Friday, August 4

Jana niliweka makala iliyokuwa inaelezea safari ya bilionea Jeff Bezos, mmiliki wa Amazon kufikia kuwa tajiri namba moja duniani na kumpiku aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo kwa muda mrefu, Bill Gates 
 Hilo lilitokea tarehe 27/07/2017 ambapo hisa za kampuni ya Amazon, inayomilikiwa na Bezos kupanda thamani ghafla kwa asilimia 40. Hii ilipelekea utajiri wake kuongezeka na kumzidi Bill Gates. Lakini kabla siku haijaisha, thamani ya hisa zake ilishuka na hilo kupelekea utajiri wake kupungua, na kumfanya arudi kuwa namba mbili na siyo namba moja pia.

Wapo watu wengi wanashangaa hili limetokeaje na mbona limetokea haraka sana. Wengine wanafikiri ni kama kuna mashindano ya moja kwa moja na mbabe ndiyo anashinda zaidi. Wengine wanaona labda kuna mchezo umefanyika kumshusha aliyepanda. Hapa nimekuandalia mambo matano unayopaswa kuyajua, ambayo yatakupa uelewa wa hili lililotokea na kujua kwa nini limetokea. Karibu sana tujifunze kwa pamoja.

1. Utajiri namba moja wa dunia haushindaniwi.

Japokuwa mtu anaweza kuweka juhudi kuhakikisha anakuwa tajiri mkubwa, hakuna juhudi za moja kwa moja ambazo mtu anaweza kuweka akajihakikishia kwamba atakuwa tajiri namba moja wa dunia. Baada ya kufikia kiasi fulani cha utajiri, kunakuwa na vigezo vingi ambavyo vinahusika mtu kufikia kuwa tajiri namba moja duniani.

Kigezo kikubwa ni hisa za makampuni ambayo matajiri hao wa dunia wanamiliki. Kupanda na kushuka kwa bei ya hisa ni jambo la kawaida kabisa kwenye soko la hisa. Hivyo kuna wakati zinaweza kupanda na mtu utajiri wake ukaongezeka, au zikashuka na mtu utajiri wake ukapungua. Lakini kwa sehemu kubwa hayo yapo nje ya uwezo wa mtu binafsi.

2. Lijue soko la hisa.

Soko la hisa ni mfumo wa kutoa umiliki wa makampuni kwa watu wengi zaidi. Mtu anapokuwa na kampuni na kuiandikisha kwenye soko la hisa, maana yake anaruhusu mtu yeyote anayetaka na anayeweza, awe sehemu ya wamiliki wa kampuni hiyo. Umiliki huo anaupata anaponunua hisa za kampuni husika.

Kampuni inapofanya vizuri, wanahisa wananufaika, hisa zinapanda thamani na bei yake kuwa juu. Kampuni inapofanya vibaya, wanahisa wanapoteza, hisa zinashuka thamani na bei yake kuwa chini.

Kupitia soko la hisa, mtu anaweza kununua na kuuza hisa wakati wowote kulingana na upatikanaji wa hisa hizo.

Kilichotokea kwa Bezos ni hisa kupanda kwa kasi, thamani yake kuwa juu na utajiri wake kuongezeka. Baada ya muda, hisa zilianza kushuka na utajiri wake kupungua.

3. Soko la hisa linaongozwa na hisia.

Kitu kikubwa kinachoendesha soko la hisa, ni hisia, na hili ndiyo limekua tatizo kubwa sana kwenye uchumi na uwekezaji. Watu wamekuwa wakiendeshwa na hisia katika kununua na kuuza hisa zao. Na hilo limekuwa linawaumiza wengi na kuwanufaisha wachache.

Kwa mfano, hisa za kampuni fulani zinapoanza kupanda bei, watu zitatengeneza faida, hivyo wengi wanakimbilia kuzinunua. Sasa wengi wanavyokimbilia kuzinunua, bei inazidi kupanda zaidi, hilo linachochea watu kuzitaka zaidi. Ikitokea hisa za kampuni zinachuka bei, kila mtu anahofia kupata hasara, hivyo anakimbilia kuuza, kadiri wengi wanavyotaka kuuza, ndivyo bei inavyozidi kushuka, hilo linawasukuma wengi kukimbilia kuuza ili wasipate hasara. Hivyo ndivyo hisia zinavyowaendesha wengi.

Wawekezaji wenye mafanikio makubwa kama Warren Buffett wamekuwa na msimamo mmoja unaowaepusha kuendeshwa na hisia. Msimamo huo ni KUNUNUA HISA PALE AMBAPO KILA MTU ANAUZA (kwa sababu bei inakuwa chini) NA KUUZA PALE KILA MTU ANAPOKUWA ANANUNUA (hapo bei inakuwa juu). Hivyo wananunua hisa kwa bei ndogo na kuuza kwa bei kubwa, wanatengeneza faida kubwa bila ya kufanya kazi kubwa.

4. Siyo mara ya kwanza hili kutokea.

Watu wengi wanachojua ni kwamba, Bill Gates ndiye tajiri namba moja duniani wakati wote. Huo siyo ukweli, ni kweli amekuwa tajiri namba moja mara nyingi kuliko mtu mwingine yeyote, lakini kuna vipindi ambavyo hakuwa namba moja.

Septemba 2016 hali kama hii ilitokea ambapo bilionea Amancio Ortega wa Hispania alimpiku Bill Gates na kuwa tajiri namba moja duniani kwa siku mbili, baada ya hapo alishuka na kuwa namba tatu.

Mwaka 2010, bilionea Carlos Slim Helu wa Mexico aliwapita Bill Gates na Warren Buffett na kuwa tajiri namba moja duniani. Alidumu kwa miaka minne kama tajiri namba moja duniani.

Warren Buffett amewahi kumpiku Bill Gates na kuwa namba moja kuanzia mwaka 2008 mpaka 2009.

5. Zama za Bill Gates kuwa tajiri namba moja duniani zinafika ukingoni.

Bill Gates amekuwa tajiri namba moja duniani kwa miaka 18 katika miaka 23 iliyopita. Pia ameweza kuwa tajiri namba moja kwa miaka 13 mfululizo. Hii ni rekodi ya kipekee. Lakini kadiri mambo yanavyokwenda sasa, zama zake hizi zinafika ukingoni. Na siyo kwa sababu zozote mbaya, ila ni kwa sababu wapo mabilionea wanaokuja kwa kasi sana, Mark Zuckerberg, mmiliki wa facebook anapanda kwa kasi kubwa. Jeff Bezos mmiliki wa Amazon naye ana kasi kubwa ya ukuaji wa utajiri.

Kitu kingine muhimu zaidi ni kwamba Bill Gates kwa sasa anatoa sehemu kubwa ya utajiri wake kama misaada kupitia taasisi yake ya Bill and Melinda Gates Foundation.

Hivyo tutegemee kuona sura nyingine kwenye nafasi hii ya kwanza kwa miaka inayokuja.

Haya ni machache muhimu ambayo nimeona niwashirikishe, kwa sababu yanatupa uelewa zaidi.

Kumbuka rafiki, tunafuatilia haya siyo tu kujifurahisha, bali kupata hamasa ya kuweka juhudi zaidi ili kupata matokeo makubwa zaidi. Siyo lazima uwe bilionea na wala siyo lazima uwe namba moja duniani, lakini kuwa na uhuru wa kifedha, ni lazima, kwa sababu fedha ndiyo zinatuwezesha kupata mahitaji yetu ya msingi.

Nakutakia kila la kheri rafiki, mapambano yaendelee.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani,


0 comments:

-