Wednesday, March 19

                         
MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, ametaja mambo manne yaliyoishawishi Tume yake kupendekeza Muungano wa serikali tatu.
Mambo hayo ni Tanganyika kuvaa koti la Muungano, kuongezeka kwa mambo ya Muungano, mgongano wa Katiba, michango na gharama za Muungano na mgao wa mapato ambayo alisema yanahatarisha Muungano wa sasa wa serikali mbili.

Jaji Warioba alisema Zanzibar inalalamika kwamba Tanganyika imejificha kwenye koti la Muungano na ndiyo inayofaidi na Wazanzibari wanaiita ni Serikali ya Tanzania Bara na sio ya Muungano.

Alisema orodha ya mambo ya Muungano ni suala ambalo limelalamikiwa kwa muda mrefu na hatua zilizochukuliwa ni kupunguza mambo ya Muungano.

Katika eneo hilo, alisema suala la uhusiano wa kifedha pia limekuwa na utata kwa muda wa takribani miaka 40 na kiini chake ni malalamiko ya kutoka kila upande kuhusu nani anafaidi rasilimali za Taifa.

“Kwa tathmini ya Tume, muundo wa serikali mbili hauwezi kubaki kwa hali ya sasa, Muungano wa Serikali mbili waliotuachia waasisi siyo uliopo sasa,” alisema Warioba na kueleza kuwa umebadilishwa mara nyingi wakati mwingine bila kufanya mabadiliko ya Katiba. Muungano wa waasisi Alisema waasisi walituachia Muungano wa nchi moja yenye serikali mbili na siyo nchi mbili zenye serikali mbili;


“Muundo wa serikali mbili, unaweza kubaki tu kama orodha ya mambo ya Muungano haitapunguzwa, bali itaongezwa. “La sivyo (kama mambo ya Muungano yatapunguzwa), Serikali ya Muungano itabaki na rasilimali na mambo ya Tanzania Bara tu, katika hali ya namna hiyo pande zote mbili zitaendelea kulalamika. Zanzibar kwa upande wake, imekuwa ikidai kwamba fedha na rasilimali za Muungano zinatumika na kuinufaisha Tanzania Bara chini ya kivuli cha Muungano.

Aidha, kwa upande wa Serikali ya Muungano, inadaiwa kwamba Tanzania Bara ndiyo inayochangia fedha na rasilimali nyingi katika Muungano hivyo inayo haki ya kutumia fedha na rasilimali hizo kwani Zanzibar kwa muda mrefu, imekuwa haichangii katika fedha na rasilimali hizo za Muungano.

Jaji Warioba alisema kwa kipindi cha miaka 30 kumekuwepo na hoja za muundo wa serikali tatu kama kuchafuka kwa hali ya kisiasa Zanzibar chanzo chake ilikuwa serikali tatu, Tume ya Jaji Nyalali, Kundi la G 55 ilikuwa ni kuundwa kwa serikali Tanganyika, Kamati ya Jaji Kisanga ilipendekeza serikali tatu na pia Tume yake imepata maoni ya wananchi kuwa wanataka serikali tatu.

Jaji Warioba alisema matendo ya Serikali katika kipindi cha miaka 30 na hatua zinazochukuliwa, zimefanya mamlaka na madaraka ya Muungano yapungue na madaraka ya SMZ yameongezeka na Serikali ya Muungano imebaki ikishughulikia mambo ya Tanzania Bara tu kwa upande wa maendeleo.

“Jambo kubwa zaidi katika kuchukua hatua hizi, ni kuvunjwa kwa Katiba, hili sio jambo dogo, kama Katiba haitaheshimiwa nchi haitakuwa salama, mapendekezo ya Tume yanalenga kuondoa matatizo yanayohatarisha kuyumba kwa Muungano ili kuzuia pande zote mbili kuendelea kuchukua hatua zinazovunja Katiba,” alisema Warioba.

Kuongezeka Akichangua mambo hayo, Jaji Warioba alisema kuongezeka kwa mambo ya Muungano Wazanzibari wanadai kuwa kunapunguza mamlaka ya Zanzibar. Alisema Tume ilifanya uchambuzi wa mambo ya Muungano ili kubaini kama yanaingilia hadhi na mamlaka ya Zanzibar.

Alisema kati ya mambo 22, Tume imebaini kuwa siyo mambo yote yanayotekelezwa kikamilifu na kimuungano na alisema mambo mengi yamebadilishwa bila ya kubadili Katiba ama kwa makubaliano kati ya pande zote mbili za Muungano au kwa hatua zilizochukuliwa na upande mmoja.

Jaji Warioba alisema katika kipindi chote cha miaka 20 iliyopita, kamati nyingi zimeundwa kushughulikia matatizo ya Muungano na baadhi yake zilipendekeza kuondoa mambo mengi zaidi kutoka kwenye orodha ya mambo ya Muungano na akatoa mfano wa Tume ya Amina Salum Ali ya Zanzibar, iliyopendekeza kuondolewa mambo 12.

Alisema mwaka 2003 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, iliunda kamati nyingine kuchambua matatizo na kero za Muungano na taratibu za kuziondoa na kamati hiyo ilipendekeza mambo 14 ambayo yanatakiwa kuondolewa kwenye Muungano ikiwemo Polisi na mambo ya usalama. Warioba alisema kuwa mambo hayo yakiondolewa kwenye orodha ya mambo ya Muungano, serikali ya Muungano itakuwa imebaki na mambo ya Tanzania bara tu kwa upande wa maendeleo.

