Monday, April 28

KUNA watu uhusiano wao unawaka moto kwa migogoro ya kila siku. Wengine ni marafiki kwa maana ya wapenzi lakini pia kuna wanandoa ambao nyumba zao zinayumba.
Wanatumia muda mwingi kuzungumzia migogoro badala ya mambo mengine ya msingi katika ndoa yao. Kuungana katika ndoa kunamaanisha kusaidiana. Mwanamke anakwenda kuwa msaidizi wa mwanaume wake. 

Kukikosekana amani maana yake kila mmoja atakuwa kivyake; kama ndivyo, maendeleo kwenye familia yatatokea wapi?
Ndugu zangu, WANAWAKE NDIYO MSINGI WA MAFANIKIO KATIKA NDOA. Hata kama baba anatafuta kiasi gani kama hatakuwa na mwanamke ambaye anampa amani, ni wazi kwamba  fedha anazosaka zitapotea!

Hapa nitakupa siri muhimu ambazo wanawake wengi hawazijui kuhusu wanaume. 

Heshima, unyenyekevu; Mwanaume kiasili ni kiongozi wa mwanamke, hivyo ikiwa mwanamke wake ataonyesha hakubaliani na uongozi wake, akashindwa kumnyenyekea kwa mapenzi mazito, ni wazi atapoteza nafasi yake au hata kama itaendelea kuwepo haitakuwa na nguvu.

Uanaume; Mwanaume anajiamini lakini anajisikia vizuri kama mwanamke wake atatambua, kuthamini na kuonyesha uhitaji wa uanaume wake. Siku zote anapenda aonekane ndiye mwamuzi wa mambo magumu. Mshauri mkuu na kiongozi bora.
Jaribu kuwa karibu na mwanaume wako, mshirikishe katika mambo na onyesha wazi kuwa bila yeye, huwezi kukamilisha jambo lako. Huu ni uchawi mkubwa sana kwa wanaume.

Kubanwa; Wanaume wengi hawapendi kufuatiliwa sana, hawapendi kubanwa na kuulizwa kila mara mahali walipo (hasa baada ya muda wa kazi). Kumbana humaanisha humwamini au hutaki kumpa nafasi angalau ya kukutana na rafiki zake.
Ukimpa uhuru utashangaa anaongeza mapenzi na atakuja na mambo mengi mapya ambayo si ajabu atakuwa amejifunza kutoka kwa wenzake.

Mahaba ya wazi; Ni kweli kwamba kuonyeshana mapenzi ya wazi hunogesha penzi lakini kwa wanaume ni tofauti kidogo. Mfano, mwanamke hujisikia fahari zaidi, akishikwa mkono na mwanaume wake na kuongozana kwenye hadhara lakini wanaume wengi hawana hulka hiyo. Ni muhimu kuchunguza, je, mwenzako anapenda? Maana yawezekana kati ya wachache wanaopenda, mwanaume wako yupo. 

Kuitikia hisia; Unatakiwa kumjua mwanaume wako na kuitikia hisia zake. Msome na umjue. Mpe anachohitaji kwa wakati uleule anaotaka. Hiyo itakufanya uwe mwanamke sahihi kwake na siyo mzigo!

0 comments:

-