Friday, January 22

 


Waandishi wawili wa habari, Simon Mkina na Jabir Idrissa walitoka mahabusu juzi, Jumanne jijini Dar es Salaam, ambamo waliswekwa baada ya gazeti lao, Mawio kufutwa na Serikali.
Wamepoteza gazeti. Wakaporwa uhuru kwa kuhojiwa na polisi mchana wote na sehemu ya usiku; na hatimaye kutupwa mahabusu.
Sasa kila siku ni kiguunjia, kuripoti polisi hadi watakapopelekwa mahakamani au kuambiwa ‘yameisha.’
Haya yote yanatokana na Serikali, kupitia Waziri wa Habari, Nape Nnauye kufuta gazeti la Mawio kwa madai kuwa linaandika uchochezi; na hivyo wahariri wake kuitwa wachochezi.
Mawio limekuwa likiripoti yaliyopo kwa njia ya uchunguzi kama wizi, migogoro na taharuki; mengi yakiwa yale yaliyosababishwa na watawala au wenza wao; na lengo likiwa kufahamisha umma na kuhimiza watawala kuchukua hatua.
Zawadi pekee kwa maripota na wahariri kwa jitahada zao za kuanika mambo na kuonya kabla hali haijawa mbaya, ni kuwaita wachochezi, kuwasaka kama wahalifu, kufuta gazeti lao na kuwasweka rumande.
Kumbe Serikali ina maana tofauti ya uchochezi. Tuangalie kauli zifuatazo na kuzilinganisha na maandishi ya gazeti linalotoa hadhari na lililofutwa.
Mara ngapi tumesikia kauli hii: “Ikulu mtaisikia redioni.” Ikiwa na maana kwamba hata mkishinda katika uchaguzi, hamtaingia Ikulu. Haya ni manukato? siyo uchochezi? Wanaoambiwa wajisikie vipi? Wafanye nini?
Umewahi kusikia hili? “Mapinduzi yalikuwa Unguja, hayakuwa Pemba; na Serikali itakuwa ya Unguja!”
Hivi wanaoambiwa kwa kauli ya kibaguzi na jeuri ya kifisadi, wanyenyekee na kusema “Insha Allah?” Wanafikiri nini? Wahusika ‘hawajafutwa’
Hili je? “Serikali ya Zanzibar haikupatikana kwa vikaratasi” na pengine wakisema “hatuwezi kutoa urais kwa makaratasi” – wakiwa na maana ya karatasi za kupigia kura na kuongeza, “Kama nanyi mnataka, basi pindueni.” Kauli chokozi inayotia kidole jichoni. Anayeambiwa ajisikie vipi? Wahusika ‘hawajafutwa.’
“Wewe (Maalim Seif), utaishia umakamu wa rais. Basi!” Anayeambiwa ndiye amekuwa akipigana kisiasa tena kwa utulivu; katikati ya propaganda kuu, kwamba “nchi yetu ni ya kidemokrasia na haina ubaguzi wa aina yoyote!” Soma kishindo cha radi ya kiangazi: “Mmekuja Unguja na njaa zenu; rudini kwenu!” Wanaoambiwa wanajisikiaje? Wafanye nini?
Waweke maneno pembeni na kuanzisha vita vya kuondoa ubaguzi; kwa misaada na ushirikiano kimataifa? Mhusika “hajafutwa.”
Eti nini? Sikilizeni anayejiita mnyofu. “…tutashinda hata kwa bao la mkono…” Ni kauli katikati ya vuguvugu la kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana. Ofisa wa “chama tawala” anatangazia taifa na dunia; kwa kiburi na jeuri isiyomithilika.
Anapeleka ujumbe gani kwa washindani kutoka vyama vingine? Anaeneza demokrasia? Anataka washindani wafanye nini? Anataka Tume ya Uchaguzi ikitangaza kuwa wameshindwa; wafanye nini na Serikali ijibu vipi? Mhusika “hajafutwa.”
Nina zaidi ya kauli 100 za aina hii zilizotoka vinywani mwa viongozi wa Serikali na chama kinachopanga Ikulu. Wahusika wanafyatua maneno kwa jeuri: Maneno ya kukera, kuudhi, kuchukiza, kutisha, kuchokoza, kudhalilisha, kubagua; yote kwa shabaha ya kuchochea majibu kwa njia ya mapigano – vita! Vyombo vya habari vimenukuu baadhi ya kauli hizi na nyingine zimesomwa katika maandiko mbalimbali; katika vijarida na mbao kwenye vijiwe vya vijana na wazee.
Wako wapi walio wakali sana ndani ya Serikali, wawezao kupambana na uchochezi huu, unaoweza kuangamiza Taifa? Uko wapi ‘mkono mrefu’ wa Serikali ambao hutamkwa kwa majigambo pale polisi wanapokuwa wakikimbiza “mwizi wa karanga.”
Upande huu kuna watoa kauli zinazotaka watu wachukie, wakasirike, waghadhibike; wachukue walichonacho na kuanza kumalizana; huku Serikali ikiwaangalia kana kwamba imewafadhili kwa kazi hiyo.
Upande mwingine kuna habari na taarifa za ‘kigazeti’ Mawio, kinachoanika wanaopanda mbegu ya maangamizi na kuonya juu ya mifarakano iwezayo kuleta umwagaji damu.
Waziri Nape anasema Mawio ndilo linafanya uchochezi. Analifuta. Hawezi kujifuta. Hawezi kufuta wengine waliobobea katika uchokozi wa kibabe na uchochezi.
Kufuta chombo cha habari ni kurejesha jamii katika nyakati za ujima. Ni kukataa elimu na maarifa. Ni kupora uhuru wa habari. Ni kupanda mbegu ya woga miongoni mwa wananchi. Ni kuingiza Taifa gizani.
Nape hana tofauti na mawaziri waliomtangulia, waliotumika kudhibiti habari kwa kukaa wamepakata na kubusu sheria ya kidikteta inayotumika kufuta vyombo vya habari, Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.
Wasiliana na Meza ya Mhariri wa Jamii kwa simu 0713 614872 au 0763679229    

0 comments:

-