Alisema Tume ilitafakari kama kuna uwezekano wa kuyarudisha mambo yaliyoondolewa kwenye orodha kutokana na muafaka wa 1994, lakini tathmini ya Tume ni kwamba kufanya hivyo ni kuzua mgogoro upya kwani itaonekana mamlaka ya Zanzibar yanaingiliwa.

Alisema wakati Tume ilipokuwa inakusanya maoni ya wananchi wengi wa Zanzibar, wote walipendekeza mambo mengi yaondolewe kwenye Muungano.

Alitoa mfano kuwa wale waliotaka serikali ya mkataba, walitaka mambo yote yaondolewe kwenye orodha ya Muungano, isipokuwa suala la ulinzi na wale waliotaka serikali mbili walitaka mambo yote ya uchumi yaondolewe kwenye orodha ya Muungano.

Jaji Warioba alisema kuyarudisha mambo ambayo hivi sasa yako chini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, hata kama sio ya kikatiba kunaweza kuleta mgogoro wa kisiasa.

Mgongano wa Katiba Jaji Warioba alisema ibara ya 132 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 imeweka masharti kwamba sheria zinazotungwa na Bunge la Muungano hazitatumika Zanzibar hadi zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi.

Alisema jambo hilo limeleta mgongano mkubwa kwani katika muafaka wa 1994, serikali zote zilikubaliana kwamba Zanzibar ifanye mabadiliko kwenye Katiba yake ili mgongano huo wa Katiba uondolewe.

“Lakini hadi sasa muafaka haujatekelezwa,” alisema Warioba na kuongeza kuwa zaidi ya hapo mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010, yametamka wazi kwamba Zanzibar ni nchi kati ya nchi mbili zinazounda Muungano wakati Katiba ya Muungano inaelekeza kwamba Tanzania ni nchi moja.

Alisema mabadiliko katika Katiba ya Zanzibar pia yamehamisha baadhi ya madaraka ya Serikali ya Muungano kwenda Zanzibar na akatoa mfano Katiba ya Jamhuri ya Muungano, inampa Rais wa Jamhuri ya Muungano mamlaka ya kuigawa nchi katika maeneo, lakini Katiba ya Zanzibar imeyahamisha madaraka hayo na kwenda kwa Rais wa Zanzibar.

Jaji Warioba alisema Tume ilibaini kwamba haitakuwa rahisi kubadili Katiba ya Zanzibar kuifanya Zanzibar kuonekana kuwa sehemu ya Muungano badala ya kuwa sura ya nchi. Alisisitiza kuwa mabadiliko ya aina hiyo yanahitaji kura ya maoni kama Katiba ya Zanzibar inavyoelekeza.

“Kwa tathmini ya Tume, baada ya kuwasikiliza wananchi wa Zanzibar ni dhahiri kwamba uwezekano wa kufanya mabadiliko kwenye Katiba ya Zanzibar ili Zanzibar iwe sehemu ya nchi moja badala ya kuwa nchi ni mdogo.

Michango, mapato Jaji Warioba alisema matumizi ya fedha za Muungano, michango ya pande zote mbili kwa shughuli za Muungano na mgawo wa mapato ya Muungano, yamekuwa ni masuala yenye utata kwa muda mrefu.

Alisema mwaka 1977 NEC ya CCM ilitoa uamuzi kwamba mapato ya kodi za Muungano yabaki upande wa Muungano yanapokusanywa lakini tatizo hilo halikumaliza matatizo.

Alisema Zanzibar imekuwa ikidai kwamba fedha na rasilimali za Muungano zinatumika na kuinufaisha Tanzania Bara chini ya kivuli cha Muungano. Pia alisema kwa upande wa Serikali ya Muungano inadaiwa kwamba Tanzania Bara ndiyo inayochangia fedha na rasilimali nyingi katika Muungano.

Kwa sababu hiyo Wabara wanadai kuwa wanayo haki ya kutumia fedha na rasilimali hizo kwani Zanzibar kwa muda mrefu imekuwa haichangii katika fedha za rasilimali hizo za Muungano.

“Kutokana na matatizo haya, chombo maalum cha kikatiba yaani Tume ya Fedha kilianzishwa ili kushughulikia masuala ya uhusiano wa kifedha baina ya Serikali ya Muungano na SMZ.

Baada ya wajumbe wa Tume hiyo kuundwa mwaka 2003 ikiwa ni baada ya miaka saba tangu kutungwa sheria ya kuanzishwa kwake, Tume hiyo ilipendekeza kiwango cha uchangiaji gharama za Muungano na kiwango cha mgawo na utaratibu wa mgawanyo wa mapato ya Muungano baina ya serikali hizo.

Warioba alisema tume hiyo ilipendekeza kwamba masharti ya Katiba yatekelezwe kuanzishwa kwa akaunti ya fedha ya pamoja ambapo fedha yote inayohusu gharama za Muungano itawekwa. “Hadi sasa huu ni mwaka wa nane tokea mapendekezo hayo hakuna hata kati ya mapendekezo hayo lililotekelezwa au kuchukuliwa hatua,” alisema Jaji Warioba.

Jaji Warioba alisema tathmini ya Tume ni kwamba siyo rahisi mambo hayo kutekelezwa chini ya muundo wa serikali mbili hiyo ni kwa sababu wizara za Serikali ya Muungano ni mchanganyiko.

Alisema zipo wizara ambazo zinashughulikia mambo ya Muungnao tu na zipo zinazoshughulikia mambo ya Bara peke yake na zipo zingine zinashughulikia mambo

0 comments:

-