Sunday, June 22

417570_heroa 
Maandalizi ya msimu wa ligi kuu ya Tanzania yameanza kupamba moto huku vilabu vikijaribu kujiimarisha tayari kwa mapambano, kwa upande wa klabu ya Yanga wameanza kwa kuimarisha benchi la ufundi kwa kumuajiri kocha Marcio Maximo.
Kocha huyo mbrazil anayeheshimika zaidi nchini, Marcio Maximo atatua Jangwani ndani ya siku nne kuanzia leo Jumamosi. Bosi huyo ambaye anasifika zaidi kwa msisitizo wake katika nidhamu za wachezaji atatua Jumanne ikiwa ni mapema kabla ya uchaguzi wa Simba utakaofanyika Juni 29 Jijini Dar es Salaam. Mwanaspoti linajua kwamba Maximo yuko jijini Brasilia akifanya kazi ya uchambuzi wa mechi za Kombe la Dunia kwenye televisheni ya Taifa ya Mexico na mkataba wake unamalizika Jumatatu.
Yanga imethibitisha kwamba Maximo ameshaanza maandalizi ya safari hiyo tangu juzi ambapo katika hilo pia amewajulisha baadhi ya maofisa wa Ubalozi wa nchi hiyo nchini kuwa atakuwa Tanzania mapema wiki hii kumalizia maongezi yake na mabosi wa Yanga.
Yanga wamemleta Maximo mapema kufanya maandalizi ya uhakika katika kikosi cha timu hiyo ikiwa ni kuwawahi wapinzani wao wa jadi Simba ambao bado wapo katika mchakato wa uchaguzi.
“Ilikuwa kuna baadhi ya viongozi waende Brazil kumalizia mazungumzo na kusainishana mkataba  lakini hilo limebadilishwa. Maximo ndiyo atakuja Dar es Salaam kuepuka gharama,”alisisitiza mmoja wa viongozi wa Yanga.
Source: Mwanaspoti

0 comments:

-