Ukomo wa madaraka wa Rais wa
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein umeibua utata na kusababisha wanasheria
na polisi kutoa tafsiri zinazokinzana.
Wakati Chama cha
Wanasheria wa Zanzibar (ZLS) kikisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar
tarehe ya mwisho ya Dk Shein kuingia ofisini ni leo Novemba 2, polisi
kwa upande wao wanasema Rais huyo anatakiwa kushika madaraka hayo hadi
pale rais mpya atakapoapishwa.
Rais wa ZLS, Awadh Ali
Said alisema mwishoni mwa wiki kuwa moja ya athari za tamko la Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi wa Zanzibar ni kusababisha
mgogoro wa kikatiba hasa katika muda wa rais kushika madaraka.
Said
alisema Ibara ya 28 (2) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 inaeleza kuwa
Rais ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia
tarehe alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais.
Alisema
tafsiri yake ni kuwa tangu Dk Shein alipokula kiapo cha uaminifu na
kiapo cha kuwa rais Novemba 3, 2010 atakuwa ametimiza miaka mitano
Novemba 2, 2015.
“Hivyo akiendelea kushikilia madaraka ya urais zaidi ya tarehe hiyo itakuwa kinyume na Katiba ya nchi,” alisema.
Kutokana
na madai hayo, Jeshi la Polisi Zanzibar limewatahadharisha wananchi
kutojihusisha na vitendo vya fujo kwa madai kwamba kuanzia leo
hakutakuwa na Serikali.
Walichosema ZLS
Kwa
mujibu wa Rais wa ZLS, maudhui ya Ibara 28 (1) hiyo ni kumpa uwezo wa
kikatiba Rais kuendelea ili kutoa nafasi ya maandalizi ya kula kiapo kwa
Rais anayefuata tu na si kuendelea kukaa madarakani bila ya kufanyika
kwa uchaguzi au kwa sababu ya Uchaguzi kufutwa.
Hata
hivyo Said alisema nchi kuendeshwa muda mrefu bila ya Baraza la
Wawakilishi (MBW) kama mazingira yaliyopo yanavyoonyesha ni tatizo.
Alisema
Katiba ya Zanzibar imeruhusu hali ya kuendesha nchi bila ya BLW kwa
muda usiozidi siku tisini (90) tu kuanzia siku Baraza lilipovunjwa.
“Kwa
mazingira tuliyonayo, siku tisini (90) zinazokubalika kikatiba
zinaishia Novemba 12, 2015 kwa kuwa BLW lilivunjwa Agosti 13, 2015,”
alisema.
Rais huyo wa TLS alionyesha pia hatari ya kuwa
na rais ambaye yuko juu ya Sheria na Katiba, akibainisha Ibara ya 37 ya
Katiba ya Zanzibar ya 1984 inayoipa Mamlaka Baraza la Wawakilishi
kuondoa kinga ya Rais kutoshtakiwa anapokuwa madarakani kama
inavyotolewa na Ibara ya 36 ya Katiba.
Alisema katika
mazingira yaliyopo hivi sasa ambapo ifikapo tarehe 12 Novemba, 2015,
Baraza la Wawakilishi halitakuwapo na haliwezi kuitishwa kikatiba, ni
wazi kuwa ikiwa Rais atafanya matendo yoyote yenye kuvunja katiba ya
nchi na kukiuka kiapo chake, hakutakuwa na mamlaka nyingine yoyote yenye
uwezo wa kuhoji matendo ya Rais.
Alidai hii inatoa fursa na inatengeneza hatari ya kuwa na Serikali inayoongozwa na ‘dikteta’.
Kauli ya Polisi
Kamishna
wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame alisema jana kuwa kutokana na
taarifa hizo za wanasiasa na watu wengine, huenda wananchi watakuwa huru
kufanya watakavyo na hivyo kuvunja sheria.
“Tunawaomba
wananchi kuacha ushabiki na jazba ili kuwaepusha na gharama za
matatizo, wao wenyewe na familia zao. Waswahili wanasema ‘vyako ni
vyako, likikupata ni la kwako na kila mchumia janga hula na mwanawe’,’’
alisema Kamishna Makame.
Makame alisema ni vyema
kipindi hiki kuhubiri amani na kuwa na subira kuiachia ZEC ambayo ndiyo
yenye dhamana na mamlaka ya kutangaza tarehe ya kurejewa kwa uchaguzi na
si mtu mwingine.
Kamishna Makame alinukuu kifungu cha 28 (1) cha Katiba
ambacho pia wanasheria wa ZLS walikitoa na kumwomba Rais wa Zanzibar
kuchukua tahadhari ili asiwe wa kwanza kuvunja Katiba ya Zanzibar kwa
kuvuka terehe ya mwisho kuwapo madarakani.
