Thursday, September 5

                                
Wiki iliyopita tulianza somo hili lenye mada kuhusu dondoo zinazoweza kusaidia kuimarisha mapenzi, bila kupoteza muda tuendelee kutoka pale tulipoishia.

TENDO LA NDOA: Wataalamu wameandika mengi kuhusu umuhimu wa kutoshelezana kwenye tendo la ndoa, hivyo sipendi kueleza mengi lakini pengine nijazie kwa kusema kuwa

mazungumzo juu ya kuridhishana na sehemu muafaka za kusisimuana ni vyema yakapewa kipaumbele ili kila upande uhudumiwe na kufurahia tendo ipasavyo.

KUAMBATANA: Tumeangalia dondoo inayoelezea umuhimu wa wapenzi kuambatana kwenye matembezi yao, lakini sehemu hii tunaelezea umuhimu wa kwenda kwenye manunuzi ya mahitaji mkiwa pamoja. Kitendo hiki hujenga mapenzi kwa kiwango cha juu na huchochea hamasa ya kila mmoja kujiona ni sehemu ya mwenzake.

KUSHIKANA: Mnapokuwa kwenye matembezi yenu ya jioni, mnashauriwa kuwa na tabia ya kushikana mikono au sehemu nyingine yoyote ya mwili. Kitendo hiki hufuta hisia za kuoneana aibu mbele za watu na huongeza uaminifu kwa wapenzi.

TENDO ALILOTAKA KUTENDA: Ikiwa mwenza wako aliwahi kukuambia kuwa anakusudia kufanya jambo fulani, unachotakiwa wewe ni kujiandaa kwa upande wako na kulifanya bila kumwambia.Kwa mfano, “Mpenzi wangu niliwahi kusikia unataka kununua kabati la vyombo, tayari lipo ndani kwetu.”

SIKILIZA: Kusikilizana ni jambo muhimu. Mpenzi wako anapokuambia kitu unatakiwa kumsikiliza, ni vibaya kuwa na maamuzi ya upande mmoja kwani utamfanya mwenzako ajisikie vibaya hasa pale anapokushauri jambo zuri lenye manufaa kwa maisha yenu halafu wewe usilitende.

KULA PAMOJA: Kitendo cha wapenzi kuamua kutoka na kwenda kwenye mgahawa kula chakula cha jioni pamoja huchochea hisia za mapenzi. Mbali na hilo, jenga penzi lako kwa kupendelea kula chakula na umpendaye.

KUTAZAMA PICHA: Inapendeza sana wapenzi wakitafuta sehemu tulivu na kutumia muda wao kutazama picha zao za utoto au zile walizopiga mwanzo wa penzi lao na kukumbushana hali ilivyokuwa wakati huo. Kusema kweli ni kitendo kilichothibitika kuchochea hamasa za mapenzi.

KUHUSU CHAI: Chai ya asubuhi ya wapendanao ni vyema ikanywewa chumbani, hasa kama wote ni wafanyakazi au mmoja wao. Usiulize kwa nini isiwe sebuleni, ni kwa sababu ya kutoa fursa ya kuhudumiana kwa ukaribu na uhuru zaidi kama wapenzi. Ila kama wapenzi hunywa chai ya kifamilia si vibaya wakiungana na jamaa zao, ila wakakaa karibu.

KUCHANGIA FARAGHA: Kuna mambo mengi yanayohusu faragha za wapenzi, hivyo ni vyema kuwa na desturi ya kushirikishana na kuyachangia kwa pamoja. Mfano kutazama video za mapenzi, kuelimishana kuhusu mitindo na mambo ya siri.

MIRADI YA PAMOJA: Mnapokuwa wapenzi mnaoaminiana ni vizuri kuwa na miradi na mipango ya kimaendeleo ya pamoja na ikiwezekana ushirika wenu uwe wazi ili kuufanya kila upande ujione ni sehemu ya mafanikio. Haifai mwanaume au mwanamke kuendesha maisha yake peke yake (kujenga nyumba, kununua kiwanja), bila kumshirikisha mwenzake. 

KUKUMBUSHANA: Kichocheo kingine cha mapenzi ni kuwa na tabia ya kukumbushana mambo yenu ya zamani. “Unakumbuka ulipokuja kunitorosha siku ile usiku, halafu tukakutana na baba?” Kifupi kumbukumbu huleta hali ya mtu kujitambua alikotoka na aendako, kukumbushana huko kusiwe kwa mambo ya zamani tu bali kwa kila jambo linaloonekana kusahaulika na upande mmoja.

KUOGA PAMOJA: Wapenzi wengi hupuuza sana tendo la kwenda bafuni kuoga pamoja, wanawake wengi hudhani kuwa kumpelekea mume wake maji bafuni au kumuandalia taulo inatosha, hapana! Kwa kadiri muwezavyo pendeleeni kuoga pamoja, kwani kuoga pamoja husaidia kujenga hisia za kimapenzi.

KUBEBA PICHA YA MWENZA WAKO: Inafahamika kuwa wanaume hubeba ‘waleti’ na wanawake huwa na pochi ambazo wataalamu wanashauri ziwe na picha za wale wanaowapenda, si kwa faida yao lakini ni ya wapenzi wao ambao hutajwa kujisikia vizuri wanapotambua kuwa wamepewa kipaumbele kwa kuwekwa kwenye waleti au pochi.

Itaendelea wiki ijayo...

0 comments:

-