Sunday, September 22

NAAM tumekutana tena kwenye kona ya mahaba ili kujuzana machache, hali yangu ni buheri wa afya sijui ninyi wenzangu. Kama ilivyo ada tunaendelea na mada nyingine ili tujue tumejikwaa wapi na wapi tuelekee.
Leo najua una hamu ya kujua nimekuja na mada gani, kwa vile madhumuni makubwa ya kona hii ni kukumbushana na kurekebishana hasa pale mtu anapokuwa amekwenda kinyume kwa kujisahau au kwa kutojua.

Katika mada ya leo nitazungumzia suala la kujipamba kwa wanaume kupita kiasi, si jambo geni kwa wanaume kujipamba ili waonekane maridadi mbele ya macho ya watu. Kama kutumia manukato ya kunukia na mafuta ya kulainisha ngozi.
Lazima tukubali mapambo ya mwanamke yana tofauti hata jinsi ya kujipamba ina tofauti kubwa. Lakini kumezuka mtindo wa kuiga kila kitu bila kuangalia mila na destuli zetu.

Kwa sasa imekuwa kazi kubwa kumtambua mara moja mwanamke au mwanaume kutokana na wanaume hasa vijana kuvamia mapambo ya kike.
Sasa hivi vijana wanajipaka mikorogo kutoga masikio zaidi ya tundu tatu, kusuka nywele kutoga midomo hata ulimi. Unajiuliza tatizo nini kipi kimepungua katika uanaume wako mpaka kujifananisha na mwanamke, unaamini kabisa wanaume wenye tabia hizo toka awali ni mashoga.

Kwa nini ifikie hatua watu wakufikirie vibaya kutokana na kujipamba kwako? Je utamaduni huo umeurithi toka wapi? Baba au babu yako amefanya hivyo?. Ni vitu ambavyo naweza kusema wazazi wamekuwa ndiyo chanzo cha mmomonyoko wa maadili kwa kuacha tatizo kuota mizizi.
Sawa zipo kabila ambazo zina utaratibu wa wanaume kusuka, wanawake kunyoa au wanaume kutoga masikio. hizo ndizo mila na destuli zao hakuna wa kuwashangaa. Leo hii kila kijana ambaye anaimba muziki wa kisasa mavazi yake na jinsi anavyojiweka ni tofauti na mila na destuli zetu.

Ajabu wazazi jambo lile wanalifumbia macho na wao kuona jambo la kawaida, nafikili ifike hatua wazazi wakubali kuwa wao ndiyo chanzo cha yote yanayoporomosha maadili yetu.
Napenda kuwaeleza vijana wote hata watu wazima ambao hutamani kila akifanyacho mwanamke na wao kufanya, ipo siku watavutiwa na kukuza matiti ili waende sambamba na mwanamke.
Lazima iwepo tofauti kati ya mwanamke na mwanaume katika mavazi, mapambo na pia muonekano. Tunajua mwanamke ni ua la dunia ameletwa ili kuipamba dunia na mwanaume ni kiongozi wake. Pia mwanamke anatakiwa kujipamba ili kumvuta mwanaume kama ua zuri kwa nyuki.

Leo hii mwanaume unajipamba ukisimamishwa na mwanamke kutofautisha inakuwa kazi. Unajipamba kama mwanamke una ajenda gani? Bado hujachelewa jiweke kama mwanaume ambaye akisimamishwa mbele ya wanaume akubalike, siyo watu wawe na mashaka na wewe.
Mfano mzuri ni kwa mzazi wako muangalie baba yako alivyo, Je anafanana na wewe unavyojiweka. Upende uanaume ili kuwa mwanaume kamili. Tuache kuiga bila kujua faida na hasara.

Kwa hayo machache tukutane kesho

0 comments:

-