Bila kupoteza muda tunaanza mara moja mada yetu, swali linakuja hivi Neno NAKUPENDA ni mapenzi kamili?
Nimeandika mada hii kutokana na watu wengi kushindwa kutofautisha neno nakupenda na mapenzi kamili. Wengi wameingia mkenge kwa neno hili hasa wageni katika uwanja huu wa mahaba. Ukiambiwa unapendwa basi unachanganyikiwa na kusahau maneno matupu hayajengi nyumba.
Nina maana gani?
Watu wengi wamekuwa wakitumia neno hili kama mtego wa kumpata mtu, kwa kujifanya anakupenda sana na nahau nyingi za mapenzi ambazo hukuziba masikio na kuona nani kama wewe.
Siku zote mtafutaji ana lugha tamu ya mapenzi na kabla ya kutamka lolote lazima atangulize nakupenda sana na kuongezea ajuavyo. Hii si mara moja watu wanaingia mkenge wanapoambiwa wanapendwa na kukubali mara moja bila kujiuliza.
Lazima uelewe serikali ya mwili wako inakutegemea wewe ukiipeleka vibaya ni wewe wa kulaumiwa. Usiwe na papara ya kutoa maamuzi ya kukubali uambiavyo unapendwa, hakuna hata siku moja mtu anayekutaka kimapenzi akuambie ANAKUCHUKIA.
Jaribu kufikiri kabla ya kutenda na kuona kauli hii ina nia gani na mimi kweli ananipenda au anataka kunichezea na kuniacha. Mwanadamu ana uamuzi tofauti na wanyama wanaotumia nguvu bila maafikiano.
Katika uchunguzi wangu nimegundua watu wengi hupima kwa macho ya kumuangalia alivyo. Na asemalo unashindwa kuchukua muda wa kufikiria na kutoa maamuzi ya pupa bila kuangalia maamuzi yako yana faida au hasara.
Neno nakupenda siyo mapenzi kamili bali tabia ya mtu na kuonyesha kweli anakupenda kwa dhati.
Na akupendae huwa hana haraka yakutanguliza kufanya ngono, hufuata taratibu zote ili mradi kujenga ukweli moyoni mwako. Na hii hutokana na kuwa na uhakika wewe ni wake, hana wasiwasi kwa kutanguliza ngono mbele. Lakini ukiona umekutana na mtu na kutanguliza ngono baada ya neno nakupenda huyo hakupendi bali anakutamani.
Tumekuwa tunatumia neno nakupenda kama kiwakilishi cha ujumbe wa mapenzi na siyo penzi kamili. Na mapenzi ya kweli ni ya vitendo na siyo maneno, anayekupenda utamjua tu wala hajifichi.
Ni mpole, mwenye hurum,a anayekujali, muaminifu na mtu aliye muwazi mwenye kukupa uhuru wa kumjua kwa undani ili kukuondoa wasiwasi. Mapenzi mengi ya siku hizi yamekuwa yenye usiri mkubwa yenye mipaka.
Kama kweli anakupenda kwa nini akudanganye? kwa nini akuwekee mipaka ya kumfahamu? Ukiona mpenzi wako msiri, si muwazi mwenye mipaka ya kumjua, lakini mdomoni kwake ana kila nahau tamu za kimapenzi na kulitamka neno NAKUPENDA kama kiwakilishi, huyo hakufahi.
Huyo si mkweli wala hana mapenzi ni muongo hana mapenzi ya kweli bali amejificha nyuma ya neno NAKUPENDA ili uamini kweli anakupenda. Kuwa macho na watu hao, sipendi kesho uniulize swali hili.
Kwa leo naamini nitakuwa nimeeleweka vizuri kwa machache haya, tukutane wiki ijayo.
0 comments:
Post a Comment