Zimebaki siku chache tu kabla kipyenga cha kuashiria kuanza rasmi kwa
michuano ya Kombe La Dunia la Soka kwa mwaka 2014 zitakazofanyikia
nchini Brazil hakijapulizwa. Jumla ya timu kutoka mataifa 32
zinatarajiwa kushuka dimbani kuwania kombe hilo ambalo mshindi
hutambulika kama mwamba wa soka duniani.
Kombe la Dunia huwa ni mkusanyiko wa mataifa na wachezaji
wanaoaminika kuwa bora kabisa duniani. Mechi ya kwanza itakayopigwa Juni
12 itakuwa kati ya wenyeji Brazil watakaoanza kwa kumenyana na Croatia
katika jiji la Sao Paulo.
Kabla ya ufunguzi na kabla bendera hazijapandishwa katika milingoni
na magari na kabla fulana au jezi za timu hazijavaliwa mitaani na katika
viunga vya sehemu mbalimbali duniani,haya hapa ni mambo 95 zikiwemo
takwimu, historia kumbukumbu na mengineyo ambayo yanahusiana na Fainali
za Kombe La Dunia ambayo tungependa uyajue [au ujikumbushe] kuhusu
michuano ya Kombe La Dunia.
- Mechi za Kombe la Dunia mwaka 2014 zitafanyikia katika miji au majiji 12 tofauti nchini Brazil
- Kikaragosi au mascot wa Kombe la Dunia mwaka 2014 anaitwa Fuleco.
- Kombe la Dunia mwaka huu 2014 linamaanisha kwamba hii ni mara ya 5 kwa fainali hizo kufanyikia katika bara la Amerika ya Kusini. Mara ya mwisho lilifanyikia barani humo nchini Argentina mwaka 1978.
- Mwaka 1998 Ufaransa walikuwa wenyeji wa fainali hizo kwa mara ya pili.Mara ya kwanza walikuwa wenyeji mwaka 1938.
- Pele, Mbrazil ambaye anaaminika kuwa Mfalme wa Soka Duniani, ana magoli 12 na hivyo ni mfungaji bora wa 5 kwa ujumla miongoni mwa wafungaji bora au wenye magoli mengi katika fainali za Kombe la Dunia.
- Urusi watakuwa wenyeji wa Kombe La Dunia mwaka 2018 wakati Qatar watakuwa wenyeji mwaka 2022.
- Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002 ndizo fainali pekee mpaka leo ambapo wenyeji wake zilikuwa ni nchi mbili. Korea ya Kusini na Japan.
- Jiji la Rio de Janeiro ambalo litakuwa mwenyeji wa mchezo wa fainali wa Kombe la Dunia mwaka huu lina jumla ya wakazi Millioni 6.3
- Uwanja wa Estadio do Maracana utakaoshuhudia fainali unatumiwa na clubs za Flamengo na Fluminese za nchini humo.
- Kuanzia fainali za mwaka 1998 FIFA waliamua Fainali za Kombe La Dunia zishirikishe timu 32 badala ya 24 ilivyokuwa kuanzia 1982 na 16 kabla ya hapo.
- Argentina walikuwa wenyeji wa Fainali za Mwaka 1978 na walichukua Ubingwa mwaka huo.
- Mfungaji bora wa fainali za mwaka 1950 alikuwa ni Ademir wa Brazil kwa jumla ya magoli 8.
- Mchezaji wa Uingereza,Geoff Hurst ndiye mchezaji pekee kuwahi kufunga hat trick [goli tatu peke yake] katika fainali ya Kombe la Dunia.Alifanya hivyo katika mchezo wa fainali mwaka 1966 dhidi ya Ujerumani Magharibi. Uingereza walikuwa wenyeji wa michuano ya mwaka huo.
- Luis Monti ndiye mchezaji pekee kuwahi kushiriki mashindano ya Kombe La Dunia kama mchezaji wa mataifa mawili tofauti. Argentina (1930) na Italy (1934)
- Uholanzi(Netherlands) inaaminika kuwa mojawapo ya timu bora kabisa ambazo kwa bahati mbaya hazijawahi kushinda Kombe la Dunia. Wamepoteza katika fainali tatu (1974,1978 na 2010)
- Takribani watu Bilioni 3.2 walitizama mchezo wa fainali wa Kombe la Dunia mwaka 2010 uliofanyikia nchini Afrika Kusini. Hiyo ni karibu nusu ya watu duniani.
- Afrika Kusini ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa wenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2010.
