Saturday, February 20



Donald Ngoma wa Yanga (kulia) akikimbia na mpira kumuacha beki wa Simba Hassan Isihaka
Na Baraka Mbolembole
Thaban Kamusoko ndiye mchezaji bora zaidi kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi kati ya ‘Watani wa Jadi’ na ‘ Wapinzani Wakuu’ wa kandanda la Tanzania. Yanga SC iliyo nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu bara ndiyo watakaokuwa wenyeji wa mchezo huo.
Simba SC ndiyo wanashikilia usukani wa ligi hadi sasa na wamefanikiwa kufika juu kwa mara ya kwanza baada ya kusubiri kwa miaka mitatu bila mafanikio. Mashabiki wengi wa Yanga wamekuwa wakiingia uwanjani kwa ajili ya kufuatilia uchezaji wa mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Zimbabwe.
Na kocha wake Hans Van der Pluijm amekuwa akimtumia kama-mchezesha timu mkuu na mtengenezaji wa nafasi za magoli, zaidi magoli yake matano aliyofunga hadi sasa katika ligi na tuzo binafsi ya mchezaji bora wa mwezi Disemba, 2015 ni wazi kuw Man-Kamusoko ni mchezaji ambaye atafuatiliwa zaidi na mashabiki ambao wanausubiri mchezo huo kwa hamu.
UWEZO WA SIMBA
Ushindi wa gemu 6 mfululizo chini ya kaimu mkufunzi mkuu Mganda, Jackson Mayanja umefufua na kuweka hai matumaini ya kampeni yao ya kurudisha ubingwa wa VPL ambao waliushinda kwa mara ya mwisho msimu wa 2011/12 ambao pia uliambatana  na ushindi wa 5-0 dhidi ya mahasimu wao Yanga.
Kazi kubwa inatakiwa kufanya timu ya Mayanja ili kuendelea kushikilia nafasi ya kwanza katika msimamo. Mbinu za Mayanja kwa kiasi kikubwa zimekuwa kivutio kutokana na kutoa fursa ya timu yake kucheza vizuri na kufunga magoli.
Hassan Kessy na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wanataraji kucheza katika fullbacks na wachezaji hao wawili wa nyuma wamekuwa na tabia ya kupanda kusaidia mashambulizi, pia wamekuwa wazuri katika upigaji wa pasi za mwisho.
Kessy amekuwa na krosi zenye macho, Tshabalala amekuwa na kasi kila anaposhambulia na mara nyingi pasi zake za mwisho hutoa akiwa katika maeneo ya hatari ya timu pinzani. Yanga hawarembi sana mchezo, na ni timu yenye wachapa kazi.
Wachezaji wa Yanga wana tabia ya kutumia mabavu uwanjani. Wanatakiwa kuwa makini kwa kuwa wanaweza kupata madhara kutokana na jambo hilo. Kocha, Hans hatokuwa na Kelvin Yondan pia si rahisi kumtumia nahodha wake Nadir Haroub. Kwa maana hiyo ngome ya Yanga haitakuwa na walinzi hao wazoefu wa kati kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2012/13.
Mbuyu Twite na Vicent Bossou watapangwa kama walinzi wa kati. Itakuwa nafasi yao ya kuwaonyesha Watanzania namna walinzi wa kati wanavyotakiwa kucheza.
Mbuyu ( raia wa Rwanda) na Bossou ( raia wa Togo) wana miili mikubwa, nguvu na uwezo wa kuondosha mipira, lakini bado wanatakiwa kuongeza wepesi ili kuendana na kasi ya washambuliaji wa Simba, Hamis Kizza, Ibrahim Ajib na Haji Ugando ambao wanaweza kuanza katika safu ya mashambulizi ya Simba.
Ukuta thabiti ndiyo mbinu sahihi ya kujilinda. Juma Abdul litakuwa chaguo sahihi tarajiwa katika beki namba 2, na nadhani hii ni mechi ya Oscar Joshua kama beki 3 na si Mwinyi Hajji ambaye alikuwa na majeraha yaliyomuweka nje katika mechi tano zilizopita.
Wakati, Kessy akishambulia vizuri kwa upande wa Simba, Juma ni mpiga krosi pasi hatari upande wa Yanga. Timu zote hutegemea fullbacks kama njia mbadala ya kupata magoli. Kama timu zote zitaingia kucheza mfumo wa 4-3-3 itakuwa mechi ya wazi na yeyote atakayebadilisha mfumo huu atakuwa katika nafasi kubwa ya kupoteza mechi.
SAFU ZA KIUNGO
