Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simon
Group, Robert Kisena ameeleza kusikitishwa na taarifa zisizo za kweli
zinazoihusisha familia ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na umiliki wa
Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) na kusisitiza kuwa yeye ndiye
mmiliki halali.
Kisena alidai kwa muda mrefu watu wenye
nia mbaya dhidi yake, wamekuwa wakihoji umiliki wa shirika hilo licha
ya kuonyesha vielelezo vyote. Alisema taarifa zilizosambaa hivi karibuni
zinazodai kuwa anaimiliki Uda kwa ushirikiano na Khalfan ambaye ni
mtoto wa Kikwete hazina ukweli.
Alidai kuwa Kampuni ya
Simon Group ambayo ilisajiliwa Mwanza 2007, inamilikiwa na watu wanane
wa familia ya Kisena isipokuwa Profesa Juma Kapuya ambaye ana asilimia
tano ya hisa kwenye kampuni hiyo.
“Kampuni hii
inamilikiwa na watu wanane, hata mkisoma hizi nyaraka mtaona majina ya
watu hao ambao ni mimi, wanangu; Simon, Gloria, Kulwa na George; mdogo
wangu William Kisena, mama yangu Modesta Pole na Profesa Kapuya.
“Hakuna jina la Khalfan Kikwete hapa, sijui hizo taarifa watu wanazitoa wapi,” alihoji Kisena huku akionyesha vielelezo.
Alisema
hata wakati kampuni hiyo inaanzishwa, Khalfan alikuwa mtoto mdogo
ambaye asingeweza kumiliki kampuni hiyo ambayo inakua kwa kasi.
Kisena
alidai taarifa hizo za uongo zinaenezwa na watu ambao ni washindani
wake kibiashara na wengine ni maadui wa kisiasa wa Kikwete.
Alisema
yeye ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na amekuwa hivyo siku zote,
lakini hajihusishi na siasa bali anafanya biashara.
“Kama kuna wanaoichafua familia ya Kikwete waache kuniunganisha na mimi, sifanyi siasa.
Na
kama kuna wanaonichafua kibiashara basi waache kuiingiza familia ya
Kikwete, wapambane na mimi kwenye biashara,” alisema Kisena.
Hata
hivyo, mwenyekiti huyo alisema kampuni yake ya Uda RT ndiyo
itakayoendesha mradi wa mabasi yaendayo kasi na kuwa nauli
zilizopendekezwa zilitokana na tathmini ya gharama halisi za uendeshaji
wa mradi huo.
Alisema baadhi ya vitu vilivyowafanya wapendekeze nauli hizo kuanzia Sh700 mpaka Sh1,200 ni pamoja na kulipia barabara za Dart.
Pia, alisema mabasi hayo yatakuwa hayakai vituoni kwa hiyo huenda wakati mwingine yatakuwa yanatembea bila abiria.
“Sababu
hizo ndiyo zimetufanya tupendekeze nauli hizo, lakini tuko kwenye
mazungumzo na Serikali ili waondoe malipo ya barabara ili nauli ipungue.
Mazungumzo yanaenda vizuri, ninaamini nauli zitapungua,” alisema.
Kisena
alisema ifikapo Machi, mwaka huu, Kampuni ya Uda itaorodheshwa kwenye
Soko la Hisa ili wananchi waweze kumiliki wenyewe kampuni hiyo.
Alisema wanaendelea kufanya mipango kwa ajili ya kuuza asilimia 70 ya hisa kwa wananchi wote.
0 comments:
Post a Comment