Wachache walio katika uhusiano wameweza kung’amua siri zilizopo mioyoni mwa wandani wao, kwa wanaoshindwa hubaki wakifanya mambo ndivyo sivyo bila kujua wanawaudhi wapenzi wao kwa namna moja ama nyingine. Leo nitazungumza zaidi na wanaume, kuhusu siri hizo.
Umeshawahi kujiuliza, kila unayomfanyia mpenzi wako anayafurahia au yanamboa? Linaweza kuwa swali gumu sana kwako, lakini leo nimekuletea siri nzito usizozijua, walizonazo wanawake mioyoni mwao juu ya wapenzi wao. Inawezekana huzijui, hii ni nafasi yako ya pekee kuzifahamu, kujifunza na kuchukua hatua.
INAMAANA GANI?
Kabla ya kuanza kuainisha siri walizonazo wanawake wengi mioyoni mwao juu ya wapenzi wao, ni vizuri kwanza nikaelezea maana halisi ya siri za moyoni. Hizi ni siri za ndani, ambazo mhusika hushindwa kuzitoa kwa hofu ya kuachwa na mpenzi wake.
Hapa namaanisha kwamba hata kama kuna kitu utakachomfanyia na hakipendi, huwa vigumu sana kwake kukueleza wazi na badala yake hubaki akiumia, akisubiri muujiza wa mabadiliko yako! Wakati mwingine huamua kukueleza kwa ishara ambazo wanaume werevu huelewa na kuweka mambo sawa, lakini wale walio na uelewa bapa hubaki wakivurunda kila siku katika uhusiano wao.
Hii ni mada muhimu sana katika maisha ya wapenzi, ila kumbuka inakuhusu sana wewe mwanaume unayesoma na kukuweka sawa ukimjua mwanamke wako vizuri.
Hata hivyo, kwa wewe mwanamke unayeteseka na siri hizo itakusaidia angalau kujua kwamba mpenzi wako atakuwa amepata nafasi ya kuelewa kinachokusumbua moyoni mwako.
Baada ya kuona siri hizi ni vizuri ukamchunguza mpenzi wako na mwisho ufanye mabadiliko katika penzi lako ili kila mmoja afurahie kuwa na mwenzake. Ona siri hizo.
HUHOFIA UAMINIFU
Kwa mtazamo wa kawaida unaweza usione kama hii ni siri, lakini tunapozungumzia Saikolojia ya Uhusiano hili ni siri nzito kwa mwanamke! Wengi wanafikiri kuishia kumwambia mpenzi wako unampenda pekee inatosha kumfanya aamini kila unachokifanya.
Hili halina ukweli hata kidogo, mwanamke anapenda uwe mwaminifu katika kiwango cha mwisho kwake, hataki kuwa na mashaka na wewe katika kila unachokifanya. Anatamani kuwa salama hata utakapokuwa mbali naye kwa sababu za kikazi au mambo mengine.
Ili uaminifu huu ambao mwanamke anauhitaji kwako uwepo, lazima uwe na penzi la dhati kwake, uwe huna ‘kimeo’ chochote nje. Kwa maana hiyo, wakati mwingine mpenzi wako atakuwa huru na simu yako. Wanaume wengi huwa wakali sana kwa simu zao, utawasikia wakisema; “Hii ni simu ya mkononi bwana, unaing’ang’ania ya nini? Sitaki kuona ukipokea simu yangu wala kusoma sms zangu!” Mh! Jamani haya ni mapenzi ya wapi hayo?
Kuna nini cha siri ulichoficha katika simu yako? Kama ni kweli unampenda na upo huru kwake, huwezi kumzuia kuishika simu yako. Kumbuka wanawake wengi ni dhaifu, huwa hawapo tayari kumpoteza mwanaume wake kwa vitu vidogo lakini ukweli ni kwamba hubaki na siri ya maumivu moyoni mwake, wakati huo huo akiwa kituoni, kusubiri mwanaume mwenye mapenzi ya kweli atakayekuwa mwaminifu kwake!
MGUMU KUELEZA TATIZO
Hii ni siri nyingine iliyojificha mioyoni mwa wanawake wengi, inawezekana kabisa hujawahi kumfikisha kileleni tangu mlipoanza uhusiano wenu, lakini hawezi kukuambia. Ni kama bubu!
Anajitahidi kukufanyia vitu fulani vya hapa na pale ili ugundue kuwa unachokifanya hakipendi, lakini kwa sababu wewe unajifikiria peke yako inakuwa vigumu kugundua moja kwa moja kwamba mpenzi wako hajafurahishwa na wewe faragha.
Tatizo kubwa katika hili ni kwamba, wanawake wengi huonyesha kufurahia sana wanapokuwa faragha na wapenzi wao kwa nia ya kukufanya usijisikie vibaya, uone kwamba kazi unaiweza, lakini moyoni mwake anaumia na anawaza kutafuta mwingine atakayeweza kumkata kiu yake ipasavyo.
Inawezekana akawa anakupenda kuliko kawaida, lakini kwa kosa hili ni rahisi sana kutafuta mwanaume mwingine ambaye hata kama hatampenda, lakini awe na uwezo wa kumfurahisha!
Marafiki zangu, nafasi yangu haitoshi, kwa leo naomba kuishia hadi wiki ijayo tena tutakapomalizia mada hii muhimu katika maisha yetu ya kimapenzi. nawashukuru sana kwa kunisoma na ni matumaini yangu kwamba mmeelewa na mtachukua hatua ya kufanya ili kuboresha zaidi maisha yenu ya kimapenzi.
0 comments:
Post a Comment