Mpenzi msomaji wangu, maisha yana changamoto nyingi sana ambazo kamwe huwezi kuzikwepa. Ukikubali changamoto hizo zikuzuie kufikia malengo yako uliyojiwekea, hujipendi na huna tamaa ya kufanikiwa!
Leo nataka kuzungumza na wale ndugu
zangu ambao wamejikuta wakikwama katika mambo yao, kufilisika na
hatimaye ndoto zao za mafanikio kuyeyuka.
Pia nataka kuzungumza na wale waliokuwa
na ndoto zao lakini wameshindwa kuzikamilisha kwa wakati baada ya
kupoteza vitu muhimu kama kazi au kufiwa na watu ambao waliwategemea
kuwafikisha kwenye vilele vyao vya mafanikio.
Mpenzi
msomaji wangu, hebu elekeza akili na mawazo yako yote hapa. Naamini leo
hutaondoka kama ulivyokuwa kabla ya kuchukua gazeti hili. Tiba ya
matatizo ya namna gani unaweza kuanza upya na kufikia tena kilele cha
mafanikio, inapatikana kupitia makala haya.
Katika maisha, kuna wakati unapitia
hatua mbalimbali za mafanikio. Lakini pia, unaweza ukajikuta umepoteza
vitu hivyo vyote na kurudi kama zamani au zaidi. Hayo ndiyo maisha. Hata
kama umepoteza kila kitu, kama umebaki na afya yako ikiwa imara,
shukuru sana kwani huo ndiyo mtaji na ushindi mkubwa uliobakiza.
Inawezekana kuanza upya. Kuanguka
kibiashara siyo mwisho wa maisha. Kupoteza ulichokuwa nacho siyo mwisho
wa kila kitu. Tayari imeshatokea, huwezi kubadili. Sawa, umepata hasara,
unadhani huo ndiyo mwisho wa maisha yako? Hapana!
Maisha lazima yaendelee na cha msingi
hapo ni kukubaliana na matokeo huku ukikaa chini na kutuliza akili. Kama
kuna mahali umejikwaa na kuanguka, nyanyuka haraka uendelee na safari.
Kamwe usiendelee kupaangalia mahali ulipojikwaa. Hapakuhusu, achana napo.
Songa mbele na mapambano ya maisha. Kuwa tayari kuanza upya. Ikifika mahali huoni njia, basi itengeneze mwenyewe.
Pia nikukumbushe wewe msomaji wangu
kuwa usiifikirie historia yako ya nyuma. Mafanikio yako hayako nyuma,
bali mbele unakoelekea. Achana na historia mbaya ya huko nyuma. Hicho
ulichokipoteza, unaweza kukirejesha zaidi ya hicho!
Hayo ndiyo maisha. Kama njia ya kwanza imeshindwa kukufikisha unapotaka kwenda, ni wajibu wako sasa kutengeneza njia nyingine.
Mwanasaikolojia mmoja aliwahi kusema kwamba, kwenye kutafuta mafanikio unapokosa njia, basi tengeneza njia.
Usiruhusu maisha yakuongoze, bali maisha
yaongoze wewe. Mwandishi mmoja wa vitabu aitwaye Michael Gian aliwahi
kupata ajali mbaya ya ndege. Akapoteza miguu yote na kupooza kuanzia
shingoni hadi kiunoni!
Akafilisika baada ya kuingia madeni
makubwa wakati wa kutibu majeraha na afya kwa ujumla. Lakini jamaa huyo
alianza upya kwa kuwatia watu moyo. Akawa anazungumza akiwa kwenye kiti
cha kusukuma cha matairi.
Akihamasisha watu kujikomboa na
umaskini. Leo hii ni bilionea na anamiliki viwanda na ndege kadhaa kama
usafiri wake binafsi! Hayo ndiyo maisha na mtu huyu akufanye wewe uamini
kwamba, ukianguka bado unaweza kusimama na ukafanya mambo makubwa
zaidi.
Yaani siyo kusimama tu, unaweza kujikusanyia mali zaidi ya ulizokuwa nazo huko nyuma.
Wakati mwingine Mungu humfilisi mtu kwa makusudi. Pengine ajifunze kuishi maisha ya kuanzia chini kwenda juu.
Hivyo nihitimishe kwa kusema kwamba,
huna sababu ya kujiona mnyonge na kuhisi safari yako ya kuelekea kwenye
mafanikio imeishia hapo, huo uwe mwanzo wa kupambana na niamini mimi,
hakuna linaloshindikana ukiamua kupambana.
GP
0 comments:
Post a Comment