
September 15, 2014

Unknown

KATIKA hali isiyo ya
kawaida, askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanadaiwa
kuwafanyia ukatili mkubwa vijana 11, wakazi wa eneo la Keko Magulumbasi
B, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam kwa kuwapiga na kuwalazimisha wanywe
maji machafu yenye kinyesi.
Tukio hilo ambalo
limefananishwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, linadaiwa
kutokea Septemba 12 mwaka huu, saa 11 jioni, katika eneo la Keko
Magulumbasi B.
Inadaiwa kuwa,
wanajeshi hao ambao walikuwa saba wakiwa na sare za jeshi hilo, walifika
Keko Magulumbasi B wakiwa na kijana mmoja mwenye asili ya Kiarabu na
kuwavamia vijana waliokuwa wakila chakula kwenye kibanda cha chipsi.
Mashuhuda wa tukio hilo
walidai kuwa, wanajeshi hao waliwakamata vijana hao na kudai wanahusika
kupora simu ya kijana mwenye asili ya Kiarabu aina ya Tecno yenye
thamani ya sh. 25,000.
Pamoja na vijana hao
kukataa kuhusika na tukio hilo, waliwekwa chini ya ulinzi, kufungwa
mikono kwa kamba, kulazwa kifudifudi na kuanza kupigwa mikanda ya jeshi.
Mashuhuda hao
waliongeza kuwa, vijana hao walichukuliwa hadi kwenye bwawa la maji
machafu yaliyochanganyika na kinyesi cha binadamu wakazamishwa vichwa
vyao ndani ya bwawa hilo la kulazimishwa kunywa maji hayo.
Waliongeza kuwa, vijana
hao wakiwa wameloana kwa maji machafu walichukuliwa na wanajeshi hao
hadi Kituo Kidogo cha Polisi Keko na kuswekwa rumande na mmoja wao
aliachiwa baada ya dakika 10.
Baadhi ya wakazi wa
eneo hilo, walilazimika kuvamia kituo hicho na kufanya vurugu
wakiwarushia mawe askari wa kituo hicho kwa lengo la kuwatoa vijana hao
kwa nguvu wakidai wameonewa.
Hata hivyo, wananchi
hao walitawanywa kwa risasi za moto zilizopigwa hewani na askari wa
Kituo Kikuu cha Polisi Chang'ombe walioitwa kuongeza nguvu kituoni hapo.
Bw. Omary Abdu (30)
ambaye ni mkazi wa eneo hilo ambaye alikuwepo kwenye eneo la tukio,
alidai kutofurahishwa na kitendo kilichofanywa na wanajeshi hata kama
vijana hao wameiba kwani walipaswa kufikishwa katika mamlaka husika ili
hatua zichukuliwe.
"Walichokifanya wale
wanajeshi ni ukiukwaji mkubwa wa sheria na haki za binadamu...naamini
wanafahamika, itakuwa vizuri kama watachukuliwa hatua za kisheria,"
alisema.
Mkazi mwingine wa eneo
hilo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, aliwashutumu wakazi
wenzake kwa kitendo cha kuvamia Kituo cha Polisi na kufanya fujo kwa
kuwarushia mawe polisi.
Katika hatua nyingine,
mkazi huyo alimtuhumu Mwenyekiti wa Mtaa wa Magulumbasi B, Bw. Mohamed
Fundi ambaye alidai kupitia kikao chake na wananchi Agosti 29 mwaka huu,
alihamasisha wagome kukamatwa na polisi.
Alidai kauli kama hiyo inaweza kuleta vurugu na uvunjifu wa amani hivyo zinatakiwa kukemewa na kila mkazi wa eneo hilo.
Majira lilimtafuta Bw.
Fundi ambaye alikiri kufanya kikao na wananchi kwa tarehe hiyo ambacho
kilikuwa na lengo la kuhamasisha maendeleo na kuwafahamisha wananchi
haki zao si kuhamasisha vurugu au kuzuia wasikamatwe na polisi kama
inavyoelezwa.
Alisema miongoni mwa
haki hizo ni namna polisi anavyotakiwa kumkamata raia na asikamatwe
usiku bila kuwepo kwa kiongozi wa eneo lake.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Kipolisi Temeke, Kihenya Kihenya amethibitisha kutokea kwa tukio hilo
akidai taarifa alizonazo ni kwamba, vijana waliokamatwa wanajihusisha
na wizi wa mifukoni.
Alisema wakiwa Kituo
Kidogo cha Polisi Keko, wananchi walikivamia na kufanya vurugu hadi
walipotawanywa na askari kutoka Kituo Kikuu cha Polisi Chang'ombe kwa
kupiga risasi hewani.
"Taarifa zinazosema
vijana hao waliteswa na kunyweshwa maji machafu na wanajeshi bado
sijazipata ila hawa vijana wanashikiliwa Kituo cha Polisi Chang'ombe
wakisubiri kufikishwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika," alisema.
Inaelezwa kuwa, wiki
moja iliyopita kijana huyo mwenye asili ya Kiarabu mkazi wa Keko Toroli,
alivamiwa na vijana eneo la Keko Magulumbasi B, ambao walimpora simu ya
mkononi tukio ambalo liliripotiwa kwenye Kituo Kidogo cha Polisi Keko.
0 comments:
Post a Comment