Friday, October 30



MBUNGE wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, Ridhiwani Kikwete amesema hana chuki kwa wale ambao hawakumpigia kura kwenye uchaguzi uliofanyika Jumapili kwani hizo ni changamoto za uchaguzi.

Aliyasema hayo jana kwenye Uwanja wa Miembe Saba mjini Chalinze wakati wa mkutano wa hadhara wa kuwashukuru Wanachalinze kwa kumchagua kuwa mbunge kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumapili.

Ridhiwani alisema licha ya baadhi ya maeneo kutompigia kura za kumchagua kuwa mbunge, lakini atawatumikia wananchi wote bila ya kujali kama walimpigia kura au la kwani kila mtu ana haki ya kumpigia kura mgombea yeyote anayempenda.

“Nawashukuru wananchi wote walionipigia kura na hata wale ambao hawakunipigia kura kwani hiyo ndiyo demokrasia nitahakikisha nawahudumia wananchi wote bila ya kuwabagua nitahakikisha napeleka maendeleo kwa watu wote wa jimbo hili,” alisema Ridhiwani.

Alisema kutopigiwa kura kwa wingi siyo sababu ya kuwagawa wananchi kwani hizo ni changamoto za uchaguzi ambao unakuwa na mambo yake ambapo baadhi ya maeneo walipiga kura kwa kuzingatia ukabila.

“Sitakuwa na chuki wala hasira kwa wale ambao hawakunipigia kura nitashirikiana nao katika suala la maendeleo ili kuhakikisha jimbo letu linakuwa na maendeleo na wananchi wanaboresha maisha yao ili yasonge mbele,” alisema Ridhiwani.

Aidha, alisema atahakikisha Mji wa Chalinze ambao umekuwa Halmashauri ya Mji Mdogo unajengwa kwa kuwekewa huduma muhimu ili wananchi waboreshe biashara zao hasa ikizingatiwa kuwa mji huo ni wa kibiashara.

“Moja ya mambo nitakayoyafanya ni kufanya Chalinze kuwa makao makuu ya Halmashauri hiyo na baadaye kuwa wilaya kwani mchakato unaendelea na tunaamini baada ya muda tutapewa wilaya hivyo tutaweza kujitegemea na kujiimarisha kiuchumi,” alisema Ridhiwani.

Alibainisha kuwa wananchi wasiwe na wasiwasi kwani kukichagua Chama Cha Mapanduzi CCM ni kuchagua maendeleo hivyo wasubiri kuona jinsi serikali mpya itakavyofanya kazi kwani kwao ni kazi tu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Chalinze, Nasa Karama alisema mbunge huyo ameonesha uwezo mkubwa kwani kwa kipindi alichochaguliwa cha mwaka mmoja na miezi mitatu amefanya mambo makubwa ambapo alitumia ziadi ya Sh bilioni moja na zaidi miradi ya maendeleo.

0 comments:

-