Saturday, July 11

Na Saleh Ally
WAKATI Alex Ferguson rasmi anatua Manchester United mwaka 1986 akitokea Aberdeen ya kwao Scotland, ndiyo Kocha Louis van Gaal alikuwa anaanza rasmi kazi ya ukocha.

Ferguson alianza kazi ya ukocha mwaka 1974, miaka 12 baadaye, van Gaal ndiyo akaanza kazi hiyo. Hivyo inakuwa ni rahisi kujua ubora wa makocha hawa kwa maana ya uzoefu.
Van Gaal, tayari ana umri wa miaka 19 katika kazi ya ukocha akifundisha nchi mbalimbali za Ulaya kama kwao Uholanzi, Hispania, Ujerumani na sasa England akiwa Kocha Mkuu wa Manchester United.
Amekuwa na mafanikio makubwa akiwa na Ajax, Barcelona na Bayern Munich na zote hakuondoka bila ya kuzipa makombe. Kazi yake inajulikana na si hadithi ngeni kuwa ni yenye mafanikio.
Wakati ametua Manchester United, ilionekana hakuwa na tofauti na David Moyes aliyeshindwa kuubeba ‘mzigo’ wa klabu hiyo baada ya kuachiwa na Ferguson. Sasa umetua mabegani kwa van Gaal na hakuna ubishi, utakwenda tu hata kwa tabutabu hivyohivyo.

Unaweza kushangazwa sana na namna ambavyo van Gaal amekuwa akiendelea kubaki katika benchi kama Man United imeishachapwa bao tatu au nne. Ataendelea kubaki hapo hata kama kuna presha kubwa. Kwa nini?
Huenda hii ni nafasi nzuri ya kujua upande wa pili wa shilingi wa kocha huyo ambaye ana nafasi kubwa ya kufikia kuwa mmoja wa makocha wenye uwezo huo.
Asili ya van Gaal ni kuwa mmoja wa makocha wenye akili sana, wanaojiamini kwa wanachokifanya na wagumu kutetereka kwa kuwa wanachoangalia cha kwanza ni mafanikio na si fedha au kupelekwapelekwa.
Nimeanza kusoma kitabu cha maisha ya van Gaal, ambacho baadaye kitaanza kuchapishwa kwenye magazeti ya Championi. Mambo kadhaa niliyoyaona, nikaona ni vema kuyaweka kwanza ili msomaji ajua kocha huyo Mholanzi ni mtu wa aina gani na amewahi kufanya nini katika soka nje ya benchi lake la ufundi.

Bluu:
Mwaka 1977, akiwa bado mchezaji kinda tu katika klabu ya SC Telstar alizua hoja iliyoonekana ya ajabu kabisa baada ya kuuliza uongozi wa klabu hiyo kama inawezekana kutumia uwanja wenye muonekano wa bluu ‘blue pitch’.
Klabu hiyo ikaona ni jambo jema kulifikisha kwa Shirikisho la Soka la Uholanzi (KNVB), nalo likapaisha jambo hilo hadi Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambao walilitosa na kusema si sahihi, itawachanganya watu na jamii ya soka kwa kuwa imezoea viwanja vya kijani ‘green pitch’, miaka nenda rudi.
Baadhi waliposikia hilo, wakaanza kulifanyia majaribio na sasa kuna viwanja vingi vya bluu katika viwanja vya mazoezi ya klabu kubwa ikiwa ni sehemu ya kubadilisha hali ya hewa na kuepusha kuwachosha wachezaji na kijani.

