Wednesday, April 13



MIAKA tisa iliyopita, mfanyabiashara maarufu wa Sudan, Mohamed Ibrahim, alianzisha Tuzo ya kila mwaka kwa viongozi wastaafu wa barani Afrika waliojitokeza katika kusimamia (wakati wakiwa madarakani) uongozi uliotukuka na wa uadilifu, kudumisha utawala bora, kuwaendeleza wananchi wake, kutokumbatia ufisadi na hivyo kuushughulikia kikamilifu na kung’atuka kwa hiari na bila mizengwe kipindi chake cha utawala kinapomalizika.

Tuzo hiyo, yenye kiambatanisho cha fedha taslimu dola za Marekani milioni 5 ni tuzo kubwa kuliko zote zinazopewa mtu mmoja binafsi hapa duniani – kuliko hata ile Tuzo ya Nobel. Lengo ni kusisitiza utawala bora katika Bara la Afrika, bara ambalo, kwa maneno yake mwenyewe Ibrahim, “limejaliwa kuwa na madini mengi ya kila aina kuliko mabara mengine yote, lakini zaidi ya wakazi wake 300 milioni wanaishi maisha duni sana — chini ya dola moja ya Marekani kwa siku.

Kwa tafsiri yoyote ile, Tuzo ya Mo Ibrahim ni ya heshima kubwa kwa kiongozi mstaafu katika Bara hili lakini kwa bahati mbaya wanaoonekana kutimiza vigezo na sifa za kupata tuzo hiyo wamekuwa adimu sana.
Kutokana na uchache huu tangu ianzishwe tuzo hiyo mwaka 2007, ni viongozi wa zamani wanne tu ndiyo wamepata. Hii ni kwa sababu wengi viongozi siku hizi wanaweka mbele masilahi yao na yale ya wanafamilia wao na maswahiba wao kuliko ya wananchi waliowachagua.

Na zaidi ya hayo, viongozi wengi barani humu ni ving’ang’anizi madarakani, pamoja na kwamba nchi zao hakuna maendeleo ya maana. Wako tayari kubadilisha katiba kuondoa ukomo wa vipindi vya urais, hata kama kufanya hivyo kunaweza kuleta farakano kubwa nchini na hata nchi kujikuta inatumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Kuna gumzo kubwa liliibuka hapa nchini mwishoni mwa 2007 pale Kamati ya Tuzo ya Mo Ibrahim ilipomtangaza mshindi wa kwanza wa tuzo hiyo – aliyekuwa Rais wa zamani wa Msumbiji Joachim Chissano. Kuna baadhi waliona Benjamin Mkapa, Rais wa awamu ya Tatu wa Tanzania ndiyo alifaa kuikwaa tuzo hiyo. Wakati huo Mkapa alikuwa katika mwaka wa pili wa kustaafu kwake, kama ilivyokuwa kwa  Chissano.
Walishangaa kuona Chissano ndiye aliyepata. Hebu angalia: Chissano na Msumbiji yake na Mkapa na Tanzania yake ni vitu vilivyotoka kwenye dunia mbili tofauti katika vigezo vingi vilivyozingatiwa na Kamati ya Tuzo. Wakati Msumbiji ilipata uhuru wake kupitia mtutu wa bunduki, Tanzania ilipata kwa kupewa kwenye sahani – tena miaka 14 kabla.
Na baada ya hapo, wakati Msumbiji ilikumbwa katika miaka mingi ya vita ya wenyewe kwa wenyewe, viongozi wetu hapa Tanzania walikuwa wakiimba majukwaani kwamba Tanzania ilikuwa nchi ya amani na hata kusema kwamba ilikuwa ya kipekee (unique) bila hata ya kutaja kivipi – ila wakisisitiza tu kwamba hali hii imetokana na uongozi bora wa Chama cha Mapinduzi (CCM) – kama vile suala la ‘amani’ ni suala ambalo linaweza kufanywa sera ya chama cha siasa.

