TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara kufuatia kifo cha mwanamuziki
maarufu na wa siku nyingi, Muhidini Maalim Gurumo kilichotokea tarehe
14 Aprili, 2014 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa
amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo uliomsumbua kwa muda mrefu.
“Nimesikitishwa
na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Muhidini Maalim Gurumo ambaye
alikuwa mmoja wa wasanii wa muziki wa dansi nchini waliolitumikia Taifa
hili kwa bidii tangu miaka ya sitini kupitia sanaa ya muziki katika
bendi mbalimbali za muziki wa dansi kuanzia Bendi ya NUTA Jazz, Mlimani
Park Orchestra, Orchestra Safari Sound (OSS) na Msondo Ngoma ambayo
ameitumikia hadi alipostaafu mwaka 2013”,amesema Rais Kikwete katika
Salamu zake.
Rais
Kikwete amesema mchango wa Marehemu Muhidini Maalim Gurumo kwa Taifa
letu ni mkubwa na wa kupigiwa mfano kupitia kipaji alichojaaliwa na
Mwenyezi Mungu ambacho alikitumia kikamilifu kwa manufaa ya wananchi wa
nchi yetu na Taifa kwa ujumla.
Rais
Kikwete amemuomba Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi kwa familia ya
Marehemu Muhidini Maalim Gurumo kwa kumpoteza kiongozi na mhimili wa
familia yao. Amesema binafsi anaungana na familia ya marehemu
kuomboleza msiba huu mkubwa kwa kutambua kuwa msiba wao ni wa wote, na
anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala
pema peponi Roho ya Marehemu, Amina.
Aidha
Rais Kikwete amewaomba wanafamilia ya marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu
na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza msiba wa mpendwa
wao kwa kutambua kwamba yote ni mapenzi yake Mola.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
14 Aprili, 2014
0 comments:
Post a Comment