Saturday, February 20


Wizara imepata taarifa zisizo na ukweli zinazoenezwa na kusambazwa na watu wasiokuwa na nia njema kwa Wizara na Serikali kwa ujumla, kuwa Wizara iliyokuwa ya Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliendesha zoezi la kukusanya wasifu(CV) za Wafanyakazi wake kwa lengo la kuwafukuza kazi.
 
 Wizara imesikitishwa na inalaani vikali uvumi wa taarifa hizi na  inakanusha kuwa taarifa hizi hazina ukweli wowote.

Zoezi la kukusanya CV za watumishi ni zoezi la kawaida kwa waajiri na hufanyika Mara kwa mara kwa lengo la kuhuisha sifa na uzoefu wa watumishi wanazopata wakiwa kazini ambapo hatimaye huwekwa kwenye majalada yao binafsi, mwajiri anapaswa kuhakikisha jalada la kila mtumishi lina taarifa zinazoeenda na wakati, hivyo zoezi hili lilifanyika kwa lengo la kuhuisha taarifa za watumishi wa Wizara kama ilivyoelekezwa na mwajiri na si vinginevyo. 
 
Wizara inapenda kutoa ufafanuzi kuwa CV si miongoni mwa nyaraka zinazohitajika katika kumfukuza kazi mtumishi bali mtumishi anafukuzwa kazi kwa kukiuka sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi ambapo taratibu maalumu za kinidhamu hufuatwa. 
Katika kipindi husika Wizara haina mtumishi anayetuhumiwa kwa kosa la kinidhamu linaloweza kupelekea kufukuzwa kazi, hivyo taarifa hizi hazina ukweli wowote.

Aidha, Wizara inakemea vikali watu wenye tabia ya kutoa taarifa zisizo na ukweli na zenye kupotosha umma. 
Vilevile Wizara inapenda kuwaasa wananchi kuheshimu sheria na taratibu za Nchi sambamba na kutoeneza taarifa zinazotokana na vyanzo visivyokuwa rasmi au zisizothibishwa na mamlaka husika, kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria na taratibu za Nchi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa AfrikaMashariki, Kikanda na Kimataifa.
19 Februari, 2016

0 comments:

-