Wednesday, April 1

Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
UPO katika mwaka wa Uchaguzi Mkuu ambao utafanyika Oktoba mwaka huu, utakaoipatia nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania rais wake wa tano, ambaye kwa mujibu wa katiba yetu, atakaa madarakani kwa muda usiozidi miaka kumi katika vipindi vya miaka mitano mitano.
Tatizo hasa lipo CCM ambako dazani ya wanachama wake, kila mmoja anaamini anao uwezo wa kukalia kiti kile cha enzi kwa sababu hadi hivi sasa, wanaotajwa kuwania nafasi hiyo idadi yao inatisha.
Kwa vile suala la maadili linaonekana kuwekwa kando, kinachoshuhudiwa hivi sasa ni mbinu binafsi za mtu anayewania nafasi hiyo katika kujipanga na kujipa uhalali wa kwa nini yeye anafaa kukabidhiwa kiti kinachoachwa wazi na Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Wiki chache zilizopita, kupitia vyombo vya habari, tuliona jinsi makundi mbalimbali ya kijamii, yalivyokwenda nyumbani kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kule Monduli na kumshawishi kuchukua fomu za kuwania urais wakati ukifika. Siku chache baadaye, wanaotajwa kama mashehe kutoka Bagamoyo, nao walimfuata Dodoma na kutoa ombi kama hilo.
Wakati watu wakiwa bado wanatafakari makundi haya ya Watanzania wenzetu waliopewa maono ya kumtambua Lowassa kuwa ndiye mtu muafaka, wakajitokeza tena wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambao nao walikwenda kwa mbunge huyo wa Monduli na kutoa wito uleule wa kumtaka kuchukua fomu kuwania kiti hicho. Makundi yote hayo, yalitoa fedha za kuchangia gharama za fomu ya urais kupitia CCM.
Lakini katika hali ya kushtua sana, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba, aliibuka na kuyaponda makundi hayo, akidai ni mchezo wa kuigiza unaoratibiwa na kambi ya mwanasiasa huyo, kwani wote wanaoshiriki kwenda kwake hulipwa posho.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Akaenda mbali zaidi na kusema nafasi kubwa kama ya urais, haiwezi kuchukuliwa na watu wanaofanya maigizo, kwa sababu hata wakipewa, wataendeleza maigizo katika kushughulikia masuala muhimu ya wananchi.
Sipendi kuzungumzia sana kuhusu maudhui ya maneno ya Makamba, lakini ninataka kutembea katika matamshi yake kuwa wakati yeye anapinga maigizo yanayofanywa na Team Lowassa, viongozi wengi wateule wa Rais Kikwete, akiwemo yeye mwenyewe, wanatufanyia maigizo mengi tu sisi wananchi.
Wanakaa na kukubaliana kuwa Kampuni ya Bia (TBL) ndiyo iendeshe bajeti ya serikali kwa kuilipisha kodi kubwa, ili kukomoa walevi, wakati tunajua kabisa, kampuni za simu zilizo chini ya wizara ya Makamba, zinaingiza fedha zaidi ya mara sita au saba ya TBL, lakini zote hazipo katika Top Ten ya kampuni zinazolipa kodi kubwa serikalini. Vigogo wetu serikalini wana hisa katika kampuni hizi za simu!
Vigogo wa serikali wanaigiza kulia katika majukwaa ya kisiasa wakihutubia wananchi, lakini hao hao ndiyo wanaosaini mikataba mibovu isiyo na tija kwa taifa, lakini hawajali kwa sababu wao wana asilimia kumi yao. Ndiyo maana wao wana majumba ya kifahari, sisi tuna vibanda vya makuti na hawajali.
Mtumishi wa umma anayeita shilingi bilioni moja kuwa vijisenti, unategemea anaishije kama siyo kwa maigizo? Kama serikali yetu ingekuwa haiigizi, ingemuita na kutaka maelezo juu ya kauli hiyo.
Wao wanatibiwa Ulaya, sisi tunaambiwa hospitali hazina dawa, kama siyo Bongo Movie ya mawaziri na serikali yote ni nini?Ni makosa kuilaumu kambi ya Lowassa kama kweli inafanya maigizo, kwa sababu ndiyo aina ya maisha ambayo nchi yetu imeamua kuyaishi. Kila sehemu ni maigizo na hata mambo makubwa ya nchi yanaendeshwa kisanii. Labda kama January utaniambia vinginevyo!

0 comments:

-