Wednesday, April 8


Madereva wa vyombo mbalimbali vya moto, wanakusudia kushiriki mgomo wa nchi nzima Ijumaa wiki hii, kuishinikiza serikali kuondoa kero mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa ajira za uhakika pamoja na agizo la kutaka kwenda kusoma.

Wakizungumza kupitia Katibu wa Muungano wa vyama vya madereva Bw. Rashid Saleh, Madereva hao wamesema kuwa suala la kurudia kusoma kila wanapohuisha leseni zao ni aina nyingine ya unyanyasaji kwa maelfu ya madereva nchini, ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa hawana mfumo mzuri wa ajira licha ya kutupiwa lawama kibao kuwa wao ndio chanzo cha ongezeko la ajali.
 
Katibu huyo wa Muungano wa Vyama vya Madereva ameitaja kero nyingine kuwa ni hatua ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji NIT kutamka hadharani kuwa vyeti walivyonavyo madereva hao sio halali na kwamba Ijumaa wiki hii wanakusudia kukutana na Waziri wa Kazi na Ajira kwa ajili ya kuzungumzia kero hizo kwa lengo la kuepusha kutokea kwa mgomo huo.
 
Saleh ametaja madereva wanaounda muungano huo kuwa ni wa bodaboda, bajaj, teksi, daladala, mabasi ya safari fupi, mabasi ya safari ndefu na za nje ya nchi pamoja na madereva wa magari yote ya mizigo.
 
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa muungano wa madereva, mkutano wa Ijumaa ndio utakaoamua iwapo madereva hao wagome au waendelee na kazi kwani wamechoka kudharauliwa hata kwa mambo ya msingi yanayogusa maisha yao.
 
Baadhi ya dharau alizozitaja ni pamoja na wamiliki wa mabasi (yaani waajiri wao) kuwaita wao ni wahuni ilhali ni watu wazima, wenye familia, wanaofanya kazi halali na wanaohitaji kuheshimiwa.


0 comments:

-