- Mipira rasmi itakayotumika kwa fainali za mwaka huu 2014 imetengenezwa na kampuni ya Adidas na imepewa jina Brazuca
- Uwanja wa Maracana ambapo fainali za mwaka huu zitafanyikia una uwezo wa kuingiza watu 79,000. Ule wa kwanza uliojengwa kwa ajili ya fainali hizo mwaka 1950 ulikuwa na uwezo wa kuingiza watu 200,000.
- Katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994, Roger Milla kutoka Cameroon aliweka historia ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa kupita wote kuwahi kufunga goli katika mchezo wa fainali hizo. Cameroon walichapwa 6-1 na Urusi.
- Wapiga upatu[watabiri] wengi wanaipa Brazil nafasi ya kuchukua Kombe la Dunia mwaka huu ikifuatiwa na Ujerumani,Argentina na Spain.
- Kombe la Dunia la mwaka huu litaonyeshwa “Live” katika jumla ya nchi 200 duniani.
- India iliwahi kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 1950 lakini walijitoa kutokana na sababu za kifedha na pia kwa sababu wachezaji wake wengi walipenda kucheza soka miguu peku kitu ambacho FIFA hawakiafiki.
- Diego Maradona wa Argentina alifunga goli la mkono dhidi ya Uingereza wakati wa fainali za mwaka 1986. Baadae aliuita au kulipa goli hilo jina la “Mkono wa Mungu”.
- Cameroon ilikuwa nchini ya kwanza ya Afrika kufikia robo fainali ya michuano ya Kombe La Dunia wakati wa fainali za mwaka 1990.
- Mwaka huu itakuwa ni mara ya pili kwa Brazil kuwa wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia. Mara ya kwanza ilikuwa 1950.
- Bora Milutinovic raia wa Serbia ana rekodi ya kuwa Kocha wa nchi nyingi zaidi wakati wa fainali za Kombe la Dunia. Amekuwa kocha za Mexico (1986),Costa Rica (1990),USA (1994), Nigeria (1998) na China (2002). Kocha mwingine mwenye rekodi inayofanana na ya Bora ni Carlos Alberto Parreira raia wa Brazil.
- Mechi zote za fainali za kwanza za Kombe la Dunia mwaka 1930 zilizofanyikia nchini Uruguay zilifanyika katika jiji moja tu la Montevideo
- Pele wa Brazil anashikilia rekodi ya kushinda Kombe la Dunia mara tatu 1958,1962 na 1970.
- Oleg Salenko wa Urusi anashikilia rekodi ya magoli mengi zaidi katika mechi moja. Alipachika jumla ya magoli 5 katika ushindi wa magoli 6-1 dhidi ya Cameron mwaka 1994. Fainali za mwaka huo zilifanyikia nchini Marekani.
- Goli la Hakan Sukur wa Uturuki linashikilia rekodi ya goli lililowahi kufungwa mapema zaidi katika fainali za Kombe la Dunia. Alilifunga katika sekunde ya 11 ya mchezo dhidi ya Korea Kusini wakati wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002.
- Zilikuwa zimebaki dakika 10 tu mchezo umalizike kabla Zinedine Zidane wa Ufaransa hajampa “ndoo” Marco Materazzi wa Italy wakati wa mchezo wa fainali mwaka 2006.
- Ronaldo wa Brazil anashikilia rekodi ya kupachika mabao mengi zaidi katika fainali za Kombe la Dunia. Ana jumla ya magoli 15 kutoka katika fainali za mwaka 1998,2002 na 2006.
- Jumla ya timu 13 tu zilishiriki michuano ya fainali za kwanza kabisa za Kombe la Dunia zilizofanyikia nchini Uruguay mwaka 1930.
- Refa kutoka Urusi, Valentin Ivanov alitoa jumla ya kadi 16 za njano katika mchezo baina ya Ureno na Uholanzi mwaka 2006 fainali zilizofanyikia nchini Ujerumani.
- Katika umri wa miaka 17, Pele wa Brazil aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kufunga goli katika Kombe la Dunia. Ilikuwa mwaka 1958 nchini Sweden.
- Hii ni mara ya 20 kwa fainali za Kombe la Dunia kufanyika. Wenyeji ni Brazil.
- Katika fainali za mwaka 1966 Korea ya Kaskazini ilijipatia jumla ya magoli 3 ndani ya dakika 22 tu za mwanzo katika mchezo dhidi ya Ureno. Hata hivyo walipoteza mchezo huo kwa jumla ya goli 5-3.
