Monday, February 29



WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amekagua bandari ya Mtwara na kunusa ufisadi katika utoaji wa zabuni ya ujenzi wa gati mpya tatu.
Amekinyooshea kitengo cha manunuzi bandarini hapo, akisema kimekuwa chanzo cha upotevu wa fedha za serikali kutokana na ujanja wa watu wachache.
Waziri Mkuu aliigusa pia Bodi ya Korosho akisema yako majipu yanayohitaji kutumbuliwa kutokana na kukwamisha mizigo kupitia bandari ya Mtwara, badala yake inapitishwa kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Utata wa zabuni Majaliwa ambaye juzi alitembelea eneo la ujenzi wa gati hizo, alisema mzabuni ameshashinda, lakini yapo madai kwamba watu wa manunuzi kupitia Mamlaka ya Manunuzi ya Umma Tanzania (PPRA) ndiyo wanakwamisha zabuni hiyo.
Alisisitiza, “Natambua kwamba kuna mpango wa kujenga gati nne ambapo moja kati ya hizo itajengwa na TPA (Mamlaka ya Bandari) lakini hizi tatu zilitangazwa na kupata mzabuni ambaye ni kampuni ya Hyundai kutoka Japan. Lakini hii kampuni imekuwa ikizungushwa bila sababu. Tutafuatilia kubaini tatizo liko wapi.”
“Sasa hivi tuna uwezo wa kupaki meli moja tu, lakini gati zikikamilika tutaweza kuwa na meli tatu kwa mpigo, cha msingi tusimamie maamuzi yetu kwamba lazima wafanyabiashara wa korosho watumie bandari hii kusafirisha mizigo yao na si kuipeleka kwingine,” alisema.
Kitengo cha manunuzi
Waziri Mkuu alimtaka Mkuu wa Bandari ya Mtwara, Prosper Kimaro kuwa makini na watu wa kitengo cha manunuzi katika bandari hiyo, akisema kimekuwa chanzo cha upotevu wa fedha za Serikali kutokana na ujanja wa watu wachache.
“Hapa si kuna mtu alitaka kuiba Sh milioni 300 kwa kufoji (kughushi) saini za wakubwa wake?” Alihoji Waziri Mkuu, swali ambalo lilijibiwa na Kimaro akikiri juu ya hilo na kusema, uongozi uliingilia kati kabla wizi huo haujakamilishwa.
Bodi ya Korosho
“Kwenye Bodi ya Korosho nako kuna majipu yanahitaji kutumbuliwa. RCC (Baraza la Ushauri la Mkoa) ilishakaa na kupitisha uamuzi kuwa mizigo yote ipitie bandari ya Mtwara lakini kuna watu ndani ya Bodi hiyo wanatoa vibali vya kusafirisha mizigo kupitia bandari ya Dar es Salaam,” alisema Waziri Mkuu.
Aliomba wabunge wa Mkoa wa Mtwara washirikiane kusimamia ujenzi wa gati uanze mara moja, ili ajira kwa wananchi mkoani humo zipatikane.
“Ujenzi ukikamilika siyo tu ajira zitaongezeka bali hata meli nyingi zitaleta mizigo katika bandari hii na mapato ya mkoa yataongezeka”, alisema.
Fidia kisiwa cha Mgao Kuhusu fidia kwa wakazi wa vijiji vya Kisiwa na Mgao ambao wamekubali kuhama ili kupisha upanuzi wa bandari hiyo, Waziri Mkuu aliwahakikishia wabunge hao pamoja na uongozi wa bandari kwamba Sh bilioni 13.8 zimekwishatengwa na Wizara na zitatolewa mapema mwezi ujao.
Alitumia fursa hiyo kusisitiza udhibiti wa bandari bubu ambazo zinatumiwa kuingiza sukari na mchele na kuikosesha Serikali mapato.
“Mkuu wa Mkoa, nilikwishatoa agizo kama hilo wakati nimeenda kukagua bandari ya Tanga. Kaa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa nanyi pia muweke mbinu za kudhibiti upenyo huu wa kuingiza bidhaa za magendo kwa sababu hawa ndiyo wanaokwepa kulipa kodi ya Serikali,” alisisitiza.
Awali, Mkuu wa bandari ya Mtwara, Kimaro wakati akitoa taarifa ya utendaji wa bandari mbele ya Waziri Mkuu, alisema ilianzishwa mwaka 1950 na imekuwa ikikabiliwa na ufinyu wa gati ya kuegesha meli, vifaa vya kupakulia na kupakia mizigo.
Alisema hivi sasa wamekwishapata winchi ya bandarini yenye uwezo wa kubeba tani 100 na wako kwenye mpango wa kujenga gati moja.
Majipu bandarini
Waziri Mkuu, Majaliwa ameshafanya ziara kwenye Bandari za Dar es Salaam, Tanga na sasa Mtwara ambako amebaini mambo mengi hayaendi vizuri hali ambayo amekuwa akilazimika kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwajibisha watendaji.
Chini ya mkakati wa Serikali ya awamu ya tano ya kutumbua majipu, Rais John Magufuli alivunja bodi simamizi ya bandari siku chache baada ya kupatikana kwa kontena ambazo hayakuwa yamelipiwa ushuru Bandari ya Dar es Salaam.
Kampuni 43 ziligunduliwa kuhusika katika makontena hayo. Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Joseph Msambichaka sanjari na Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Awadhi Massawe walivuliwa nyadhifa zao .
Pia Katibu mkuu wa wizara ya uchukuzi, Dk Shaban Mwinjaka aliondolewa kwenye wadhifa huo. Waziri Mkuu, Majaliwa alipofanya ziara ya kushitukiza katika bandari ya Dar es Salaam, aligundua kontena 329 zilipitishwa bila kulipiwa kodi kinyume na utaratibu wa bandarini.
Aidha, Waziri Mkuu, hivi karibuni alifanya ziara ya kushitukiza katika Bandari ya Tanga ambako pamoja na masuala mengine, alikuta tishali tatu zikiwa chakavu bila ya injini wakati serikali ilitoa fedha za ununuzi wa matishali ya kisasa.
Baada ya kubaini jipu hilo, alimwagiza Meneja wa Bandari ya Tanga, Henry Arika kutoa maelezo kwa maandishi ya nani alihusika na ununuzi wa matishali hayo badala ya zile mbili zilizopaswa kuwapo ambazo Serikali ilitoa dola za Marekani milioni 10.
Arika alijitetea kwamba tishari hizo ziliwasili nchini miaka minne iliyopita iliyopita lakini zilianza kufanya kazi rasmi mwaka jana na kwamba yeye hana muda mrefu katika bandari hiyo.

0 comments:

-