Dk John Magufuli (Kushoto) na Edward Lowassa (kulia)
Dar es Salaam. Wakati zikiwa zimesalia siku 14
kabla ya kuanza kwa kampeni za urais, ubunge na udiwani, macho na
masikio ya wengi yanaelekezwa kwa wagombea wawili kutoka vyama vikuu vya
siasa, Dk John Magufuli wa CCM na Edward Lowassa wa Chadema, ambao
uchambuzi wa gazeti hili unaonyesha wana mengi yanayoshabihiana.
Wawili
hao ni kati ya makada saba waliosimamishwa na vyama saba kuwania urais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambao inaelekea kuwa ndiyo
watakaochuana vikali, hasa kutokana na ukweli kuwa Dk Magufuli anatoka
chama tawala na Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu, anaungwa mkono na
vyama vinne vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wengine wanaowania urais ni
Mchungaji Christopher Mtikila wa DP, Chifu Lutayosa Chemba (ADC),
Macmillan Limo (TLP), Hashimu Rungwe (Chauma), Fahami Dovutwa (UPDP) na
mgombea wa ACT Wazalendo ambaye bado hajateuliwa.
Pamoja
na kwamba katika siasa lolote linaweza kutokea, wagombea hao watano
hawatazamiwi kuweka ushindani mkubwa zaidi ya ule wa Dk Magufuli na
Lowassa.
Dk Magufuli hakutarajiwa kupita kwenye mbio za
urais ndani ya CCM, ambako Lowassa na vigogo wengine walikuwa wakipewa
nafasi kubwa, lakini ushindi wake umemfanya awe mgombea wa chama chenye
mtandao mkubwa nchini na hivyo mwanzoni kupewa nafasi kubwa ya kushinda.
Hata
hivyo, uamuzi wa Lowassa kujivua uanachama wa chama kilichomlea na
kilichompa umaarufu mkubwa, umebadili upepo na sasa vita ya kuingia
Ikulu Oktoba 25 inaonekana kuwa ya watu hao wawili.
Gazeti
la Mwananchi linaangalia sifa ambazo wawili hao wanashabihiana pamoja
na tofauti zao, kwa kuzingatia maelezo ya wachambuzi wa masuala ya
kisiasa.
Wote wamesomea ualimu
Moja ya
mambo ambayo wawili hao wanashabihiana ni kusomea ualimu, ingawa wa
fani tofauti. Dk Magufuli, ambaye atakuwa akitimiza miaka 56 siku nne
baada ya Uchaguzi Mkuu, ni mwalimu aliyejikita kwenye masomo ya kemia na
hesabu.
Alipata diploma ya ualimu mwaka 1982 kwenye
Chuo cha Elimu Mkwawa, kabla ya kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
ambako alipata shahada yake ya kwanza, ya umahiri na ya uzamiri
akijikita kwenye somo la kemia.
Lowassa, ambaye Agosti
26 atakuwa akitimiza miaka 62, alisomea shahada ya ualimu Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam mwaka 1977, lakini shahada yake ya uzamili ilijikita
kwenye masomo ya maendeleo ya jamii.
Dk Magufuli
alitumia taaluma yake kufundisha kemia na hesabu kwenye Shule ya
Sekondari ya Sengerema, lakini Lowassa hakufundisha.
Wote ni makini
Pengine
ni kutokana na maadili ya ualimu, wawili hao wamedhihirisha kuwa ni
watu makini katika utendaji wao, jambo ambalo limekuwa likiwafanya watu
wanaofanya kazi chini yao kuwa na wasiwasi kila wanapowapeleka taarifa.
Dk
Magufuli na Lowassa hutumia muda mwingi kujiridhisha na taarifa
wanazopelekewa kabla ya kufanya uamuzi ambao wakati mwingine huonekana
kama wamekurupuka.
Mhandisi mmoja ambaye amewahi
kufungiwa leseni na Magufuli aliiambia Mwananchi kuwa kosa moja kubwa
alilofanya ni kumwandikia Dk Magufuli taarifa ndefu, lakini iliyojaa
mambo yasiyo sahihi.
Anasema kuwa aya hiyo ilikuwa ukurasa wa 20, lakini ndani ya muda mfupi Magufuli aliibaini na kibarua chake kiliota nyasi.
