Thursday, May 22

Mwimbaji mahiri nchini aliyefariki dunia wiki iliyopita huko Thailand, Amina Ngaluma.

 MWILI wa mwimbaji mahiri nchini aliyefariki dunia wiki iliyopita nchini Thailand, Amina Ngaluma ‘Japanese’ unatarajiwa kuwasili Dar es Salaam Ijumaa wiki hii.
Kwa mujibu wa mume wa marehemu, Rashid Sumuni tayari taratibu muhimu kuhusiana na kuuleta mwili huo nyumbani zimefanyika na wana amini mambo yataenda kama wanavyotarajia.
“Naomba niwajulishe kuwa mwili wa mke wangu utaondoka Thailand Alhamisi wiki hii kwa ndege ya KLM na utawasili Dar es Salaam siku inayofuata saa tatu usiku.
“Tunaamini kama mambo yataenda kama tulivyopanga baada ya mwili kuwasili basi Jumamosi tutamhifadhi mwenzetu. Msiba upo kwa wazazi wa marehemu Kitunda, Machimbo, Dar es Salaam ambako ndiko maziko yatafanyika.
“Kimsingi imekuwa ngumu kusema tutazika lini, kwa sababu bado mwili haujaletwa, lakini tayari familia kwa kushirikiana na sehemu alikokuwa anafanya kazi na Watanzania wengine waishio kule tumeshamaliza taratibu zote zilizokuwa zikihitajika ili kuuleta mwili nchini,” alisema Sumuni kwa masikitiko.
Pia alivishukuru vyombo vya habari kwa kuwa karibu na familia yao wakati wa kipindi hiki kigumu, lakini akiomba wanapotaka kutoa habari kuhusiana na msiba huo wawasiliane na wahusika wa familia ili kupata taarifa sahihi zaidi.
Ngaluma aliyepata kung’ara na bendi mbalimbali nchini, alifariki dunia Alhamisi iliyopita kwa shinikizo la damu akiwa Thailand alikokuwa akifanya shughuli za muziki katika bendi ya Jambo Survivor.
Wakati wa uhai wake alitamba na bendi mbalimbali zikiwemo African Revolution ‘Tamtam’,  Double M Sound ‘Mshikemshike’ na TOT Plus zote za Dar es Salaam.
Pia alipigia makundi ya Arusha Sangoma, Sayari Band na Less Mwenge yote ya Arusha na Mangelepa na Sky Sound za Kenya. Pia amepata kufanya shughuli za muziki kwa miezi sita nchini Uganda.
Baadhi ya nyimbo alizotunga wakati wa uhai wake ni Manyanyaso Kazini na Mapendo alizotunga akiwa Tamtam, wakati Double M Sound alitunga nyimbo za Wajane na Ukewenza.
Pia alitoa albamu yake binafsi iitwayo Jitulize yenye nyimbo kama Vidonge, Pete ya Uchumba, Good Night, Uombalo Hutopata, Jitulize na Mzigo wa Moto.
Baadhi ya nyimbo alizopata kuimba na kumpatia umaarufu mkubwa ni Mgumba, Maisha Kitendawili,  Ndugu Lawama, Zawadi ya Watanzania, Ugumu wa Maisha na Call Box zote zikitungwa na Muumin Mwinjuma ‘Kocha wa Dunia’. Mungu amuweke mahali pema peponi. Amin

0 comments:

-