Sunday, February 8

ENDAPO ulinzi binafsi na wa kazini hautaimarishwa kwa majaji, uwezekano ni mkubwa wa watu wabaya kuwavamia ofisini na kuwapiga risasi kwa sababu ya hukumu zao za kunyonga au kufunga watu jela maisha, Risasi Jumamosi limebaini.
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam. 
Hilo limekuja kufuatia chanzo kimoja toka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kupiga simu kwenye Ofisi za Magazeti Pendwa ya Global Publishers na kusema anasikitika kuona majaji, licha ya kutoa hukumu nzito zinazowaumiza watu lakini  hawana ulinzi wa maisha yao.

Kamanda wa Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ wa Global akiwa mbele ya mlango wa ofisi ya Jaji wa Mahakama Kuu na bastola kiunoni.
MSIKIE HUYU
“Jamani naamini hapo ndo Global?”
Risasi Jumamosi: “Ni sahihi kabisa, tunaweza kukusaidia?”
Chanzo: “Jamani ni hivi, mnawajua majaji wetu hapa mahakama kuu. Wanahukumu watu kunyongwa, wanafunga watu maisha, lakini pamoja na mambo yote hayo makubwa hawana ulinzi.”

Kamanda wa Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’akiondoka eneo la tukio.
KUMFIKIA JAJI RAHISI TU
“Utakuta jaji yupo ndani ya ofisi yake lakini hana ulinzi wowote. Mtu mbaya anaweza kuingia kuanzia chini mpaka ofisini akamfanya lolote.
“Nadhani serikali ingetafuta njia ya kuwalinda hawa watu. Kazi yao ni ya hatari sana na inagusa jamii moja kwa moja.”

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe Omar Othman Makungu na majaji wengine.
WASIWASI ULIOPO
“Unajua, kumfunga mtu maisha jela au kumhukumu kunyongwa ni hatari sana. Utakuta mtu ana familia inamtegemea, sasa unadhani familia anayoiacha itafurahi kumwona jaji aliyeharibu maisha yao? Wasiwasi wangu ipo siku tutasikia jambo kubwa sana.”
Risasi Jumamosi: “Tumekusikia, hilo tutalifanyia kazi ndani ya siku moja tu. Tutaona kama madai yako ni ya kweli au la!”
Chanzo: “Nyiye chunguzeni tu mtajua ni kweli.”

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania Mhe. Shaban Ally Lila (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Majaji wa Mahaka Kuu Tanzania.
OFM YAINGIA KAZINI
Baada ya kupewa taarifa hizo, Makamanda wa Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ wa Global walijipanga kwenda mahakama kuu wakiwa na bastola mfukoni ili kuona kama kweli raia yeyote anaweza kupita kuanzia lango kuu hadi kupanda ghorofa ya kwanza ambako majaji wana ofisi bila kukutana na ulinzi wa upekuzi!

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimwapisha Mhe Winfrida Beatrice Korosss kuwa Jaji wa mahakama Kuu ya Tanzania katika sherehe zilizofanyika Ikulu jijini Dar es salaam leo Aqgosti 15, 2014
Kamanda mkuu wa OFM akiwa na wasaidizi wake, wiki iliyopita walifika mahakamani hapo akiwa na bastola hiyo na kuzama ndani bila kukutana na kizuizi chochote kinachoweza kubaini (detector) kuwa mtu anayeingia ana silaha.
OFM MLANGONI KWA JAJI
Kama vile haitoshi, kamanda wa OFM  bado akiwa na bastola kwenye mfuko wa suruali alipandisha ngazi hadi ghorofa ya kwanza na kutembea kwa kujidai kwenye korido yenye milango ya vyumba vya majaji.
Kuna wakati, kamanda huyo alisimama kwa muda kwenye mlango wa jaji mmoja (jina tunalo) na kuchomoa bastola kisha akairudisha tena mfukoni, hakuna mlinzi aliyejitokeza wala mtu wa kuuliza kamanda alikuwa akifanya nini katika eneo hilo! Ni hatari sana!

DAKIKA KUMI
Mpaka dakika kumi zinakatika, kamanda wa OFM huku akipigwa picha mbalimbali na fotografa wake, hakuna mtu aliyeonekana kuhusika na masuala ya ulinzi.

TAFSIRI RAHISI
Kwa maana hiyo, kama kamanda angekuwa ndiye adui wa mmoja wa majaji, angeweza kusukuma mlango na kuzama ndani kisha kufanya lolote akiwa na silaha yake hiyo. Majaji wafikiriwe upya!

MSEMAJI WA MAHAKAMA AONGEA
Baada ya kamanda wa OFM kuondoka eneo la mahakama, siku iliyofuata, Risasi Jumamosi, lilimtafuta Kaimu Msemaji wa Mahakama Kuu Tanzania, Mary Gwela ambapo alisema:
“Kwanza ni kweli majaji wanastahili kuwa na ulinzi wa kutoka ofisini hadi nyumbani na nyumbani hadi ofisini.

“Lakini hali hii imetokana na ukweli kwamba, askari ni wachache. Hata Kova (Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam) alisema askari ni wachache.
“Hata hivyo, majaji wanapokwenda kikazi mikoani ndiyo wanaondoka na ulinzi wa askari. Majaji ni uteuzi wa rais, kwa hiyo kisheria walitakiwa wawe na ulinzi.
“Lakini jambo la kushangaza ni kwamba, majaji waliopo mikoani wote wana ulinzi kwa hiyo wako salama.”

Baada ya maelezo hayo, Risasi Jumamosi lilimtafuta Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-rose Mtengeti Migiro ambapo hakuwa hewani.
Kwa upande wake, Kamanda Kova ambaye ilidaiwa aliwahi kutamka kuwa askari ni wachache, hakuwa hewani ambapo Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu simu yake iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

MEZANI KWA MHARIRI
Ni vizuri serikali ikaliangalia hilo ili kuweza kuwapa ulinzi majaji wetu kwani kazi wanayoifanya ni ya hatari. Kumfunga maisha au kumhukumu kunyongwa mtu aliyekutwa na hatia si jambo dogo katika jamii.


0 comments:

-