Hali
ni kama hiyo kwa Lowassa, ambaye akiwa Waziri Mkuu aliwahi kumtimua
mkandarasi wa Wilaya Temeke kwa kushindwa kukagua ujenzi wa maghorofa
ikiwemo la Chang’ombe Village lililoporomoka na kusababisha maafa ya mtu
mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa mwaka 2006.
Uchapakazi
Mbali
na umakini, wawili hao wamedhihirisha kuwa ni wachapakazi hodari katika
wizara na taasisi walizopitia kiasi cha kujijengea jina kubwa kwa
wananchi.
Utendaji wa Dk Magufuli hauna shaka na
ameshaeleza bayana kuwa hapendi wazembe na wasiowajibika sanjari, kama
Lowassa ambaye hata siku ya kwanza alipoingia ofisini mwaka 2005
aliwataka wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuacha kufanya kazi kwa
mazoea.
Wakati Dk Magufuli alipohamishiwa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, wengi walidhani kuwa amemaliza kisiasa, lakini mbunge
huyo wa Chato alifanya kazi kubwa ya kutambua fursa za kiuchumi zilizoko
hasa kwenye uvuvi na akafanikiwa kuonyesha ni kiasi gani Serikali
ilikuwa ikipoteza fedha.
Wakati huo, Tanzania iliingia
makubaliano na Afrika Kusini na nchi nyingine za ukanda huu kufanya
doria kwa pamoja kwenye pwani ya Afrika Mashariki na juhudi hizo
zilifanikiwa kunasa meli ya Tawaliq 1 iliyokuwa na samaki wenye thamani
ya Sh20 bilioni.
Uchapakazi wake umedhihirika hasa
kwenye ujenzi wa barabara, akiwa amefanikiwa kuunganisha takriban mikoa
yote ya Tanzania katikja kipindi alichokaa Wizara ya Ujenzi.
Lowassa
anaonekana zaidi katika kusimamia utekelezaji wa mradi wa maji ya Ziwa
Victoria katika shughuli za maendeleo baada ya mpambano mkali dhidi ya
Misri, ambayo ilikuwa na ukiritimba wa maji hayo kabla ya nchi tano
kuungana na kusaini makubaliano ya matumizi ya maji hayo.
Lowassa
pia anajinadi na mafanikio ya ujenzi wa shule za kata, ambazo kwa kiasi
kikubwa zimefanikisha watoto wengi kupata elimu kwa gharama nafuu,
ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ambao aliufanya kwa kukutanisha mifuko
ya hifadhi ya jamii na kuiamuru ichangia gharama za ujenzi.
Jambo
lingine walilonalo Dk Magufuli na Lowassa ni misimamo. Dk Magufuli ni
kiongozi mwenye misimamo isiyotia shaka na siku zote husimamia
anachokiamini, sanjari na Lowassa, ni mwenye misimo yake na itakumbukwa
alipokuwa Waziri wa Maji na baadaye Waziri Mkuu alionyesha misimamo.
Dk
Magufuli alitofautiana hata na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati
aliposimamia uendeshaji wa kivuko cha Kigamboni, na suala la kiwango cha
mizigo inayobebwa na malori.
Moja ya kauli
zilizonukuliwa sana ni ile ya “asiyekuwa na nauli ya kulipia kivuko,
apige mbizi”, ambayo ilitafsiriwa kuwa ya kutojali wananchi, lakini
faida zake ndio zinamfanya aonekane kuwa msimamo wake ulilenga
kunufaisha wananchi.
Hali kadhalika Lowassa anajulikana
kwa kusimamia uamuzi kama wa kubomoa maghorofa yaliyojengwa kinyume na
sheria Masaki jijini Dar es Salaam. Msimamo wake pia kwenye suala la
mkataba wa City Water iliyokuwa ikihusika na ugavi wa maji jijini Dar es
Salaam ndio uliosababisha uvunjwe.
Ufuatiliaji
Lowassa
na Dk Magufuli pia wanajulikana kwa kuwa wafuatiliaji wazuri kwa watu
walio chini yao au wanaofanya kazi chini ya mamlaka zao. Dk Magufuli,
ambaye anajulikana kwa kukariri tarehe, kiwango cha miradi, urefu wa
barabara na kiwango cha fedha zilizotengwa kwenye miradi, hutumia
talanta hiyo kufuatilia miradi mbalimbali na hasa muda wa kumalizika,
hali inayomfanya kila mara atishia kuvunja mikataba na wakandarasi au
kuivunja kabisa.