- Akiwa na umri wa miaka 23, Alcides Ghiggia wa Uruguay alifunga goli lililoipa Uruguay ubingwa wa dunia katika mchezo wa fainali dhidi ya Brazil mwaka 1950 uliofanyikia katika Uwanja maarufu wa Maracana. Miaka mingi baadae Ghiggia anasema, “Kuna watu watatu tu ambao wamewahi kuwanyamazisha mashabiki wa Brazil wapatao 200,000 katika Uwanja wa Maracana; Frank Sinatra,Papa John Paul wa II na mimi”
- Katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006, Argentina walipigiana pasi 24 kabla ya kiungo wao Esteban Cambiasso kufunga dhidi ya Serbia na Montenegro. Yes pasi 24!
- Katika fainali za mwaka 1954 nchini Switzerland, Hungary walitikisa nyavu mara 27 [magoli 27] kiwango ambacho ni kikubwa zaidi katika fainali moja za Kombe la Dunia.
- Katika mechi za kuwania kufuzu kwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2001, Australia iliwabamiza American Samoa jumla ya magoli 31-0 kiwango ambacho ni kikubwa zaidi kuwahi kufikiwa.
- Katika umri wa miaka 40, golikipa wa Italy,Dino Zoff alikuwa mchezaji mwenye umri mkubwa kupita wote kuwahi kushinda Kombe la Dunia. Alifanya hivyo mwaka 1982 wakati wa fainali zilizofanyikia nchini Spain.
- Inakadiriwa kwamba kila mchezo wa fainali za Kombe la Dunia huhudhuriwa na watazamaji wapatao 43,000
- Jumla ya hat tricks 48 zimerekodiwa katika historia ya Fainali za Kombe la Dunia tangu mwanzo wake mpaka sasa.
- Rekodi ya refa mwenye umri mkubwa kupita wote kuwahi kuchezesha fainali ya Kombe la Dunia inashikiliwa na George Reader wa Uingereza ambaye alikuwa ana umri wa miaka 53 aliposimamia mchezo kati ya Brazil na Uruguay mwaka 1950.
- Jose Batista wa Uruguay anashikilia rekodi ya mchezaji aliyewahi kutolewa kwa kadi nyekundu mapema zaidi katika historia ya michezo ya fainali za Kombe la Dunia. Alitolewa katika sekunde ya 56 katika mchezo dhidi ya Scotland wakati wa fainali za mwaka 1986.
- Miongoni mwa makosa makubwa kuwahi kufanywa na marefa wakati wa michuano ya Kombe la Dunia mojawapo ni lile la refa muingereza Graham Poll. Graham alimpa kadi tatu za njano beki wa Croatia,Josip Simunic katika mchezo wa raundi ya kwanza dhidi ya Australia wakati wa fainali za mwaka 2006. Kwa kawaida kadi ya pili ya njano hufuatiwa na nyekundu.
- Katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1962 zilizofanyikia nchini Chile, jumla ya wafungaji 6 akiwemo Garrincha wa Brazil walifungamana kama wafungaji wa mabao mengi zaidi. Wote walikuwa na magoli 4.
- Eusebio wa Ureno [Black Panther] alikuwa mfungaji bora wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 1966 zilizofanyikia nchini Uingereza. Alipachika magoli 9.
- Jumla ya magoli 171 yalipachikwa wakati wa fainali za Kombe la Dunia zilizofanyikia Ufaransa mwaka 1998. Ufaransa walishinda fainali hizo.
- Jumla ya nchi 75 zimeshashiriki fainali za Kombe la Dunia. Tanzania haijawahi kushiriki fainali za Kombe la Dunia.
- Mara ya mwisho fainali za Kombe la Dunia kufanyikia barani Amerika ya Kusini ilikuwa ni mwaka 1978 zilipofanyikia nchini Argentina.Zinarudi tena mwaka huu-Brazil.
- Katika fainali za mwaka 1974, Yugoslavia waliibugiza Zaire[sasa DRC] jumla ya magoli 9-0 ikiwa ni mojawapo ya vipigo vikali zaidi katika historia ya fainali za Kombe la Dunia.
- Katika fainali za mwaka 1982, Hungary waliibugiza El Salvador jumla ya magoli 10-1 na hivyo kufikia rekodi ya “vibonde” waliowahi kutandikwa magoli mengi zaidi. Goli la mwisho katika mchezo huo lilifungwa na Tibor Nyilasi kunako dakika ya 83 ya mchezo.
- Jumla ya mashabiki 93,000 waliingia uwanjani [Montevideo Estadio Centenario] kushuhudia mchezo wa fainali za kwanza kabisa la Kombe La Dunia mwaka 1930. Kati ya Uruguay na Argentina. Uruguay walishinda kwa jumla ya magoli 4-2.
