa zaidi wa kufanya mambo mengi sana (multi tasking). Utafiti wa Dr. Nick Cherbuin wa Chuo Kikuu cha London unaonesha kuwa mashoto wana uwezo mkubwa zaidi wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja na ndiyo sababu ni wazuri zaidi hata kwenye video games.

Mashoto wana vipaji vingi zaidi. Mashoto mmoja anaweza kuwa mchoraji, mshairi, mcheza mpira, mchonga vinyago, mwandishi wa hadithi, mbunifu wa mitindo, mbunifu wa bustani, mcheza filamu, mpigapicha, mpambaji, mwanamuziki na vingine vingi.

Wastani wa umri wa kuishi wa mashoto ni miaka 9 pungufu ya wastani wa wanaotumia mkono wa kulia.

Mashoto wana uwezo mkubwa zaidi wa kuona chini ya maji.

Mashoto waliopo vyuoni hufanikiwa kwa asilimia 15 zaidi ya wanaotumia kulia. Na baada ya kumaliza vyuo, mashoto huwa na mafanikio kwa asilimia 26 zaidi ya wengine. Mtafiti Chris McManus katika kitabu chake cha ‘Right Hand, Left Hand’ amesema kuwa mashoto wameonesha kuwa ni watu wenye mafanikio kwa kiwango kikubwa zaidi.

Mashoto wengi baada ya masomo hufanya kazi za ubunifu zaidi kama uandishi, ushairi, muziki, uigizaji na sanaa yote kwa ujumla. Hata wanaofanya kazi zingine, huwa ni wenye kupenda ubunifu zaidi katika kufanikisha kazi zao.

Katika wabunifu watano wa kwanza wa kompyuta za Mcintosh, wanne kati yao walikuwa mashoto.

Mashoto ni wachoraji wazuri zaidi, lakini huchora michoro mingi ikiwa imeelekea upande wa kulia.

Katika marais wanne wa hivi karibuni wa Marekani, marais watatu ni mashoto. Tazama, George Bush mkubwa (mashoto), Bill Clinton (mashoto), George Bush mdogo (kulia) na Barack Obama (mashoto). Na, katika uchaguzi wa urais wa Marekani wa 1992, wagombea wote watatu wakubwa walikuwa mashoto. Uchaguzi wa Marekani wa 2008, wagombea wote wawili Obama na McCain ni mashoto.

Katika keyboards za QWERTY, mkono wa kushoto peke yake huweza kuchapa maneno 3400 ya Kingereza wakati mkono wa kulia peke yake huweza kuchapa maneno 450 tu ya Kingereza. Mfano wa maneno marefu ya Kingereza ambayo huchapwa na mkono wa kushoto peke yake katika kibodi ya QWERTY ni; desegregates, reverberated, watercress, aftereffects, na pia sweaterdresses.

Mashoto wana miandiko (handwriting) mizuri na yenye kuvutia mno. Na wanao uwezo mkubwa wa kuandika maandishi (herufi na tarakimu) kwa kinyume (toka kulia kwenda kushoto)

Mashoto wanapenda zaidi wanyama. Jambo la kusisimua ni kuwa dubu (bear) wote ni mashoto. Mashoto wa kiume huwapenda sana paka, na jambo la kushangaza zaidi paka wote wa kiume ni mashoto. (Naomba kukiri kuwa hili jambo linanihusu).

Asilimia 50 ya mashoto hutumia mouse za kompyuta kwa mkono wa kulia, asilimia 68 hushika mkasi kwa mkono wa kulia, na asilimia 74 hushika kitu cha chakula kwa mkono wa kulia na uma kwa mkono wa kushoto.

Watafiti wa Kikanada wanasema mashoto wanamudu kwa kiasi kikubwa zaidi kuyazowea mazingira yoyote yale. Ingawa vitu vingi vya utumizi kama milango, magitaa, visu, mikasi, magari na kadhalika vimewapendelea wanaotumia mkono wa kulia, ni mashoto ndio wanaovimudu zaidi.

Mashoto wanajiamini zaidi na ni majasiri zaidi.

Baadhi ya watu mashuhuri ambao ni mashoto
Marais wa Marekani: James A. Garfield, Herbet Hoover, Harry S. Truman, Gelard Ford, Ronald Reagan, George H. W. Bush, Bill Clinton na Barack Obama.

Watu maarufu katika historia: Joan of Arc, Napoleon Bonaparte, Julius Caesar, Michelangelo, Leonardo da Vinci, Raphael na Hellen Keller, Alexander The Great, Malkia Victoria, Mfalme George II, Mfalme George VI, Prince Charles, Prince William, Henry Ford, Benjamin Franklin, Steven Forbes na Oprah Winfrey.

Wanasiasa maarufu: Benard Membe, Fidel Castro, Ross Perot, Bob Dole, John McCain, Robert S. McNamara, Benjamin Netanyahu, Ehud Olmert na Brig. Jen. Lee Hsien Loon.

Wanamuziki maarufu: Phil Collins, Paul McCartney, Ringo Starr, Jimi Hendrix na George Michael.

Waandishi na washairi:
James Baldwin, Bet Bowen, Samuel C. Warner, Viktoria Stefanov, Diane Paul na Richard Condon.

Wacheza filamu: Charlie Chaplin, Tom Cruise, Robert de Niro, Whoopie Goldberg, Bruce Willis, Kadeem Hadson, Angelina Jolie, Marilyn Monroe, Nicole Kidman, Cary Grant, Julia Roberts,

Wacheza soka maarufu: Pele, Diego Armando Maradona, Romario na Hugo Sanchez.

Hayo ndiyo niliyoweza kukusanya kuhusu mashoto kutoka katika machapisho mbalimbali.

Natuma salamu zangu za upendo kwa mashoto wote ulimwenguni.

Heri ya siku ya mashoto duniani.

0 comments:

-