Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), imesema ongezeko la wapigakura limetokana na idadi hiyo
kuongezeka baada ya kufanya uhakiki kwenye Daftari la Kudumu la
Wapigakura kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Kabla ya uchaguzi
huo uliofanyika Jumapili iliyopita, katika taarifa yake, tume ilisema
jumla ya wapiga kura 23.78 milioni waliandikishwa katika Daftari la
Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR).
Baadaye
tume hiyo ilipochambua taarifa za daftari hilo ilibaini kasoro na
kuondoa wapiga kura zaidi ya milioni moja na kubaki na wapiga kura 22.75
milioni.
Daftari hilo lilibaki NEC huku vyama vya
siasa vikipewa nakala za daftari kwa ajili ya kumbukumbu zao. Hata
hivyo, maswali yaliibuka siku NEC ilipotangaza matokeo ya urais baada ya
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva kusema watu
waliojiandikisha kupiga kura idadi yao ni 23 milioni, idadi ambayo ni
sawa na ile ya awali kabla ya wale milioni moja kuondolewa.
Kati ya hao, waliopiga kura walikuwa 15,589,639.
Utata
huo umeshalalamikiwa na baadhi ya vyama vya upizani vikiwamo vile
vinavyounda Ukawa ambavyo viliitaka NEC kutoa ufafanuzi. Kaimu Mkuu wa
Kitengo cha Habari NEC, Clarence Nanyaro akizungumza na gazeti hili
jana, alisema ongezeko hilo limekuja baada ya kupeleka daftari kwenye
vituo walikojiandikisha watu kwa ajili ya uhakiki.
Alisema
kuna watu waliojiandikisha na walipokwenda kuhakiki majina yao kwenye
vituo walivyojiandikisha, hayakuonekana kwenye takwimu za tume.
“Tulifanya
uhakiki siku za mwisho karibu na uchaguzi na kubaini kulikuwa na watu
wengi ambao majina yao yalikuwa hayaonekani,” alisema Nanyaro
Alisema kutokana muda kuwa mdogo, hawakuweza kutoa nakala nyingine kwa vyama vya siasa kama walivyofanya awali.
0 comments:
Post a Comment