Kamusoko, Haruna Niyonzima na Said Juma ‘Makapu’ inaweza kuwa safu imara ya kiungo. Makapu ni mkabaji, anacheza faulo za kitaalamu, ana uwezo wa kucheza ‘tackling’, pia ana maarifa ya kupanga mashambulizi. Amekwishacheza mechi tatu za mahasimu hao na hajawahi kuiangusha timu yake.
Uwezo wake wa kupora mipira kuvuruga njia za hatari za wapinzani wake ni sababu kubwa ya kutaka kumuona kijana huyo akicheza kama namba 6 upande wa Yanga. Wakati Justice Majabvi amekuwa mtulivu na mpangaji mzuri wa mashambulizi ya Simba akicheza kama namba 6.
Makapu atamfanya Mwinyi Kazimoto asiwe huru na kama Mwinyi hatokuwa huru uwanjani itamaanisha kuwa Simba watabadili mbinu za kushambulia na wataanza kupitia pembeni ya uwanja. Majabvi ni injini ya Simba, hapotezi pasi hovyo, yuko makini na uwezo wake wa kuusoma mchezo huko juu.
Kuendelea kutembea sana na mpira kunaweza kumuangusha mbele ya Mzimbabwe mwenzake, Kamusoko. Kamusoko yuko fasta na pasi zake timilifu, anakimbia uwanjani muda wote hilo litampa wakati mgumu Majabvi na mechi inaweza kuwa ngumu kwake.
Mkude atakuwa msaidizi wa Kazimoto katika upangaji wa mashambulizi. Naye anapenda kukaa na mpira kwa muda mwingi lakini pia amekuwa na tatizo la kupoteza pasi nyingi.
Mchezo wake wa nguvu unaweza kumfanya Haruna Niyonzima asiwe huru sana lakini bado naitazama Yanga kama timu itakayotawala sana mchezo na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga kwa kuwa ‘wako makini na wenye maamuzi ya haraka’ kuliko Simba katikati ya uwanja.
Umakini mdogo wa Mkude, na kiwango kisichotabirika cha Kazimoto kinaweza kutoa nafasi kwa Niyonzima na Kamusoko kutawala mechi na kama hilo litatokea watapigwa haswa. Msuva atawatesa walinzi wa Simba kutokana na kasi yake, lakini atakuwa msaada mkubwa pia katika kiungo. Simba wajipange hasa, na hawapaswi kupoteza mipira mingi katikati ya uwanja.
USHAMBULIAJI
Katika mechi zilizopita kila timu imeonyesha makali katika ufungaji. Mayanja anaweza kuwapanga Ajibu, Kizza na Daniel Lyanga kama timu yake itacheza 4-3-3. Anaweza kuwapanga Ajib na Kizza kama washambuliaji wa mbele ili kumpa nafasi Said Ndemla au kijana Haji Ugando.
Mfumo ambao unaweza kuleta uwiano sawa wa kimchezo ni 4-3-3 ambao Yanga pia watautumia. Kuwapanga washambuliaji watatu wenye uwezo wa kufunga na kasi nzuri kutawafanya walinzi wa Yanga kuwa katika presha kila mpira utakapokuwa unaelekea katika maeneo yao ya kujihami.
Yanga hutumia nguvu kulinda goli lao hivyo kuwaacha Ajib na Kizza pekee itawafanya wawe huru lakini itawachanganya endapo watapangwa washambuliaji watatu-Ajib, Kizza na Lyanga. Safu ya ulinzi ya Simba licha ya kuonekana inajilinda vizuri na kusaidia mashambulizi wakati mwingine bado inapaswa kupunguza makosa mengi ya kiuchezaji hasa katika ngome ya kati.
Juuko Murishid amekuwa imara na kiongozi wa safu yote ya ulinzi lakini Mganda huyo anaweza kuyumbishwa na kiwango cha umakini cha patna wake na nahodha wa Simba, Hassan Isihaka ambaye si mzuri katika kujipanga wakati wakishambuliwa. Kama Simba watapokea mashambulizi mengi watafungwa magoli ya kutosha tu.
Amis Tambwe ni mmaliziaji wa kiwango cha juu akiwa ndani ya eneo la hatari. Mshambulizi huyo wa Burundi ni mtaalamu wa kuruka juu na kufunga magoli ya kichwa. Donald Ngoma ni mpambanaji, ana kasi, nguvu na uwezo wake wa kufunga na kutengeneza nafasi uko juu.
Hii itakuwa mechi ngumu kwa Simba, watabanwa katikati ya uwanja na watazimwa katika mbinu zao za kupanga mashambulizi. Mpango pekee utakaowakomboa ni kucheza kwa umakini wakati wote na kujitahidi kudhibiti mpira kwa muda mwingi. Kama ni kete, basi kete  yangu ya ushindi naiweka upande wa Yanga.

Comments

9 comments

0 comments:

-