Monday, September 7

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. 
 Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kesho anatarajia kujibu mapigo kuhusu tuhuma dhidi yake zilizotolewa na Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ambaye hivi karibuni alimweleza kuwa ni mshenga wa Edward Lowassa kwa viongozi wa Chadema.
Akizungumza jana katika kanisa hilo lililopo Ubungo huku akishangiliwa na waumini wake waliokuwa wakiimba; “mshenga, mshenga, mshenga...’ Gwajima alisema kuna watu wanaodhani kwamba atazungumza masuala ya Dk Slaa kanisani hapo.
“Leo sitazungumzia masuala hayo hapa kwa kuwa hili si pango la wanyang’anyi ila nitazungumza na vyombo vya habari Jumanne ijayo (kesho),” alisema.
Jumanne iliyopita, Dk Slaa alimwita Gwajima kuwa ni mshenga akisema ndiye aliyefanya mipango ya kufanikisha mkakati wa Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa kujiunga na Chadema kwa kumkutanisha na viongozi wa chama hicho.
Gwajima alikiri kuwaunganisha Chadema na Lowassa na kueleza kuwa amekuwa rafiki wa wote hao.
Gwajima alisema mkutano na wanahabari utafanyika kesho saa 7 mchana katika Hoteli ya Landmark Ubungo na utarushwa moja kwa kwa moja na televisheni kadhaa.
“Kwa hiyo hapa leo tusikilize neno la Mungu masuala mengine hapa si mahali pake tusubiri siku hiyo nitakayokuwa Landmark,” alisema.
Alisema mkutano huo utakaochukua saa moja utaanza saa 7.00 mchana.

0 comments:

-