Katika hadithi za kijasusi za Urusi na Marekani, si kawaida kuacha kutaja majina ya 'mashujaa wa ujasusi wa urusi' waliojitoa kufa kupona kutumikia Taifa lao. Ama kwa kujitoa wenyewe au kwa kuwatumia wamarekani wenyewe. Isingelikuwa kazi ya majasusi hawa wa kidola, pengine leo Urusi isingelikuwa Taifa tishio kijeshi. Wanadamu hawa ndio walifanikisha kuiba taarifa muhimu kutoka Marekani na Uingereza, zilizosaidia Urusi kuwa na teknolojia ya nyukilia, na kutengeneza silaha za kiatomiki.
Kwa kumbukumbu;
Kulikuwa na Klaus Fuchs, aliyefanya kazi katika miradi wa ujenzi wa mabomu ya atomiki, huku akiiba taarifa na kuzipeleka kwa majasusi wa Urusi walioku wa Uingereza. Alihukumiwa jela miaka 14 (hakuuawa kwa sababu alivujisha taarifa kutoka Uingereza kwenda Urusi wakati wa vita kuu ya pili ya dunia, ambapo Urusi na Uingereza walikuwa upande mmoja. Hiyo ndio sababu ya kutokuuawa kwakweli na badala yake akaambulia jela miaka 14.
Harry Gold, ndiye aliyechukua Taarifa za siri kutoka kwa Klaus Fuchs, na kuzipeleka Urusi. Harry Gold aliigiza kama mtembeza watalii wa kirusi, huku watalii hao wakiwa majasusi na yeye kuwa kiungo cha taarifa kutoka kwa Fusch. Harry Gold hakuwa Mrusi, bali mmarekani, mzaliwa wa Pennsylvania. Harry Gold alishtukiwa na kukamatwa mwaka 1951, na baada ya kuhojiwa sana, akawataja wenzake akina David Greenglass na wengine wa kundi la Rosenberg spies. Harry Gold alihukumiwa miaka 30 jela.
Anatoli Yatskov! Mwanadiplomasia wa kirusi alifanya kazi jijini New York huku akifanya Ushushu na kina Harry Gold na Julius Rosenberg. Hakuwahi kukamatwa lakini alikufa kwa maradhi. Kabla ya kufa, alikiri kuwa karibu nusu ya watu wa kundi lake, walishtukiwa.
David Greenglass, mwanasayansi wa maabara katika miradi wa Manhattan uliohusu ujenzi wa mabomu ya nyuklia nchini marekani, pia mwanajeshi wa jeshi la Marekani, lakini jasusi wa Urusi. Greenglass aliunganishwa katika ujasusi na mkewe Ruth Greenglass ambaye alikuwa na itikadi ya kikomunisti. Alipeleka taarifa kwa Harry Gold, na kwa shemeji yake (kaka yake Ruth), Julius Rosenberg. Ikumbukwe kuwa Klaus Fuchs (aliyetajwa awali) amewahi kuwa akifanya kazi na huyu Greenglass na wote walipeleka taarifa kwa Harry Gold, lakini hawakuwahi kujua kuwa wote ni majasusi wa Urusi hadi pale walipokamatwa. Harry Gold alichukua taarifa kutoka kwao bila wao kukutana.
David Greenglass, alipokamatwa alikiri na kuwataja wenzake baada ya kuahidiwa kutohukumiwa kufa. Aliwataja Julius Rosenberg na mkewe Ether Rosenberg pamoja na Morton Sobell.
Julius na Ether Rosenberg waliuawa kwa kukalishwa kwenye kiti cha umeme mnamo June 1953, huku Morton alihukumiwa miaka 30 katikajela ya Alcatraz. Na kama alivyoahidiwa, David Greenglass hakunyongwa Bali alifungwa miaka 15. Mkewe Ruth Greenglass alisamehewa na kubaki kulea watoto wao wawili. Baada ya miaka 15, Greenglass alitoka na kuungana na mkewe.
(Note. David alimuoa Ruth, Julius alimuoa Ether. David ni kaka wa Ether na Julius ni kaka wa Ruth. Kwa hiyo David aliwataja dada yake na shemeji yake (Ether na Julius) wakanyongwa badala yake.)
Lona Cohen! akiwa kiongozi wa chama cha kikomunisti cha Marekani, aliunganishwa na mawakala wa KGB wa Urusi mwaka 1939. Lona aliwatumia akina Theodore Hall na Saville Sax. Hawa ni vijana wawili kutoka chuo kikuu cha Havard waliofuzu shahada ya fizikia. Wakiwa wanasayansi katika miradi ya kutengeneza mabomu ya nyuklia, walivujisha taarifa kwa Lona Cohen ambaye naye alizipeleka kwa Leonid Kvasnikov, Afisa wa KGB mjini New York. Mnamo miaka ya 1950, Lona Cohen alikimbilia Urusi, kisha akasafiri hadi Uingereza na kuendelea kuiba nyaraka muhimu na kuzipeleka Urusi kuanzia mwaka 1954 hadi 1961 alipokamatwa akiwa na Mumewe. Hata hivyo alirudishwa Urusi kwa kubadilishana na majasusi wa kiingereza waliokamatwa Urusi. Wakiwa mjini Moscow, Urusi, Lona na mumewe waliendelea na kazi ya kufundisha katika taasisi za kiintelijensia za nchini humo.
Vijana Theodore Hall na Saville Sax waliokuwa wakivujisha taarifa kwa Lona, alipokuwa New York, hawakuwahi kukamatwa hadi walipotoboa siri wenyewe wakiwa wazee.
Leonid Kvasnikov. Shujaa wa KGB, mtaalamu wa ujenzi wa mashine za kemikali, mwanasayansi na mkufunzi wa intelijensia ya kiufundi (technical intelligence).
Huyu ndiye aliyekuwa kiungo muhimu cha taarifa kutoka Marekani na Uingereza, kwenda Urusi. Ndiye moja ya waratibu wa shughuli za kijasusi za wizi wa teknolojia ya nyuklia. Alifanya kazi hizo akiwa Moscow, na baadae mwaka 1943 hadi 1945 alikwenda mwenyewe Marekani. Baadae alitunukiwa tuzo ya Lenin (order of Lenin) na tuzo ya Red star, tuzo za ngazi ya juu kabisa katika intelijensia ya Urusi.
Hao, na wengine, katika ushushushu wao, katika kazi hiyo ya hatari, pamoja na kuchomana, kusalitiana na kubadilishana siku za kufa, walifanikisha kuhamisha teknolojia ya nyuklia kutoka Marekani na Uingereza na kuifikisha Urusi.
Huo ndio ujasusi wa kidola! Hakuna katika dunia, njia nyingine ya kuchota maarifa yanayolindwa na wenye nayo, zaidi ya njia za kijasusi. Njia za hatari, zinazolazimu matumizi ya ubongo.
"Intelijensia bila tamaa ya mafanikio chanya ni kama mbayuwayu asiye na mbawa"
0 comments:
Post a Comment