Friday, September 20

Ni Jumatano nyingine tena tunakutana katika safu yetu nzuri ya kubadilishana mawazo juu ya uhusiano na wapenzi wetu. Ni imani yangu kwamba utakuwa mzima wa afya njema huku gurudumu la maisha likisonga kama kawaida.

Rafiki zangu wapenzi, Jumatano ya wiki iliyopita, nilipokea simu kutoka kwa msomaji mmoja usiku sana. Alisema aliguswa sana na mada zangu hasa ya siku ile, lakini alikuwa na matatizo ambayo alihitaji kupatiwa ushauri.

Katika mazungumzo nami, msomaji wangu huyo ambaye ni mwanamke (nitaficha jina lake) alisema yupo kwenye uhusiano na mwanaume ambaye kwake ni kero. Alisema, mpenzi wake huyo ana umri wa zaidi ya miaka 45 na yeye ana miaka 34, wakiwa katika uhusiano huo kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Hata hivyo, alisema tatizo kubwa linaloyumbisha uhusiano wao ni kitendo cha mwanaume huyo, kuwa na tabia za kuwatongoza wadogo zake (wa kike) ambao anaishi nao nyumbani kwake. Baada ya kero hizo kuzidi, dada huyo aliona ni bora kuachana naye. Akamweleza mwanaume huyo msimamo wake na kuachana.

Kilichomfaya anipigie simu ni juu ya mwanaume huyo kumsumbua kila wakati, akitaka warudiane. Amekuwa akiomba msamaha na kuahidi kwamba hatarudia tena. Alisema, hii siyo mara yake ya kwanza, kwani mara nyingi amekuwa akiwatongoza hata rafiki zake wa karibu na akishtukia mchezo, kazi yake imekuwa kuomba msamaha akiahidi kutorudia lakini baada ya muda, hadithi inabaki kuwa ile ile!

Kinachomuuma zaidi ni kwamba, amejikuta akimpenda sana mwanaume huyo na anashindwa kabisa kumuondoa kichwani mwake. Nilizungumza naye juu ya tatizo lake, lakini niliona yawezekana kabisa kuna wengine wengi wenye tatizo kama lake, lakini hawajui cha kufanya.

Dada na kaka zangu, hapa nitakupa njia madhubuti za kutumia ili uweze kukabiliana na tatizo hilo katika uhusiano wako.
Je, wewe ni mwanaume/mwanamke ambaye upo katika uhusiano na mpenzi ambaye haishi kuwatongoza rafiki, ndugu au watu wako wa karibu? Vipengele vifuatavyo ni dawa tosha kwako...

ANAWEZA KUBADILIKA?
Siku zote katika uhusiano wowote ule, suala la msamaha ni jema na lenye nafasi kubwa ya kuboresha uhusiano, lakini kabla ya kuchukua hatua ya kusamehe ni lazima ujiulize, anaweza kubadilika?

Hili linaweza kuthibitishwa na historia yake ya nyuma. Haiwezekani ikawa ndiyo mara yake ya kwanza kukosea, lazima atakuwa ameshakukosea mara nyingie huko nyuma. Je, hili ni kosa lake la kwanza? Alivyokosea huko nyuma aliomba msamaha?
Kama aliomba, alirudia tena? Maana kama mtu anakosea kosa lile lile zaidi ya mara tatu na anaomba msamaha akiahidi kubadilika na habadiliki, ujue kwamba si rahisi kubadilika tena! Lazima ujiridhishe kwamba ni kweli atabadilika na hatarudia tena. Kama nilivyosema hapo juu, utapata ukweli huu kupitia historia yake ya nyuma!

MAKOSA NA UMRI
Rafiki zangu, kuna aina ya makosa fulani, ukishavuka umri fulani unakuwa huwezi kuyafanya tena, kwa mfano, kesi za kwenda disko na demu mwingine, kwa mwanaume wa miaka 45 huwezi kuzisikia tena. Sasa hata katika hili, lazima uangalie umri wake kama unafanana na kosa lake.

Unajua, kuna tabia nyingine hubadilishwa na wapenzi na nyingine ni za kuzaliwa ambazo kwa hakika huwezi kufanya mabadiliko. Suala la kubadilisha wapenzi, linaonekana kuwa fasheni zaidi kwa vijana, lakini kama umri wake umeshasonga na bado akawa na tabia hizo, ujue kwamba hiyo ni tabia yake ya asili ambayo haibadilishiki!

Mwanaume wa miaka 52 bado unakimbikizana na ‘vitoto’ vidogo, lazima kuna tatizo. Wataalamu wa Saikolojia ya Uhusiano na Mapenzi wanaamini wanaume wenye uwezo wa kuwa na familia bora na kuisimamia vyema ni wale wenye zaidi ya miaka 35, kwamba atakuwa ameshapitia mambo mengi na sasa anatamani kuwa baba tu! Msimamizi wa familia.

Fungua ubongo wako, msimamizi wa familia hawezi kuwa malaya, anatakiwa awe mwenye kujiheshimu. Huyu anafaaa? Wa nini? Akili kichwani mwako.
NI MWENZI SAHIHI?
Lakini pia, kabla hujachukua uamuzi wa kuachana naye, lazima ujiulize swali hilo hapo juu, ni mwenzi sahihi? Lazima awe na sifa zitakazomfanya apewe kofia ya mwenzi sahihi.

Rafiki zangu wapenzi, kutokana na ufinyu wa nafasi, naomba kuishia hapo kwa leo, nikikusihi usikose wiki ijayo katika sehemu ya mwisho ya mada hii ambapo nitafafanua sifa za mwenzi sahihi pamoja na suluhisho la mwisho la kukabiliana na tatizo hili.
Nakuacha na ujumbe mmoja muhimu zaidi, ni vyema kuwa makini sana na wenzi wetu, tuache kuamini na kusikiliza sana moyo, kwani wakati mwingine, huweza kukutumbukiza kwenye moto. Hata kama unampenda kiasi gani, lakini ana matatizo ambayo yanakulazimisha uachane naye. Kwanini unamng’ang’ania?

KESHO tutaendelea....

0 comments:

-