Kundi maarufu la muziki wa Kwaito la nchini Afrika kusini, Mafikizolo linatarajia
kutua mchana huu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya onesho moja tu linalotarajia
kufanyika katika ukumbi wa Mlimani City, kesho, Jumamosi Aprili 5 mwaka huu.
Mafikizolo imekuwa
na rekodi nzuri ya kushinda kwenye tuzo mbalimbali za muziki, kutokana na kupiga
muziki na kucheza kwa umahiri, hasa mtindo wao maarufu wa Kwaito.
Kundi hilo
linaloundwa na wasanii wawili(Nhlanhla Nciza na Tebogo Madingoane pichani juu), kwa sasa linalotamba na vibao kama
"Khona" na "Happiness", watawasili nchini kesho mchana kwa
ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini.
Hii itakuwa ni mara
ya kwanza kwa kundi hili kufika nchini, tangu kuachia wimbo wao wa
"Khona", wimbo ambao umesababisha kundi hilo kujizolea umaarufu
mkubwa kwenye kumbi za starehe, na hata katika vituo mbali mbali vya redio.
Mafikizolo kwa sasa
wanashikilia taji la kundi bora la mwaka, kwa mujibu wa tuzo za muziki za SAMA
(South African Music Awards), huku wakiongozwa kwa kutajwa mara nyingi kwenye tuzo za Ulaya kama kundi bora la
muziki kutoka Afrika.
Kundi hilo maarufu
kuliko yote yaliyowahi kutokea kusini mwa Afrika liliwahi kutamba pia miaka ya
nyuma na nyimbo kama "Ndihamba Nawe", "Ndixolele",
"Sebenza", "Ndashata" na "Ndizolila".
Onesho la hilo,
linatarajiwa kuanza saa moja usiku ambapo kiingilio kitakuwa shilingi 20,000
kwa watakaolipa kabla ya onyesho, huku mlangoni watalipia shilingi 35,000 za
kitanzania.
Kundi hilo mwaka
huu, limeingia katika vipengele vinne kwenye kinyanga’anyiro kikubwa cha tuzo
za SAMA.
Katika
kinyang’anyiro hicho chenye vipengele 28, kundi hilo limepata nafasi ya kuwania
vipengele vinne, ambavyo ni Kolabo Bora ya Mwaka, albam Bora ya Pop ya Mwaka,
albam ya Mwaka kupitia albam ya Reunited, na kundi bora la Mwaka.
Kwa mujibu wa
tovuti ya destinyconnect, hafla ya ugawaji tuzo hizo itafanyika nchini humo
Aprili 28 mwaka huu.
Kundi hili lilianza
shughuli za kimuziki tangu miaka ya 1990, albamu yao ya kwanza walitoa mwaka
1996. Tangu hapo wameshatoa albamu sita, baada ya kutoa albamu yao ya tano
mwaka 2003 "Kwela".
0 comments:
Post a Comment