Friday, September 15

[​IMG]
Rais Kim Jong-un



Mwaka wa 2010 uliingia katika kumbukumbu za Korea Kaskazini baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Kim Jong-il kuzindua kombora lake ambalo wakakti wowote kuanzia sasa litafanyiwa majaribio.

Baada ya kifo cha rais Kim Jong-il , Desemba mwaka 2011 nchi hiyo ilikabidhiwa mikononi mwa mtoto wake Kim Jong-un aliyeelezwa kuwa na uwezo mkubwa wa kulingoza vyema taifa hilo.
Baada ya kuapishwa rasmi Aprili 2012 , Kim Jong-un alichukua jukumu hilo na kuzindua satellite iitwayo "rocket-mounted' kama sehemu ya kumbukumbu ya kuenzi siku ya kuzaliwa kwa babu yake ambaye ni muasisi wa taifa hilo Kim Il-Sung.

Msimamo wa kwanza wa Rais Kim Jong-un ulikuwa ni kupinga msaada wa chakula unaotoka Marekani ili kuondoa kifungo cha kufanya majaribio yake ya silaha za nyuklia.

Kwa sasa taifa hilo la kaskazini limeimarisha vitisho vyake kama hatua ya kujibu mazoezi makali ya kivita, yanayondeshwa na Korea Kusini kwa ushirikiano wa Marekani, sanjari na kupinga vikwazo vilivyowekewa dhidi yake katika hatua yake ya kuimarisha zana za kinyuklia.
Katika ilani yake ya hivi karibuni, Rais huyo wa Korea Kaskazini amesema kuwa mpango wake umelenga makombora ya masafa marefu na yale ya kawaida kwa lengo la kuvamia vituo vya Marekani vilivyo Bahari ya Pacific wakati wowote.

Kim Jong-un ameweka tayari makombora hayo kukabiliana na tishio la mashambulio kutoka kambi za kijeshi za Marekani na ndege zake za kivita.
Rais Kim anasema hatua zake zitakwenda sambamba na kujibu ndege za kivita za Marekani kuruka katika anga ya Rasiya Korea.

Kim amesema kuwa kwa sasa muda umewadia wa kumaliza mgogoro na Marekani. Kwa upande wake Marekani na Korea Kusini zinasema kuwa hadi sasa imefanikiwa kunasa mipango ya ndani kutoka Korea Kaskazini kwamba ina kombora lenye na uwezo wa kushambulia umbali wa kilomita 3,000 likiwa na ujazo wa mafuta, tayari kwa kulipuliwa.

Mgogoro huo ulitokana na Peninsula ya Korea kugombewa na mataifa hayo, hatua iliyowahi kusababisha vita baina ya nchi Korea Kaskazini na Korea Kusini iliyopiganwa kati ya mwaka 1950 hadi 1953 ikijumuisha pia China,Umoja wa Kisovyeti na Umoja wa Mataifa (UN).
Machi 29 mwaka huu, mataifa makubwa duniani, China na Urusi yameelezea hofu ya kukithiri kwa mzozo katika Rasi ya Korea na kutaka pande zote kujiondoa katika majibizano.

Makubaliano ya mkutano huo ilikuwa ni kumaliza mgogoro uliopo kati ya nchi hizo.
Taarifa za kiuchunguzi uliofanywa na Korea Kusini zinaeleza kuwa Korea Kaskazini inajiandaa kukamilisha mipango yake ya kuzindua kombora, baada ya kuhamisha makombora yake mawili upande wa Pwani mwa nchi hiyo.

Katika mipango ya kujibu tishio hilo, Korea Kusini kwa ushirikiano na Marekani, zimeimarisha mitambo yake ya kuchunguza shambulio lolote kutoka kwa Rais Jong. Kufuatia hali hiyo, Korea Kusini nayo imeeleza kuimarisha hali yake ya tahadhari baada ya habari kuwa Korea Kaskazini inajiandaa kufanya jaribio la kombora lake moja la masafa ya kati, lililotarajiwa kufanyika April 15, mwaka huu kama sehemu ya kumbukumbu za kuzaliwa muasisi wa Taifa hilo Kim Ill-Sung.

Rais mpya wa Korea Kusini, Park Geun-Hye, amehimiza Korea Kaskazini kubadilisha mkondo wake wa siasa, ili kutuliza uhasama unaoendelea kukuwa kati ya mataifa hayo mawili.
Hali iliyopo kwa sasa kati ya nchi hizo mbili inadaiwa kutokuwa salama kwani Korea ya Kusini imedai kuwa Korea Kaskazini inawazuia hata raia wake kufika katika upande wa pili wa mpaka.

Wakati Marekani akiunga mkono harakati za Korea Kusini, Januari 25, mwaka huu, China pia imesema itaendelea kutoa ushirikiano wa misaada ya chakula kwa swahiba wake Korea Kaskazini, huku ikithibitisha kushiriki endapo kutatokea vita yoyote kati ya nchi hizo.

Mbali na kauli hizo, Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki moon amemtaka Rais wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un kupunguza makali yake kwa mzozo unaoendelea kushika kasi, akidai kuwa umeanza kuvuka mpaka. Ban Ki moon ameeleza kuhuzunishwa na namna ugomvi huo unavyotishia maisha ya wananchi wa kawaida na kutoa wito kwa viongozi wa Korea Kaskazini, kubadili mwenendo wao. Awali, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Urusi alisema kuwa uamuzi wa Korea Kaskazini kuendeleza mpango wake wa kuimarisha uwezo wa zana za kinyukilia, unavuruga mipango ya kuanzisha upya mashauriano yanayohusu mataifa sita ya kupatanisha Korea Kusini na Kaskazini.

0 comments:

-