Ukiwauliza wengi nini hasa maana ya
Valentine’s Day, ni wachache wanaoweza kukueleza kwa ufasaha maana yake
na kwa sababu hiyo, wengi wanakuwa na kawaida ya kuiadhimisha siku hiyo
kwa mazoea tu, huku wakifanya mambo ambayo hayafai mbele ya jamii.
HISTORIA YA SIKU YA WAPENDANAO
Mtakatifu Valentine ndiye hasa muasisi
wa Siku ya Wapendao ambapo karne nyingi zilizopita, katika utawala wa
Warumi, alikuwa akipita kwenye magereza ya wafungwa wa kivita na kambi
za wanajeshi, akiwahubiria watu habari za kuwa na upendo kati yao.
Mtakatifu Valentine hakuishia hapo,
alifanya pia kazi ya kuwafungisha ndoa kwa siri wanajeshi wa Kirumi
ambao hawakuwa wakiruhusiwa kuoana wawapo kambini. Kazi hiyo ya
kuwafungisha ndoa na kuhubiri upendo, ilisababisha Mtakatifu Valentine
akamatwe na kutupwa gerezani kwa kuvunja sheria za utawala wa Kirumi.
Akiwa gerezani, Mtakatifu Valentine
aliendelea na kazi yake ya kuwahubiria wafungwa wenzake upendo,
kuwasaidia waliokuwa wagonjwa kwa kuwaponya, kuwafungisha ndoa wanajeshi
kwa siri na kuendeleza huduma za kiroho zikiwemo kuwaombea watu wenye
matatizo mbalimbali.
Kesi yake iliendelea kuunguruma,
akishtakiwa kwa kosa la kuwafungisha ndoa wanajeshi wa Kirumi, jambo
ambalo lilikuwa ni kinyume na sheria za kipindi hicho, mwisho
akahukumiwa adhabu ya kifo.
Akiwa anaendelea kusubiri siku yake ya
kunyongwa, mtoto wa mkuu wa gereza alilokuwa amefungwa aitwaye Asterius,
alipatwa na maradhi ya ajabu ambayo yalisababisha akaribie kukata roho.
Mtakatifu huyo aliposikia habari hizo,
aliomba kwenda kuonana naye ambapo alimponya maradhi yaliyokuwa
yanamsumbua. Habari za tukio hilo la kipekee, lililodhihirisha upendo wa
dhati, zilisambaa kwa kasi ndani na nje ya gereza.
Siku chache kabla Mtakatifu Valentine
hajanyongwa, alimuandikia barua ya kumuaga binti huyo wa mkuu wa gereza,
chini kabisa akaandika maneno ‘Your Valentine’, akaambatanisha na ua
waridi jekundu.
Hata aliponyongwa na kufa, wafuasi wake
waliokuwa wakiyakubali mafundisho yake, waliendelea kuiadhimisha siku
aliyonyongwa, Februari 14 kwa kupeana kadi na barua zenye maneno ‘Your
Valentine’ au ‘To My Valentine’ kudhihirisha upendo waliokuwa nao kwa
wahusika.
TAFSIRI SAHIHI
Kwa kuitazama historia hiyo fupi,
tunajifunza kuwa kumbe Valentine’s Day siyo siku ya kufanya ngono hovyo,
kuanzisha uhusiano wa kimapenzi, kulewa na kufanya kufuru nyingine kama
hizo bali ni siku ya kuoneshana upendo, kupeana zawadi zikiwemo kadi
nzuri, maua na chocolate.
Na unayemfanyia hivyo, siyo lazima awe
mpenzi wako, anaweza kuwa mama yako, baba yako, rafiki yako, mwanao au
mtu yeyote unayetaka kudhihirisha kwamba unampenda, ingawa pia wanandoa
(waliohalalishwa) huitumia siku hiyo kuongeza mapenzi kwenye ndoa zao
kwa kupeana zawadi na kutoana ‘out’, wakiwa katika mavazi maalum ya
rangi nyekundu.
Ni matumaini yangu kwamba msomaji wangu
utakuwa umepata mwanga kuhusu maana na tafsiri ya Valentine’s Day.
Nakushauri na wewe usiwe miongoni mwa watu wanaofuata mkumbo kwa
kuiadhimisha siku hii tofauti kabisa na maana yake halisi. Epuka kufanya
ngono hovyo au kukesha gesti kwa kisingizio cha kuadhimisha Valentine’s
Day kwani hiyo siyo tafsiri yake.
Tukutane tena wiki ijayo, Happy Valentine’s Day.
0 comments:
Post a Comment