- Brazil ndio nchi inayoongoza kwa wachezaji wake wengi kupewa kadi nyekundu katika historia ya mashindano ya Kombe La Dunia. Wameshapewa jumla ya Kadi Nyekundu 11.
- Rigobert Song [Cameroon] na Zinedine Zidane[ Ufaransa] ndio wachezaji wanaoshikilia rekodi ya kutolewa na kadi nyekundu mara nyingi zaidi katika historia ya Kombe la Dunia.Wote wameshatolewa mara 2. Song alitolewa kwa kadi nyekundu katika fainali za 1994 na 1998 wakati Zidane alitolewa mwaka 1998 na 2006.
- Brazil ndio wanashikilia rekodi ya kuwa timu iliyowahi kushinda mechi nyingi zaidi katika historia ya Kombe la Dunia. Wameshinda mechi 67.
- Mexico,kwa upande mwingine, ndio wanashikilia rekodi ya kufungwa mechi nyingi zaidi katika historia za fainali za Kombe la Dunia.Wameshapoteza mechi 22.
- Cafu, beki mstaafu wa Brazil, ndio anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyewahi kushinda mechi nyingi zaidi[kwa maana akiwa na timu ya Brazil] katika historia ya Kombe la Dunia. Cafu alishinda mechi 16 tangu mwaka 1994-2006.
- Baadhi ya wachezaji wenye majina au waliowahi kuwa na majina makubwa sana katika soka na ambao hawajawahi kushiriki katika fainali za Kombe la Dunia ni pamoja na Alfredo di Stefano,Ryan Giggs,George Best na George Weah.
- Norman Whiteside ndiye anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo kabisa kuwahi kucheza katika mechi za fainali za Kombe La Dunia. Alicheza mwaka 1982 katika mchezo baina ya Ireland ya Kaskazini na Yugoslavia akiwa na umri wa miaka 17 na siku 41.
- Brazil ndio inashikilia rekodi ya kuwa nchi ambayo imepachika mabao mengi zaidi katika historia ya fainali za Kombe la Dunia. Wameshapachika mabao 210.
- Ronaldo anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyewahi kupachika mabao mengi zaidi katika michezo ya fainali za Kombe la Dunia. Ana mabao 15
- Bosnia-Herzegovina wanashiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka huu nchini Brazil wakiwa miongoni mwa wawakilishi wa Bara Ulaya.
- Miongoni mwa viwanja vitakavyotumika katika michezo ya Kombe la Dunia mwaka huu huko Brazil, ujulikanao kama Arena da Baixada uliopo katika jiji la Curitiba ndio wenye uwezo mdogo zaidi wa watazamaji wanaoruhusiwa kuingia.Unaingiza watu 28,000 tu.
- Hakuna nchi kutoka nje ya Bara la Amerika Kusini iliyowahi kuchukua Kombe la Dunia katika ardhi au nchi za Amerika Ya Kusini.Yaani kila mara Kombe la Dunia linapofanyikia Barani humo basi Kombe hubaki na mojawapo ya timu za nchi za bara hilo.
- Mabalozi rasmi wa FIFA kwa ajili ya fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia wote wanatoka Brazil. Ni Legends wa mchezo huo Carlos Alberto,Amarildo, Bebeto na Ronaldo.
- Jumla ya fainali 5 za Kombe la Dunia zimeshafanyikia barani Amerika Kusini.Wenyeji wamewahi kuwa Uruguay,Argentina,Chile na Mexico na Brazil. Hii ni mara ya pili kwa Brazil kuwa wenyeji.
- Nchi za Ulaya zimeshashinda au kunyakua Kombe la Dunia mara 10.
- Brazil ndio nchi pekee ambayo inashikilia rekodi ya kushiriki katika kila fainali za Kombe la Dunia. Wameshiriki mara 20. Yaani kila mwaka wamo.
- Lother Matheus wa Ujerumani ndio anashikilia rekodi ya kucheza michezo mingi zaidi ya fainali za Kombe la Dunia. Mara 25.
- Kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia zilionyeshwa “Live” katika luninga mwaka 1954. Inaaminika kwamba bado tukio la fainali ya mwaka huo ndio inashikilia rekodi ya kuwa tukio la kimichezo lililowahi kutazamwa na watu wengi zaidi.
- Golikipa Oliver Khan wa Ujerumani ndio golikipa pekee katika historia ya Kombe la Dunia kuwahi kupewa Kiatu Cha Dhahabu.
