Friday, August 30

 
Ni matumaini yangu kuwa msomaji wangu umzima wa afya njema na unaendelea na majukumu yako ya kujitafutia mkate wa kila siku. Namshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema na kunipa tena nafasi ya kubadilishana mawazo kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu uhusiano wa kimapenzi.

 
Rafiki, bila shaka ipo wazi kwamba kila mmoja anapenda kuwa na mpenzi ambaye mbali na kumpenda kwa moyo wake wote, atapenda kumfanya awe kama ndugu, rafiki au zaidi ya hapo. Atakayekuwa tulizo la moyo, kivuli kwenye jua kali, maji jangwani na tiba kwenye maradhi.
Hakuna anayeweza kuukabidhi moyo wake kwa mtu ambaye anajua fika kwamba atamtesa, atamnyanyasa, kumsababishia maumivu ya moyo, kuwa kero kwenye maisha yake na ‘kum-treat’ kama adui yake.
Mapenzi ni sanaa kama zilivyo sanaa nyingine. Kwa mfano, ili kumudu kupiga gitaa au kinanda na kupata muziki mzuri, ni lazima ujifunze. Kwenye mapenzi ni hivyohivyo, ili kuishi vizuri na mpenzi wako ni lazima ujifunze. Usichoke kujifunza kila kukicha ili kuwa na uhusiano imara na ndoa inayoweza kudumu, jifunze kupenda na kumuenzi umpendaye kwa moyo wako wote.
Labda nikuulize rafiki yangu, wewe ulijifunzia wapi mapenzi? Shuleni, nyumbani, chuoni, mitaani au mtandaoni? Yawezekana ukatafsiri mapenzi kwa maana ya tendo la ndoa lakini hapa simaanishi hivyo, nazungumzia sanaa nzima ya mapenzi katika tafsiri pana.
Ukweli ambao unashangaza, watu wengi wana uelewa mdogo juu ya suala zima la maisha ya kimapenzi, jambo ambalo linasababisha waishi kimazoea na kushindwa kufuata misingi halisi ya jambo hilo nyeti katika maisha.
Matokeo yake, watu ambao awali wakati wanaanzisha uhusiano wa kimapenzi walikuwa wanapendana na kugandana kama ruba, huishia kuwa maadui na kuvunja uhusiano wao kwa majuto mengi. Yaani mtu ambaye awali alikuwa kipenzi cha roho yako, anabadilika na kuwa mwiba mkali maishani mwako.

NINI HUMFANYA MPENZI AWE ADUI?
Kwa kawaida, mnapoanzisha uhusiano wa kimapenzi kila mmoja humueleza au kumuonesha mwenzake nini anapenda na kipi hakimfurahishi. Kwa kuwa mapenzi ni suala la hiyari, mwenzio anapokukabidhi moyo wake anategemea kuwa utayafanya yale yanayomfurahisha na kuepuka yale yanayomuudhi kwa kadiri uwezavyo. Wazungu wana msemo mmoja kwamba ‘penzi la kweli humsukuma mtu kumfurahisha mpenzi wake kwa kadiri ya uwezo wake na kamwe halitafuti visingizio’.
Usitafute visingizio linapokuja suala la kumfurahisha mwenzio. Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo yanaweza kumgeuza mpenzi wako akawa adui yako.

UKISHINDWA KUMSIKILIZA
Mapenzi ni kusikilizana kwa kila jambo, hakuna nguzo muhimu kama kukubali kuupokea udhaifu wa mwenzako. Jenga mazoea ya kumsikiliza mpenzi wako kwa staha! Hata kama amekukwaza (lazima itatokea tu kwani yeye siyo malaika), tafuta namna nzuri ya kufikisha hisia zako kwake.
Kabla ya kumsikiliza usikimbilie kumhukumu, kumsimanga, kumvunja moyo au kutoa kashfa ambazo zitamfanya asononeke ndani ya moyo wake kwani vitu hivyo vikizidi, hupunguza hisia za upendo na chuki huanza kujengeka taratibu.
Epuka maudhi ya mara kwa mara, endapo mwenzako ameshakwambia kwamba jambo fulani halipendi, msikilize na muoneshe kwa vitendo kwamba umebadilika. Mpe muda wa kuzungumza mambo yanayomkera ndani ya moyo wake bila kumkatisha, hata kama anachokizungumza hukubaliani nacho.
Mapenzi ni hiyari, ni lazima wakati mwingine ukubali kuwa mjinga kwa lengo la kulinda uhusiano, usiendekeze malumbano na mabishano yasiyo na lazima kwani hapo ndiyo mbegu ya chuki humea haraka.
Kama amekuudhi na unadhani huwezi kuzungumza naye au kumsikiliza kwa wakati huo, kaa mbali naye mpaka hasira zitakapoisha kisha rudi na zungumza naye kwa lengo la kutaka suluhu.

Itaendelea wiki ijayo.

0 comments:

-