Sunday, August 11

Wanawake wengi hupenda sana kujitangaza kwamba wanapendwa na wapenzi wao, lakini nyuma yao huwa hawana majibu au hoja za msingi za kuthibitisha kwamba wanachokisema ni cha kweli. Kupendwa na mwanaume hakuishii kwenye kutamkiwa na kukubaliana bali ni zaidi ya hapo.
Ni vyema kwa kila mwanamke kujiuliza maswali ishirini yafuatayo kabla ya kuruhusu moyo wake kuridhika na mapenzi kutoka kwa mwanaume aliyenaye.

Kwanza: Je mpenzi wako anajaribu kwa kila hali kukufanya ujisikie kuwa huru na mwenye kufurahia uhusiano wa kimapenzi?

Pili: Je mwanaume uliyenaye anaonesha kukujali, kujitolea na kukuepushia madhara kwenye maisha yako? Fikiria kuhusu namna anavyokusaidia.

Tatu: Je anapokusaidia kwa chochote amekuwa akifanya hivyo kwa moyo au huambatanisha na masharti fulani? Mfano anapokupa zawadi ya kadi, maua na nguo huwa anawajibika kwako au hukuwekea vitu vya kufanya kabla hajakupa? “Nina zawadi yako lakini huko siji njoo kwangu uchukue.”

Nne: Anafanya vitu vinavyoonesha kwamba anakupenda? Maana ni lazima mapenzi yaambatane na matendo isiwe ni kusema peke yake.

Tano: Je ni mara ngapi amekufanyia ‘sapraiz’?
Sita: Je anakuchukulia wewe kama malkia wake unapokuwa naye? Haitoshi kuwa wawili sehemu, halafu ukawa kama mtu unayejipendekeza kwake. Lazima uwepo wako ujaze furaha.

Saba: Mnapokuwa pamoja hujaribu kukuchombeza kwa utani kidogo kwa lengo la kukufanya ucheke au ni kununa na ukali mwanzo mwisho?

Nane: Je amekuwa mtu mwenye kuonesha hisia zake za mapenzi kwako bila kutumia maneno. Mfano mnapokuwa wawili amekuwa mtu anayependa kuegemeza kichwa chake kwako au kukushika mwilini na wakati mwingine kupenda mgusane?

Tisa: Amekuwa akitoka nawe ‘out’ au ni mwingi wa kutoa visingizio?

Kumi: Ni hodari kukushirikisha katika mipango ya maisha yake ya baadaye na safari zake hasa za mwishoni mwa wiki au anafanya apendavyo?

11: Je amekuwa mwepesi kukutambulisha kwa rafiki zake na utambulisho huo huufanya sawa na uhusiano wenu au huficha na kukwepesha maana?

12: Vipi kuhusu ushiriki wako kwenye shughuli za jamii, amekuwa anaenda peke yake au mnaambatana?

13: Je amekuwa akiwazungumzia ndugu zake mbele yako na kukueleza maisha yao kwa ujumla na pengine kukuelimisha mila za kwao?

14: Mapenzi huonekana kwenye macho, vipi unapokuwa unatazamana naye unaona hisia za penzi machoni au ndiyo kama unaangalia na mwanamke mwenzako tu?

15: Je mpenzi wako huridhishwa na muonekano wako, hasa uvaaji na amekuwa akikurekebisha ili kukufanya uvutie?

16: Vipi kuhusu kukusikiliza, mwanaume uliye naye ni msikivu kwako au anapenda kuongea zaidi yeye na kutaka ufanye anavyokuagiza?

17: Mnapokutana na mpenzi wako huwa na furaha au huhisi kero kiasi cha kutaka kuondoka haraka haraka?

18: Je amekuwa akitimiza ahadi zake? Mfano, kama amekuahidi kukununulia nguo amekuwa akitekeleza kwa wakati au huchelewa? Vipi anapochelewa hukupa sababu au hubaki kipya mpaka umkumbushe.

19: Je amekuwa akishiriki nawe kwenye vitu unavyovipenda na pengine kutaka kujifunza ili muwe pamoja?

20: Je anaweza kuacha kazi zake muhimu na kuja kukusikiliza hasa pale unapohitaji uwepo au msaada wake? Bila shaka majibu ya maswali haya yatakupa mwanga wa kujua kama kweli unapendwa au unajipenda mwenyewe.

0 comments:

-