Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile (kulia) akibadilishana
hati ya mkataba wa msaada wa sh. Bilioni 134 waliosaini kwa niaba ya
Serikali ya Tanzania leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Balozi EU
nchini Filberto Sebregond.
(Picha na Wizara ya Fedha)
Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile (kulia) akisaini mkataba
wa msaada wa sh. Bilioni 134 kwa niaba ya Serikali ya Tanzania leo
jijini Dar es salaam. Kushoto ni Balozi EU nchini Filberto Sebregond.
………………………………………………………
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
SERIKALI
ya Tanzania imetiliana saini mkataba wa msaada wa zaidi ya Shilingi
Bilioni 134 sawa na Euro milioni 59.5 kutoka Umoja wa Ulaya (EU)
kusaidia sekta ya kilimo na usafirishaji nchini.
Mkataba
huo ulisainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile
kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa EU nchini Filberto
Sebregond leo jijini Dar es salaam.
Akizungumza
baada ya kutia saini mkataba huo, Dkt. Likwelile alisema kuwa sehemu ya
msaada huo ambao ni Shilingi Bilioni 82.4 ambazo ni sawa na Euro
milioni 36.5 utatumika kuendeleza sekta ya kilimo na kukuza uchumi
nchini kwa kupitia kituo maalum cha uendelezaji kilimo ukanda wa Kusini
Tanzania (SAGCOT) na kuboresha miundombinu ya barabara za ukanda huo.
Vilevile
Dkt. Likwelile alisema kuwa sehemu iliyobaki ya msaada huo ambao ni
Shilingi Bilioni 51.9 ambazo ni sawa na Euro milioni 23 itatumika
kuimarisha biashara na ushirikiano katika jumuiya kwa kuanzisha kituo
cha pamoja cha ukaguzi mipakani (OSIS).
“Vituo
hivyo vya ukaguzi mipakani vitakuwa na manufaa si kwa Tanzania tu, bali
hata katika nchi mbalimbali zinazopakana na Tanzania” alisema Dkt.
Lkwelile.
Alifafanua
kuwa msaada uliosainiwa unamanufaa kwa wananchi kwa kuboresha
miundombinu vijijini na kusambaza umeme vitu ambavyo vitasaidia kukuza
uchumi na kupunguza umaskini nchini.
Naye
Balozi wa EU nchini Filberto Sebregond alisema kuwa anaamini msaada huo
utasaidia juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuongeza nafasi za
ajira, kupungua kwa bei za bidhaa mbalimbali na kuendelea kukuza uchumi
nchini.
Balozi
huyo alisema kuwa EU inaamini kuwa ushirikiano wake na Tanzania
utaendelea kuimarika kwa kuhimiza maendeleo kwa pande zote mbili na
amani ya watu wake.
Hafla
hiyo ya kusaini mkataba ilihudhuriwa na wawakilishi kutoka Wizara ya
Fedha, Nishati na Madini, Uchukuzi na Ujenzi, EAC, DFID, SAGCOT, wajumbe
kutoka EU, Shirika la maendeleo ya Ufundi kutoka Ubelgiji na washirika
wa maendeleo.
0 comments:
Post a Comment