Sunday, August 11

                                
ASALAAM aleiykhum msomaji wangu, Nitakuwa hapa kila siku kwa uwezo wa Mungu ili kukupa somo, vilevile kujibu maswali yako. Lengo langu ni moja tu, kukuwezesha wewe mwanamke mwenzangu kutulia kwenye ndoa au penzi lako.
Mwanamke ndiyo dira ya mwanaume. Ukiona mumeo hatulii, mwanaume wako anakuwa na hulka ya kurukaruka, jiangalie mwenyewe mara mbili. Katika kila uhusiano wenye migogoro, ukiuchunguza kwa makini unabaini uwepo wa upungufu mkubwa wa mwanamke katika ‘kumhendo’ mwanaume wake.
Mada yangu leo inahusu namna ya kumtuliza mwanamke kiguu na njia. Shoga yangu, nataka kuanzia leo utambue kuwa mwanaume si malaika. Kwa maana hiyo, unatakiwa ujue jinsi ya kucheza naye kama binadamu. Acha kiburi, usizubae, msome vizuri kisha mpatie. Atatulia tu.
Shosti, kumbuka kuwa unatakiwa kumbembeleza mumeo kwa njia yoyote mpaka atulie. Mwanaume hauzwi dukani, ‘supermarket’ wala hana bei. Ingekuwa anauzwa na bei yake inajulikana, kila mtu angekuwa naye. Angetumia jeuri ya fedha kumpata anayemtaka.
Hebu shoga yangu kaa na mshangao sasa, wanawake wengi tu tena wana fedha nyingi, wanaumia upweke, hawana waume wa kutulia nao. Kama wewe unaye wako, tena bahati nzuri mmefunga ndoa, hakikisha unamtuliza ili ufurahie maisha yako ya kimapenzi.

TUMIA NJIA HIZI KUMWEKA SAWA MWANAUME WAKO
Kwanza kabisa, unapoona mwanaume wako amekuwa kiguu na njia, yaani hatulii, tafuta sababu zinazomfanya awe hivyo. Je, sababu ni wewe mwenyewe? Una wivu sana, una mdomo mchafu, kiburi, huelekei anavyokuelekeza? Labda una roho mbaya kwa ndugu zake. Tazama mambo hayo.
Hatua ya pili; Ukishajichunguza, muombe mwanaume wako kikao ili mzungumzie matatizo yenu. Usikae kimya wala usimwogope. Katika kikao hicho, mwache aongee ya moyoni, nawe sema yako, mwisho utajua nani mwenye matatizo. Baada ya hapo, fanyeni masahihisho. Ulipokosea omba msamaha.
Hatua ya tatu; ikiwa katika mazungumzo umegundua mwanaume wako ndiye tatizo, mweleweshe taratibu mpaka aelewe makosa yake. Achana na maneno ya watu wasiojua thamani ya mume ambao hudiriki kusema: “Atajijua akitaka atasema na mimi asipotaka aache mimi nd’o mkewe.”
Kasoro nyigine ni kwamba wapo wanawake hutaka kuishi kwa mashindano na wanaume zao. Nawaombeni mashoga zangu msifanye hivyo, mwanamke akiwa kiguu na njia, aibu yake ni kubwa zaidi ya mwanaume. Uchafu wako, utamfanya yeye aonekane msafi wakati ukweli naye hajatulia.
Pengine mwanaume wako hatulii nyumbani lakini si kwa sababu ana wanawake wengine. Inawezekana ni mtu wa kuwaendekeza marafiki, kwa hiyo wanakaa baa au maeneo mengine, wanazungumza mpaka usiku wa manane ndiyo anarudi nyumbani.
Sasa ikiwa nawe utaanza kuzurura halafu mna watoto, mtawalea saa ngapi? Nani atamrekebisha mwenzake? Nakuhakikishia shoga, wewe ukiamua, mwanaume wako atatulia nyumbani. Maneno yako mazuri na tabia yako njema, ni silaha.
WANAWAKE TUNAPOTEA
Bibie, sisi wanawake wa siku hizi ni tatizo. Angalieni ndoa za zamani zilikuwa zinadumu kwa  sababu wanawake walikuwa wakifuata taratibu. Mke anamuomba mume wake wakae na kutafuta suluhu pasipo hata jirani kujua. Siku hizi, rafiki au shoga ndiyo wa kwanza kwenda kumhadithia na kumuomba ushauri.
Ikiwa mtaweka vikao, hamtapigana hata kama mmoja wenu atakuwa na jazba. Vizuri pia kuweka vikao kipindi ambacho kila mmoja hasira zake zimepungua.
Bila mazungumzo hamtapata ufumbuzi, wanaume wengine siyo waongeaji ila akishakasirika utaona tu amebadilika. Sasa basi, kwa nini usimshawishi akwambie? Hiyo ni kazi yako, atakwambia tu. Ukienda kumsimulia rafiki ndiyo utapata jawabu?

MWANAMKE NDIYO SERIKALI YA MWANAUME
Mwisho kabisa nakutaka mwanamke ujitambue na uelewe nafasi yako ndani ya nyumba. Mwanamke ndiyo serikali ya mume, usijaribu kukaribisha shetani ndani ya nyumba. Endapo utampa maneno mazuri mumeo, wazimu wake wote utaondoka. Shoga mwanaume ni kama mtoto. Ukimdekeza atadeka, ukimbembeleza anabembelezeka, ukimchapa, atakuchukia.
Hata kama una kazi, jaribu kupanga muda wa kumpikia mumeo, kumfulia nguo na kumwandalia mambo megine muhimu ili ajisikie raha na ajivune kuwa na mwanamke mzuri. Ukimwachia kila kitu afanye dada wa kazi, matokeo yake hali ya hewa kuchafuka ndani ya nyumba.
Naomba niishie hapa kwa leo. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine motomoto.

0 comments:

-