Na. Julius Mtatiro -
(TAHADHARI:
Kama una Jazba usichangie POST hii - Utakufa kwa Presha Bure, Posti hii
inaweza kuibua hisia kali, hofu, wasiwasi na majuto ikiwa unakubaliana
na maoni haya au unayapinga na ikiwa mgombea wako amegongwa mahali hapa
au ameparazwa, jadili hoja wala usimguse mtoa hoja)
Ndugu zangu,
Jana Chama Cha Mapinduzi kimetoa orodha ya wagombea wake nchi nzima.
Katika orodha hiyo kuna watuhumiwa wengi tu wa masuala ya ufisadi, kuna
watuhumiwa wengi wa rushwa na wengine walikamatwa na kuhojiwa na
TAKUKURU, kwa kifupi kuna watuhumiwa kibao sana.
Lakini kubwa kuliko yote USHAHIDI WA WAZI unaonesha kuwa hakuna mgombea
hata mmoja wa CCM anaweza kupita kwenye kura ya maoni nchi nzima bila
kutoa rushwa kubwa na ndogo, kwa wapiga kura wa kawaida na kwa viongozi
wanaosimamia uchaguzi. Nina marafiki zangu wengi tu wameshinda na
kushindwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM, kila mmoja (aliyeshinda na
aliyeshindwa) wanasema kuwa PESA ndiyo inaamua nani hasa apitishwe ndani
ya CCM.
Leo nataka kumuuliza ndugu yangu Humphrey Polepole na
aje hapa anijibu kwa hoja. Je, msimamo na mtizamo wake juu ya rushwa
ndani ya CCM uko namna gani? Nilipofuatilia mjadala kati yake na
Mchungaji Msigwa nilimuona Polepole akisisitiza kuwa kiongozi
akishatuhumiwa tu anapoteza political legitimacy ya kuwa kiongozi kwa
sababu anakuwa amepoteza "moral authority" (mamlaka ya kimaadili).
Polepole amesisistiza kuwa Lowassa ni mtuhumiwa mkubwa wa ufisadi hasa
kwenye eneo la RICHMOND na kwamba hawezi kumuunga mkono, katika hilo
nakubaliana naye. Lakini pia nilitaraji Polepole atueleze kuwa Magufuli
pia ni mtuhumiwa mkubwa wa ufisadi na hasa akihusishwa na uuzaji holela
wa nyumba za serikali kwa manufaa binafsi na kuwapatia ndugu zake nyumba
nyingine zenye thamani kubwa.
Kama kutuhumiwa tu kwa masuala ya kuvunja maadili kunamfanya mtu anyimwe
haki ya kuwa kiongozi basi mwaka huu tumeingizwa chaka na CCM na UKAWA!
Kwamba vyama vyote vimesimamisha wagombea ambao ni watuhumiwa wa
ufisadi lakini hakuna mmoja kati yao aliyewahi kuthibitishwa kwamba
amekula pesa ngapi kwenye ufisadi huo.
Polepole alikwenda mbali zaidi na kutoa sharti kubwa kwa uongozi wa juu
wa CCM, kwamba uongozi huo ukate wabunge wote ambao wana tuhuma au
wamepita kwa njia ya rushwa. Kwa bahati mbaya sana watuhumiwa wote wa
ufisadi na rushwa ndani ya CCM wamerejeshwa kugombea ubunge na nyadhifa
zingine, kina Andrew Chenge a.k.a Vijisenti, kina Prof. Tibaijuka a.k.a
Hela ya Mboga n.k. Kuna watuhumiwa wengine wa utoaji rushwa wakati wa
kura za maoni za CCM ambao walikamatwa na TAKUKURU na kuhojiwa, wote
hawa wameshapoteza MORAL AUTHORITY na POLITICAL LEGITIMACY!
Polepole njoo usaidie kueleza watanzania nini ni mtizamo wako juu ya
uchaguzi huu ambao CCM imesimamisha mgombea urais ambaye ni mtuhumiwa
namba moja wa ufisadi wa UUZAJI WA NYUMBA ZA SERIKALI na UKAWA
imemsimamisha mgombea ambaye ni mtuhumiwa wa ufisadi wa RICHMOND. Njoo
utueleze msimamo wako juu ya uchaguzi ambao CCM imesimamisha zaidi ya
robo tatu ya wabunge ambao ni watuhumiwa wa ufisadi mkubwa na utoaji
rushwa wa wazi kwenye kura ya maoni dhidi ya UKAWA ambayo imesimamisha
takribani zaidi ya ROBO TATU ya wabunge ambao hawajawahi kujihusisha na
ufisadi wala kutoa rushwa kwenye kura za maoni za ndani ya vyama.
Na mwisho njoo utueleze tatizo la Rushwa na Ufisadi ni la kimfumo zaidi
au ni la mtu? Njoo utueleze kuwa ni nani yuko kwenye nafasi nzuri ya
kupambana na ufisadi, Magufuli ambaye yumo bado ndani ya CCM au Lowassa
ambaye yuko nje ya CCM.
Njoo utueleze ni nani anaweza kupambana na ufisadi, ni Magufuli
Mtuhumiwa wa Ufisadi wa Nyumba za Serikali ambaye amezungukwa na robo
tatu ya wabunge waliotumia rushwa na uvunjaji wa maadili kupita kwenye
kura za maoni au ni Edward Lowassa mtuhumiwa wa Ufisadi wa Richmond
ambaye amezungukwa na wabunge waadilifu na wazalendo waliopita kwenye
kura za maoni bila kuhonga wala kutoa rushwa nikiwemo mimi Mtatiro.
Na je baada ya CCM kuwapitisha watuhumiwa wa rushwa lukuki kugombea
ubunge kwenye kampeni za mwaka huu bado utakipigia debe chama chako CCM?
Wala jazba hazihitajiki katika kujadili, tunahitaji hoja kwa wachangiaji
wote, tusiwe wanafiki, kama unakula Nguruwe hebu kunywa na mchuzi wake,
huwezo kujidai huli nguruwe huku unakunywa mchuzi wake "daily".
Leo nimepasua JIPU kama Malisa Godlisten!
Dar Es Salaam.
0 comments:
Post a Comment