Kifungu cha
28 (1) cha Katiba kinasema, “Kufuatana na Katiba hii mtu ataendelea kuwa
Rais mpaka (a) Rais anayefuata ale kiapo cha kuwa Rais, au (b)afariki
wakati akiwa Rais, au (c) hapo atakapojiuzulu; au (d) iwapo amechaguliwa
kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ; au (e) kwa sababu yoyote
nyingine ameacha kuwa kiongozi kwa mujibu wa vifungu vingine vya katiba
hii.
“Ikumbukwe kuwa kutokuwapo Rais wa nchi kama
inavyodaiwa, haimaanishi sheria hazipo na watu wafanye watakavyo. Kuna
makosa ukiyafanya moja kwa moja sheria itachukua mkondo wake ikiwamo
kufanya kitendo cha uvunjifu wa amani, kufanya maandamano au mikusanyiko
ya watu isiyo halali,” alisema kamishna huyo.
Lipumba: Ni jukumu la JK
Sakata
hilo la Zanzibar kwa mara ya pili lilimwibua mwenyekiti wa zamani wa
Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba akimtaka Rais Jakaya
Kikwete kumaliza tatizo la Zanzibar kwa kuiamuru ZEC kumtangaza mshindi
wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 ili kuliepusha Taifa lisiingie kwenye
machafuko.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Lipumba alisema ni muhimu Kikwete akahakikisha anatekeleza hilo kabla ya
kumaliza muda wake, badala ya kumwongezea matatizo na mzigo rais mpya,
Dk John Magufuli anayetarajiwa kuapishwa Novemba 5.
“Alhamisi
ijayo Dk John Magufuli ataapishwa kuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa
Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Tanzania, Kikwete usimwongezee Magufuli
matatizo, yaliyopo yanamtosha,” alisema Lipumba ambaye wiki iliyopita
akizungumzia pia mgogoro huo akiitaka ZEC imtangaze mshindi.
Lipumba
aliyepokewa na wafuasi zaidi ya 100 kwenye ofisi za makao makuu ya
chama hicho, Buguruni , Dar es Salaam, alisema amelazimika kutoa ushauri
huo baada ya kuona hatari iliyo mbele, iwapo wananchi wa Zanzibar
watanyang’anywa haki yao.
“Vigogo wa Tanzania na
Zanzibar wasisubiri hadi maafa yatokee ndipo waanze kuchukua hatua,
watumie muda huu kuyazuia,” alisema na kuonya:
“Nayakumbuka
mauaji ya wafuasi wa CUF yaliyotokea mwaka 2001 na wengine kukimbilia
uhamishoni Shimoni nchini Kenya, nimeona kukaa kimya kutaleta madhara
katika nchi hii,” alisema.
Mmoja wa wanachama wa chama
hicho, tawi la Buguruni, Ashura Mohammed alisema ni muhimu Wazanzibari
wapewe haki yao kwa matokeo ya uchaguzi walioufanya kutangazwa.
ADC : Jecha, ZEC wamekosa sifa
Wakati
huohuo, Mwenyekiti wa chama cha ADC, Said Miraaj Abdulla amesema ZEC
chini ya Jecha Salim Jecha haiwezi kusimamia tena uchaguzi wa Zanzibar
baada ya siku 90 kwa sababu ina mapungufu mengi kama ilivyoyaainisha
yenyewe.
Abdulla alisema sababu zilizotolewa na Jecha
kufuta matokeo hazina mashiko, zimelenga kuficha ukweli na kutetea
maslahi ya upande mmoja. Alisema chama chake kitasimamia haki na ukweli
kuhakikisha kwamba matakwa ya wananchi yanasikilizwa.
“Kwanini
Jecha aje leo kutueleza kuwa tume yake iliingiliwa na wanasiasa? Siku
zote alikuwa wapi na alichukua hatua gani katika kuhakikisha tume yake
inakuwa huru,” alihoji mwenyekiti huyo na kusisitiza kuwa kuna ajenda
inafichwa na Jecha.
Mwenyekiti huyo aliendelea kusema,
Jecha alisisitiza katika matamshi kwamba wajumbe wa ZEC walikuwa
wamegawanyika kwa misingi ya vyama vyao lakini hakueleza ni kwa namna
gani mgogoro wa wajumbe hao umeathiri kura zilizopigwa.
Aliwataka
viongozi kuwa makini na matamshi yao ili yasije kusababisha migogoro na
kuvunja amani ya nchi na vyama vyote kuwa na sauti moja ili viweze
kutetea haki za wananchi wa Zanzibar ambao wamechagua viongozi wao kwa
misingi ya kidemokrasia.
“Viongozi wa CUF na CCM waache
kuangalia maslahi ya vyama vyao bali waangalie maslahi mapana ya umma.
Chama changu kiko tayari kushirikiana na chama chochote katika
kuhakikisha kwamba suluhu ya mgogoro huo inapatikana,” alisema.
Imeandikwa na Salma Said, Raymond Kaminyoge na Peter Elias
0 comments:
Post a Comment