- Kwa mara ya kwanza katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu tekinolojia ya “mstari wa goli” itatumika. Kwa maana hiyo yale mambo ya mpira haukuvuka au ulishavuka mstari mwaka huu hayatokuwepo.
- Imechukua miaka 36 kabla ya fainali za Kombe la Dunia kurejea barani Amerika Kusini. Mara ya mwisho zilifanyikia nchini Argentina mwaka 1978.
- Nchi za Argentina na Colombia pia zilikuwa na nia ya kuandaa fainali za Kombe la Dunia mwaka huu.
- Fainali za mwaka huu zinasemekana kuwa ndizo “aghali” zaidi kupita zingine zote katika historia. Ughali huo unatokana na maandalizi na mambo mengine ya kimikakati.
- Wimbo au muziki rasmi wa fainali za mwaka huu unaitwa We Are One[Ole Ola] na umeimbwa na wanamuziki Pitbull,Jeniffer Lopez na Claudia Leitte.
- Lionel Messi ndio mchezaji “ghali” zaidi miongoni mwa wachezaji wanaoshiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka huu.
- Nchi ikayoshinda fainali za mwaka huu,pamoja na Kombe wanaondoka na kitita cha jumla ya dola elfu 35,000 za Kimarekani.
- Ni marufuku kwa wachezaji kuonyesha “ujumbe” wa aina yoyote katika fulani za ndani wanazozivaa.
- Rekodi ya Ronaldo ya kuwa mchezaji mwenye magoli mengi zaidi katika historia ya Kombe la Dunia inaweza kuvunjwa na Miroslav Klose wa Ujerumani ambaye ana magoli 14. Endapo atafunga magoli mawili 2 atakuwa amefikia na kuvunja rekodi ya Ronaldo.
- Fainali za mwaka huu hazitokuwa na nchi au timu yeyote kutoka nchi za Scandinavia. Sio Denmark,Norway,Sweden wala Finland waliofua dafu mwaka huu.
- Jumla ya marefa 25 watasimamia fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia nchini Brazil
- Miongoni mwa nchi zinazoshiriki fainali za mwaka huu Honduras na Bosnia-Herzegovina ndio pekee ambazo hazijawahi kushinda mechi ya Kombe la Dunia.
- Tofauti na michezo ya fainali ya Kombe la Dunia siku hizi ambapo hatua za mwanzo huanzia kwenye miji mbalimbali,fainali za kwanza mwaka 1930 michezo yote ilifanyikia katika jiji moja la Montevideo,Uruguay huku kukiwa na mechi mbili za ufunguzi.
- Nigeria ndio nchi pekee ya Afrika kuwahi kufikia hatua ya 16 bora katika fainali za Kombe la Dunia mara mbili mfululizo….mwaka 1994 na 1998.
- Katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006, timu ya Ivory Coast ilijumuisha jumla ya wachezaji 23 ambao wote walikuwa wanacheza soka nje ya Ivory Coast. Yaani ilikuwa sio dili kabisa kuwa unacheza ligi ya nyumbani.
- Aroune Kone na Bakari Kone ndugu wa kuzaliwa waliichezea Ivory Coast katika fainali za mwaka 2006 huku Yaya Toure na nduguye Kolo Toure wakiichezea Ivory Coast katika fainali za mwaka 2006 na 2010.
- Mshambuliaji Didier Drogba ndiye mchezaji wa timu kutoka Afrika wa kwanza[mwafrika] kuifunga bao Brazil katika mchezo wa Kombe la Dunia. Alifanya hivyo nchini Afrika Kusini katika fainali za mwaka 2010.
- Algeria itakuwa inashiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya tatu.Kwanza ilikuwa 1982 na kisha 1986.Kwa maana hiyo imewachukua Algeria miaka 24 kurudi tena ulingoni.
- Ujerumani watakuwa wakicheza mchezo wao wa 100 watakapombana na Ureno nchini Brazil. Timu hizo zitakutana tarehe 16/June katika mchezo wa fungua dimba wa kundi G.
- Kombe la Dunia mwaka huu litaonyeshwa “Live” duniani kote kupitia televisheni na vyombo vingine vya kurushia na kuonyesha matangazo ya mpira kama vile simu za mikononi,iPads nk.
*Pamoja na jitihada ya kuhakiki taarifa za hapo juu kupitia vyanzo
mbalimbali,yawezekana kuna mahali tumeteleza.Jisikie huru kuturekebisha
kupitia sehemu ya maoni ili kuweka kumbukumbu sawa sawia.Asante-Jeff
Msangi/Mhariri
0 comments:
Post a Comment