Mahabusu
wawili kati ya sita wanaotuhumiwa kwa kesi za mauaji wameleta kizaazaa
baada ya kujaribu kutoroka na kukimbilia kwenye mlingoti wa Bendera ya
Taifa na kuing’ang’ania kisha kuvua nguo na mmoja wao kubaki mtupu.
Tukio hilo limetokea May 7 2014 saa nne asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Nyamagana Mwanza walipofikishwa
kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi zao lakini ghafla walipofika kwenye
viwanja vya mahakama hiyo walitimua mbio kuelekea kwenye mlingoti wa
Bendera hiyo
ya Taifa na kuvua nguo kisha kuanza kupiga kelele kwa kupaza sauti kudai haki itendeke.
Ni
Thobiasi Warioba (35) alieamua kuvua nguo zote na kubaki mtupu eneo la
mlingoti wa bendera ya taifa, ambaye anakabiliwa na kesi ya mauaji Na.
32/2012.
Watuhumiwa
wengine waliojaribu kutoroka ni Hamis Ramadani (30), Anthony Petro
(35), Marwa Mwita (38), na Chacha Wangwe (35), na mwingine ambaye
hakufahamika majina yake mara moja, wote wanakabiliwa na kesi ya Jinai
Na. 215/2013 na walikamatwa tangu mwaka 2011.
Baada
ya kudhibitiwa na askari polisi walisikika wakisema: “haiwezekani tangu
mwaka 2011 tulipokamatwa hadi sasa kesi zetu hazijasikilizwa, wengine
tumebambikiziwa kesi tunaomba haki zetu, polisi mnatuonea, vyombo vya habari tunaomba mtusaidie tumekaa
muda mrefu bila kusikilizwa na hatujui hatma yetu tangu 2011
tulipokamatwa, tumechoka kukaa mahabusu tunaomba kesi zetu zisikilizwe”.
Baada
ya malalamiko yao askari mmoja aitwae Inspekta Henry akiwa na wenzake
sita waliokuwa wakiwadhibiti wasikimbie aliwahoji kuhusiana na madai yao
huku askari hao wakiwataka kuondoka katika mlingoti huo na kumtaka
Warioba avae nguo ili waweze kuingia Mahakamani.
Mmoja
wa maofisa waandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza ambae
alikataa kutajwa jina lake, alidai ushahidi wa kesi za watuhumiwa hao
bado haujakamilika na kwamba kesi zao haziwezi kusikilizwa na mahakama
ya wilaya kwani haina uwezo na badala yake zitatajwa tu kisha
kuhamishiwa Mahakama Kuu.
0 comments:
Post a Comment