Sijamaliza – Mkapa aliongoza kwa miaka 10 ya amani na utulivu nchini na aliingia Ikulu akikumbatia kifuani mwake ‘shahada’ ya
‘Bwana Msafi.’ Hivyo kutokana na uwingi wa rasilimali za nchi ikilinganiswa na Msumbiji, Mkapa angeweza kuwa ‘mgombea’ bora wa Tuzo hiyo mwaka 2007 kama angelikuwa na visheni iliyotakata.
Na kama Mkapa angeikwaa Tuzo hiyo hali ya majisifu ingeikumba serikali ya CCM na majukwaa yangejaa kauli za kujipongeza kwa kuonyesha kwamba tuhuma zote za ufisadi dhidi ya serikali zilikuwa majungu tu yaliyokuwa yanapikwa na wapinzani.

Lakini sasa hivi sote twafahamu tuhuma nyingi za ufisadi ziliukumba utawala wa Mkapa hasa kipindi cha mwisho mwisho cha utawala wake na ambazo zilikuwa vigumu kuzificha kwa kamati ya Tuzo ya Mo Ibrahim.
Kwa namna moja suala hili latuambia kitu kimoja: kwamba hali ya amani na utulivu nchini si kigezo muhimu katika kuchochea maendeleo katika nchi, kwani ingekuwa hivyo, basi Tanzania ingelikuwa ni nchi iliyoendelea sana katika sehemu hii ya Bara la Afrika, kama siyo katika Bara lote. Sasa hivi kuna uwezekano mkubwa kwa Tanzania kutoa Rais anayeweza kuinyakuwa Tuzo ya Mo Ibrahim baada ya kustaafu. Hata hivyo kuna ‘lakini’ nyingi sana.
Takriban miezi miwili hivi iliyopita wakati upepo wa utumbuaji majipu wa Rais John Magufuli ulipokuwa unashika kasi kulikuwapo pendekezo katika mitandao ya jamii hapa nchini kwamba iwapo akiendeleza kasi hiyo anaweza akawa katika nafasi nzuri ya kushinda Tuzo ya Mo Ibrahim ya uongozi uliotukuta katika bara la Afrika.

Ilikuwa vigumu kutambua iwapo pendekezo hilo lilitolewa kwa dhati au kwa njia ya kejeli tu. Lakini maoni yangu ni kwamba kabisa inawezekana, kama asipoingiliwa na watu wengine hasa kutoka katika chama chake – CCM.

Akitambua hivyo, basi itabidi ajifunze somo kutoka kwa watangulizi wake, hususan Mkapa na awaaminishe wananchi kwamba anayo azima kubwa ya kuziinua hali zao za maisha kwa kutumia rasilimali nyingi zilizopo nchini ambazo hapo nyuma zilikuwa zinaporwa tu na wajanja wachache wakiwemo wataumishi wa serikali.
Ni lazima wananchi wamuone anawawajibisha wote wale waliotuhumiwa katika uporaji huo, bila upendeleo wowote. Imani hiyo ya wananchi kwake inaweza ikatoweka mara moja pindi tu akionekana anawawajibisha watuhumiwa kwa njia ya upendeleo – yaani kuyaruka baadhi ya ‘majipu’ yanayopaswa kutumbuliwa bila ya sababu ya msingi.

Ninavyoandika hivi tayari yapo malalamiko kutoka kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kwamba kuna baadhi ya viongozi wake aliyowateua muda si mrefu, wakiwemo mawaziri, wanabeba tuhuma za ufisadi mkubwa kiasi kwamba hawakupaswa kuwa nao katika kampeni yake ya utumbuaji majipu.
Masuala haya yameanza kidogokidogo, lakini akiyapuuza kuchukua hatua stahiki, hataweza tena kuchukuwa hatua kwa masuala mengine ya ufisadi yatakoibuka hata yakiwa makubwa namna gani.
Na ikifika hapo, basi wananchi hawatakuwa na budi ila kusema “mnaona, mambo ni yale yale – CCM ni ile ile” – na Tuzo ya Mo Ibrahim ataisikia tu inampitia pembeni.

0 comments:

-