Monday, February 29


MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameagiza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga kumaliza haraka mgogoro wa uongozi ndani ya halmashauri hiyo, kuharakisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa wananchi.
Alitoa agizo hilo katika Ikulu ndogo ya Tanga wakati akizungumza na viongozi baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya mkoa wa Tanga baada ya kuwasili kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa mazingira unaoratibiwa na Unesco.
Alisema kwa kuwa uchaguzi mkuu umekwisha salama, ajenda inayopaswa kutekelezwa sasa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kuwezesha wananchi kupata maendeleo.
“Ni wajibu wa kila mkoa wa Tanga kutekeleza ilani ya CCM bila kujali kwamba jimbo moja limekwenda, kwa kuwa hapa hapako shwari ni dhahiri kwamba tutachelewesha utekelezaji wa ilani … ,” alisema.
Alisema serikali ina mpango mkubwa wa kuwekeza katika viwanda kwenye jiji la Tanga. Hata hivyo alisema endapo hakutakuwa na uongozi wa Baraza la Madiwani katika halmashauri hiyo, malengo hayo hayataweza kutekelezwa.
“Hasara nyingine ninayoiona hapa endapo hamtamaliza hayo makando kando katika baraza la madiwani ni kuvunjwa kwa halmashauri nzima … ipo hiyo hatari na naomba muelewe kwamba kama hamtafanya jitihada ya kumaliza mgogoro huu kwa utulivu, jueni kwamba serikali haitakuwa na fedha nyingine ya kurudia uchaguzi hapa,” alisema Makamu wa Rais.
Akizungumzia uwepo wa biashara za magendo ambazo hupitishwa katika bandari bubu, alisema, “magendo hapa Tanga ni mengi sana watu wanaleta bidhaa za magendo kutoka Pemba na Unguja kuja hapa Tanga bila kulipia ushuru… ” “Mapato yanavuja, kamati ya ulinzi na usalama mjitahidi kuzuia magendo hayo ili mapato ya mkoa yasivuje… mnaachia watu wanaleta magendo halafu baadaye wakishapata hela wanakuja kutupiga kisiasa ... sasa nawataka mbane hiyo mianya yote,” alisema.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza akisoma taarifa, alisema mkoa umejipanga na kuweka mikakati ya kutekeleza mipango mbalimbali katika sekta za elimu, afya, maji, viwanda na mazingira kuwezesha wananchi kujipatia maendeleo.

0 comments:

-