Michezo mingine ya soka kama futsal (ule wa ndani na uwanja mdogo unaoonekana kama wa mpira wa kikapu), wamekuwa wakitumia viwanja vya bluu na inaonekana, chanzo ni van Gaal, enzi hizooo.
Waamuzi zaidi:
Van Gaal anawekwa katika kundi la makocha ‘vipanga’, yaani wenye akili na mchango mkubwa katika mabadiliko ya soka likiwemo jambo la kuongezeka kwa waamuzi wawili wa pembeni katika mchezo wa soka.
Ingawa imekuwa haizingumzwi sana, van Gaal alikuwa wa kwanza kusema kuwa waamuzi watatu hawatoshi katika uamuzi wa soka uwanjani. Hivyo kushauri waongezwe wengine pembeni wawili au zaidi, lakini ilionekana ni sawa na kuvuruga utamaduni wa kisoka.
Pamoja na kukataa wazo lake, kadiri siku zinavyosonga mbele. Wazo alililotoa, limekuwa likiendelea kujadiliwa hadi mwisho Fifa na wadau wake lilipokata shauri kwamba yaanze majaribio, sasa waamuzi hao wameanza kutumika hadi katika mashindano makubwa kabisa.
Mtambo langoni:
Baada ya Thierry Henry kufunga bao la mkono na kuibeba Ufaransa kucheza Kombe la Dunia. Siku chache kabla ya tukio van Gaal alikuwa ameeleza umuhimu wa kuhakikisha kuna mitambo maalum kutambua usahihi wa bao.
Ingawa hakuwa akizungumzia mkono au mguu uliotumika, lakini alitaka uhakika wa kuvuka mstari au la. Jambo ambalo lilionekana ni tatizo na litaharibu ladha ya mpira.
Ingawa hakuwa wa kwanza kulianzisha, lakini ufafanuzi wake katika makongamano kadhaa ya Fifa na Uefa, yaliibua ushawishi upya hadi Fifa kutaka hilo lianze kufanyiwa kazi.

Hataki penalti:
Inawezekana wapo wanaofikiria kama van Gaal, lakini yeye ni mtu ambaye ana uwezo mkubwa wa kuthubutu kila inapofikia kuna jambo amelifanyia uchunguzi na kuliona ni sahihi.
Van Gaal si mtu wa kujisikilizia, akitaka jambo na akaliamini basi atalisema hata mbele ya watu ambao anajua watalikataa.
Miaka michache kabla ya kutua Manchester United, van Gaal aliibuka na jambo jipya, yeye akisema anapinga upigianaji penalti, anaona si sahihi na hauufanyi mchezo wa soka kuwa “pambano la wanaume wa shoka”.
Penalti ndani ya dakika 90, haoni tatizo, lakini ushindi wa mwisho kuamuliwa kwa ile mikwaju mitano au zaidi anaona ni kuufanya mchezo wa soka kuwa wa watu lainilaini.
Van Gaal, hajawahi kupinga kitu halafu asitoke na wazo lake ambalo anaamini litakuwa suluhisho.
Katika hili la penalti, amesema baada ya kuongezwa dakika 90 kwisha bila kupata mshindi. Basi zile dakika 30 zitakapoongezwa, kila baada ya dakika 5, kila timu itatoa mchezaji mmoja nje.
Maana yake, baada ya dakika 30, kila timu itakuwa imepoteza wachezaji sita, yaani 12 watakuwa wametoka uwanjani.
Hiyo itaufanya uwanja kuwa mkubwa sana kwa wale wanaobaki na inakuwa rahisi timu yoyote kufungwa kwa wakati wowote.
Mwisho akasisitiza, mpira una maajabu na kama ikitokea dakika 120 bado bao halijapatikana. Basi bao la dhahabu kwa muda kadhaa, ndiyo litumike kuamua. Hili bado Fifa, Uefa na wengine hawajalifanyia kazi.
Kasi:
Katika mkutano wa mmoja na Fifa, pia alipendekeza kuwa na mipira ya kisasa ambayo itakuwa ikipima kasi ya mchezo ili kujua miaka ya nyuma, kasi ilikuwa kiasi gani na kama inapanda, basi kwa kiasi gani ndani ya miaka mingapi.
Tayari kuna makampuni yanayofanya kazi hiyo, yameishaanza kulifanyia kazi hilo lakini baadhi ya makampuni ya vifaa vya michezo, yamekuwa yakiweka vifaa maalum kwenye viatu vya wachezaji, kupima kasi.
Van Gaal ana mengi kuonyesha ni kocha wa aina yake. Huenda utafurahia zaidi kufuatilia historia ya maisha yake katika magazeti ya Championi.

0 comments:

-