Monday, September 7

Pengine kituo cha redio cha eFM ndio habari ya mjini kwa sasa. Kwenye daladala, vijiweni, sokoni
Mkude Simba
Pengine kituo cha redio cha eFM ndio habari ya mjini kwa sasa. Kwenye daladala, vijiweni, sokoni na kwenye baa nyakati za asubuhi, lazima ukute watu wanasikiliza redio hiyo ambayo imeanza kwa nguvu mwaka huu kwa kuajiri watangazaji maarufu kutoka vituo mbalimbali vya redio nchini.
Lakini kivutio kikubwa na matangazo yake yanayowekwa kwa ajili ya kuitangaza redio hiyo.
Ndani ya matangazo hayo yumo Mkude Simba, ambaye vichekesho anavyobuni huwavunja mbavu wengi.
Vichekesho hivyo huwa katika mfumo wa majibizano baina ya mtu mmoja anayeonekana kuwa ni mbumbumbu asiyejua kitu na mwingine ambaye humuuliza maswali kuhusu mambo mbalimbali.
“Ilikuwa kama zari tu,” anasema Mkude Simba, ambaye jina lake halisi ni Musa Yusuf au Kitale.
“Ilituchukua muda mrefu kuhangaikia maisha yetu kimaisha. Watu wengi walikuwa wakituchukulia poa tu. Hawakuelewa umuhimu wetu.
“Tulikuwa tukirusha vichekesho vyetu kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo whatsapp mpaka ilipofika muda Mkurugenzi wa efm, Majey alipotaka kumjua Mkude Simba ni nani.”
Mkude Simba anasema kuwa mkurugenzi huyo aliomba wakutane ili kujadili kipaji chake na kuafikiana masuala ya kazi.
Leo hii, Mkude Simba ni jina kubwa katika ulimwengu wa redio, na karibu redio zote zinajaribu kutengeneza matangazo yanayoiga vichekesho vya Mkude Simba, lakini inaonekana bayana kuwa kumfikia msanii huyo wa filamu itakuwa kazi kubwa.
Mkude Simba ni maarufu katika uigizaji wa vichekesho na anajulikana kwa kuigiza mtu anayezungumza lugha ya Kilugulu.
Mkude Simba, ambaye kwa sasa ni mtangazaji wa kituo cha runinga cha Azam, anasema ameamua kutumia lugha hiyo baada ya kugundua kuwa wasanii wengi hawaitendei haki katika uigizaji wao.
Kwa zaidi ya miaka 13, Mkude Simba amekuwa akijulikana kupitia uhusika wake wa uteja katika kila kazi ambayo amekuwa akifanya.
Mkude Simba ambae ni mmiliki wa kampuni ya usambazaji filamu ya Macho Media, anasema jambo lilomfanya kuingia katika uchekeshaji ni kushindwa kufanya vizuri katika fani nyingine.
“Nilianza kuigiza kawaida muda mrefu, lakini sikuwahi kuona dalili za kutimiza ndoto zangu kitu ambacho kilinisukuma kujaribu kuwa na mwelekeo tofauti wa utafutaji maisha,” anasema.
Anasema jina lake lilianza kujulikana mwaka 2003 alipoanza kuonekana katika kituo cha Televisheni ya Taifa (TVT, sasa TBC1) na alikuwa akifanya mazoezi na kundi la Kaole Arts.
Mwaka 2006 tamthilia ya Jumba la Dhahabu ilianza kufanyiwa mazoezi na wakati inaanza kurushwa TBC alipishana lughai na mkurugenzi wake na akaamua kuondoka. Baada ya muda wasaniiu wengine 35 walitoka kundi hilo n akumtafuta kwa lengo la kuanzisha kundi jipya.
Anasema baadaye alianzisha kundi lililoitwa Jumba Arts ambalo lilitunga tamthilia ya Elikanza.
Hata hivyo, Mkude Simba anasema kuwa hawezi kumsahau rafiki yake mpendwa, Sharo millionea, ambaye jina lake halisi ni Hussein Mkieti kwa kuwa ni mmoja kati ya watu waliompa changamoto sana katika maisha.
Anasema baada ya kuanzisha kundi hilo alifanikiwa kumshawishi Sharo Milionea kujiunga naye.
Anafafanua kuwa walianza kufanya kazi na Sharo Milionea mwaka 2008 baada ya kutoka Jumba Arts Group kutokana na changamoto ambazo rafiki huyo alikutana nazo pale kutoka kwa wanakikundi.
Anasema akiwa na rafiki huyo, walifanya kazi kadhaa ikiwamo Bad Night, Mbwembwe, Mtoto wa Mama, Back from Newyok, Back from Prison pamoja na kipindi cha vichekesho cha Vituko Show kilichokuwa kikionyeshwa kituo cha runinga cha Channel Ten.
Hata hivyo, Mkude Simba anasema kuwa anapata wakati mgumu kutokana na jamii kumuona mtu wa ajabu.
“Situmii dawa za kulevya, sinywi, wala sivuti sigara lakini watu wengi wanavyoniaona hudhani kuwa natumia vitu hivyo... ni kazi tu,” anasema nyota huyo wa vichekesho.

0 comments:

-