Hilo pia limekuwa likifanywa na
Lowassa, ambaye akiwa Waziri Mkuu alikuwa akihakikisha wakuu wa wilaya
na mikoa wako sehemu zao za kazi na yeyote ambaye alitaka kutoka
alitakiwa awe na kibali, kwa mujibu wa baadhi ya watu waliofanya kazi
naye.
Udhaifu
Mbali na sifa hizo
nzuri, wanasiasa hao wanashabihiana katika udhaifu, hasa uamuzi wa papo
kwa papo ambao pia husababishwa na kiu yao ya kutaka kuona kazi
inafanyika.
Wote wawili hufanya uamuzi wa papo kwa pamo
ambao wakati mwingine huwa na athari za kisheria. Uamuzi kama huo huwa
na kadhia kwa wafanyakazi na makandarasi wanaopewa zabuni mbalimbali na
Serikali.
Hawaachi mfumo wa utendaji
Udhaifu
mwingine wa wawili hao ni hali ya kujituma wao bila ya kutengeneza
mfumo ambao unaendeleza ufanisi na badala yake wanapoondoka, hali
hubakia kama ilivyokuwa awali.
Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Dk Magufuli kwenye wizara alizopitia kama ya uvuvi na hali kadhalika kwa Lowassa.
Pia wanatofautiana
Tofauti
kubwa kati ya Dk Magufuli na Lowassa ni mgombea huyo wa CCM kutokulia
ndani ya chama na badala yake amekuwa kwenye nafasi za utendaji zaidi na
uwaziri. Dk Magufuli amekuwa mwanachama wa CCM na mbunge, nafasi ambayo
humuingiza kwenye kikao cha Halmashauri Kuu pekee.
Lakini Lowassa ameshika nafasi mbalimbali kwenye chama kuanzia katibu wa mkoa hadi mjumbe wa vyombo vya juu vya CCM.
Kauli za wachambuzi
Baadhi
ya wachambuzi na wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (Udsm)
wamesema kwa nyakati tofauti kwamba wagombea hao wanaonekana kuwa na
tofauti kubwa zinazoweza kufanikisha ushindi katika uchaguzi huo.
Mohammed
Bakari, ambaye ni mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, alisema wagombea hao wanafanana katika kigezo cha
utendaji kazi lakini kiuamuzi na uzoefu wanatofautiana.
“Dk
Magufuli ana uamuzi wa kukurupuka ila Lowassa ametulia,” alisema.
“Kuhusu uzoefu pia Lowassa ni mzoefu kiuongozi kuliko Dk Magufuli.”
Alisema
suala la uadilifu siyo rahisi kupata kiongozi mwadilifu kwa wagombea
hao na bila kuzitaja kashfa hizo, alisema wote wana kashfa. Aliongeza
kwamba, Lowassa ni mgombea anayeweza kuleta mabadiliko kwa Taifa hili,
lakini Dk Maghufuli hawezi kutokana na mfumo uliopo kwenye chama chake.
Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa wa Udsm, Dk Alexander Makulilo pia anaona sifa hizo zinazolingana.
Alisema
wagombea hao wanafanana kwa utendaji mzuri wa kazi na uamuzi wa papo
kwa hapo. Aidha, alisema Magufuli ni kiongozi anayeweza kuleta siasa
mpya zisizokuwa na makundi.
Alisema Lowassa ni mgombea
anayekabiliwa na changamoto ya Richmond iliyomfanya ajiuzulu uwaziri
mkuu, wakati Dk Magufuli hana kashfa kubwa iliyowahi kujadiliwa bungeni.
“Lakini
hali hiyo haiwezi kuwa changamoto kubwa kutokana na mwamko mkubwa wa
kundi linalohitaji mabadiliko ya uongozi serikalini. Uchaguzi huu
ninaufananisha na Zambia wakati chama cha UNIP kilipoondolewa madarakani
kwa kuwa makundi ya kijamii yalikuwa yameamua kiondoke madarakani,”
alisema.
Kuhusu mfumo kuibeba CCM, Dk Makulilo alisema
ni sehemu ya changamoto kubwa inayoweza kufanikisha ndoto za Lowassa
kuingia madarakani.
RSS Feed
Twitter
August 08, 2015
Unknown
0 comments:
Post a Comment