Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 26 April 2017,
ameongoza maelfu ya Watanzania katika sherehe za miaka 53 ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Mjini
Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kukagua gwaride la vikosi vya ulinzi na
Usalama lililoandaliwa kwa heshma yake, Rais Magufuli amewahakikishia
watanzania kuwa yeye na Rais wa Zanzibara Dkt. Ali Mohamed Shein
wataendelea kuulinda Muungano kwa nguvu zao zote na kwamba atakayejaribu
kuuvunja atavunjika yeye.
''Muungano ndio silaha yetu. Ni nguvu yetu. Mimi na
mwenzangu Dkt. Shein tutaulinda Muungano kwa nguvu zote. Yeyote
atakayejaribu kuuvunja atavunjika yeye'' amesema Rais Magufuli.
Aidha Dkt. Magufuli amewataka watanzania kuendelea kudumisha amani
iliyopo nchini kwani amani ndio chachu ya maendeleo yanayopatikana
nchini.
Rais Magufuli amesema Tanzania imeweza kufikisha miaka 53 ya Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar kwa sababu ya amani iliyopo nchini
iliyowezesha kupatikana mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuunganisha
mataifa yetu mawili na kuuunda taifa moja lenye nguvu.
Aidha amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umewezesha
kupatikana mafanikio makubwa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na
kijamii.
Mhe. Rais ametaja mafanikio mengine yaliyopatikana kutokana na
Muungano ni kukua kwa uchumi na kukabiliana na matatizo ya umasikini na
ukosefu wa ajira,kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, majini,reli
na nchi kavu.
Aidha Muungano umeimarisha na kuboresha upatikanaji wa huduma za
jamii ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya shule na hospitali
pamoja na kukua kwa demokrasia nchini.
Kwa mara ya kwanaza katika historia ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar Maadhimisho ya Sherehe za Muungano zinafanyika mkoani Dodoma
makao makuu ya Serikali ikiwa ni ishara tosha kuwa Serikali ya awamu ya
tano inayoongozwa na chama cha Mapinduzi imedhamiria kwa dhati
kuhakikisha makao makuuu ya Serikali yanakuwa Dodoma.
''Niwahahakikishie wana Dodoma na Watanzania kwa ujumla
kwamba Serikali sasa tumefika Dodoma na hatutarudi tena, na kama
tulivyoahidi mwaka 2020 Serikali yote itakuwa imehamia hapa'' amesema Rais magufuli.
Sherehe za miaka 53 ya Muungano zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali
ikiwa ni pamoja na wajane wa viongozi waasisi wa Muungano mke wa hayati
Mwalimu Julius Nyere Mama Maria Nyerere na hayati Abeid Aman Karume,
Mama Shadya Karume,Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa, na viongozi wa chama na serikali.
Kauli mbiu ya Sherehe za Muungano mwaka huu ni ''Miaka 53 ya muungano,Tuuulinde na kuuimarisha, Tupige vita Dawa za Kulevya na Kufanya Kazi kwa Bidii''
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
26 Aprili, 2017
0 comments:
Post a Comment