KIONGOZI
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Shina Namba 30, Kigamboni Kisiwani jijini
Dar, Bernadetha Shabani (53) amefariki dunia baada ya kupigwa shoka la
kichwa na anayedaiwa kuwa ni mpangaji wake aliyefahamika kwa jina la
Shija Ng’waya (33).
Tukio
hilo la kikatili lilijiri Mei 5, mwaka huu nyumbani kwa marehemu,
Kigamboni jijini Dar es Salaam na marehemu alizikwa Mei 6.Akizungumza
na Uwazi kwa uchungu katika msiba wa marehemu huyo mwishoni mwa wiki
iliyopita, mtoto wa marehemu, Ester Shija (hakuna undugu na mtuhumiwa)
alisema mlalamikiwa huyo alikuwa mpangaji wao kwa mwaka mmoja akahama.
lisema baada ya muda, mtuhumiwa alirudi kwa marehemu mama yake na kudai kuna vitu vyake aliviacha kwenye chumba.
“Mama
alimuuliza ni vitu gani akasema mwiko, tambi za jiko la Mchina, tochi
na redio ndogo. Mama alimwambia hakuviona pengine watoto walivichezea.
Shija akasema yeye anachotaka ni vitu vyake, akaondoka na kuahidi kurudi
siku nyingine.
“Kweli, alirudi tena siku nyingine na kumdai mama vitu vyake na akasema vikikosekana atamuua kisha akaondoka.
“Mama
alikwenda kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa (hakumtaja
jina). Shija akaitwa na kuulizwa ni vitu gani? Akavitaja na kusisitiza
kama asingevipata angemfanyia kitu kibaya mama. Mwenyekiti aliripoti
polisi kutokana na vitisho hivyo.
“Awamu
nyingine, Shija alikuja nyumbani akiwa uchi wa mnyama na kudai vitu
vyake. Siku hiyo akasema kama hatavipata lazima aue, mwenyekiti akaenda
tena polisi, wakaja kumchukua lakini haukupita muda alikuja akamwambia
mama, ‘nimetoka na ni lazima nitakuua.’
“Siku
nyingine tena Shija akaja. Hii ni mara ya nne, tena alikuwa uchi.
Akasema amefuata vitu vyake, mama akampigia simu mwenyekiti na
kumtaarifu, akaja na wajumbe wengine wa serikali na kamati ya ulinzi ya
kijiji wakamchukua Shija mpaka ofisini kwao, wakamuuliza kama alikuwa
tayari kulipwa fedha akavinunue vitu hivyo, akasema yuko tayari kama
atapewa shilingi milioni 3.
...Mazishi.
“Mama
alimwambia kutokana na maisha yake yalivyo anamuomba amlipe shilingi
elfu sabini, Shija akanyanyuka na kuuambia uongozi, ‘mnaona mama huyu
alivyo na dharau, hiyo hela haitoshi thamani ya vitu hivyo, nitamuua
tu,’’ alisema mtoto huyo akimkariri mtuhumiwa na kulia.
Naye
mtoto wa pili wa marehemu, Sofia Mabula alisema: “Shija alifungwa
kifungo cha nje cha miezi sita kutokana na makosa yake lakini cha ajabu
ndani ya mwezi mmoja akatimiza lengo lake la kumuua mama.
“Sidhani
kama mahakama ilistahili kumfunga kifungo cha nje maana alimtishia mama
zaidi ya mara nne mwisho wa siku akamuua kweli, inauma sana.”
Mwenyekiti
wa serikali ya mtaa aliyejitambulisha kwa jina moja la Zakaria ‘Waiti’
alisema aliposikia kwa mara ya kwanza kuhusu madai ya vitu hivyo.
Alijiuliza vilikuwa na nini cha zaidi!
...Waombolezaji.
“Niliwahi
kumuuliza mtuhumiwa kwa nini aling’ang’ania vitu hivyo, akasema alipewa
na babu yake ambaye kwa sasa ni marehemu na vifaa hivyo vilikuwa
vinamsaidia katika maisha yake kwani vina nguvu ya ziada ndani yake,”
alisema mwenyekiti huyo.
Akaongeza:
“Alisema tochi kazi yake ilikuwa kuwatibu watoto wadogo wenye mtoto wa
jicho, mwiko ulikuwa wa mti wa Mkula ambapo alikuwa akipikia chakula
unampa nguvu za kulima. Kuhusu redio ilikuwa ikimsaidia kusikiliza
matatizo ya watu.
Askari
wa JWTZ aliyejitambulisha kwa jina la Koplo Deus wa Kikosi cha
Wanamaji, Kigamboni ndiye aliyemkamata mtuhumiwa wakati akikimbia kwa
kujitumbukiza kwenye Bahari ya Hindi.
Kamanda
wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, SACP Alibert Kiondo alithibitisha kutokea
kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa yuko mikononi mwa polisi,
uchunguzi unaendelea ili kujua utimamu wa akili yake.
0 comments:
Post a Comment