Wako watu ambao uwepo wao katika ulimwengu wamechangia kwa namna moja au
nyingine kuufanya huu ulimwengu uwe jinsi ulivyo. Wako wengine ambao
wamechangia kwa kiwango kikubwa kuifanya 'mifumo' ya dunia iwe jinsi
ilivyo. Mara nyingi watu hawa tunawasoma kwenye vitabu endapo kama
waliishi miaka mingi iliyopita na endapo kama bado wako hai huwa ni watu
tunao wahusudu na kuwachukulia kama mifano ya kuigwa.
Lakini wako watu ambao ni vigumu kuwahusudu au kuwaandika katika vitabu
vya historia kutokana na jinsi ambavyo walichangia kubadilisha mifumo ya
kimaisha dunia. Moja wapo ya watu hawa ni Wezi ambao mimi binafsi
napenda kuwaita 'Wezi wa Daraja la kwanza' (First Class Thieves). Hawa
wamekuwa toka enzi za kale na wamekuwa wanaushangaza ulimwengu kwa
kiwango cha akili walichotumia na uthubutu walionao katika kutekeleza
matukio.
Moja wapo kati ya wezi hawa ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa
kubadilisha mifumo ya kiusalama ni mtu ambaye ameandika historia katika
ulimwengu na hususani taifa la ufaransa kwa kutekeleza tukio kubwa zaidi
la ujambazi na lenye thamani kubwa zaidi ambayo mpaka leo hii bado
hajatokea mtu mwingine katika nchi ya ufaransa aliyefanikiwa kutekeleza
tukio kubwa kama hilo na kwa mafanikio. Yeye binafsi hakuiba ili tu
apate kutajirika pekee na kuishi maisha ya anasa bali pia aliiba kwa
kuwa aliamini huo ndio wito wake (destiny) na aliiba ili kuudhihirishia
ulimwengu kuwa anaweza. Jina lake aliitwa Albert Spaggiarri.
May 1976: Nice, Ufaransa
Alfred Spaggiari moja ya watu mashuhuri kwenye jiji la Nice nchini
ufaransa na swahiba mkubwa wa Meya wa jiji la Nice Bw. Jacques Medécin,
Spaggiari ambaye shughuli zake alikuwa amebobea kwenye upigaji picha za
mitindo na matukio muhimu zaidi ya kiserika na binafsi alikuwa ameitisha
kikao kilichohudhuriwa na watu wapatao ishirini katika nyumba yake ya
mapumziko ya mwisho wa wiki iliyopo nje kidogo ya jiji la Nice. Kikao
hicho hakikuhusu upigaji picha au siasa bali aliitisha kikao hicho cha
siri na aliwaalika wahalifu kadhaa ili awashirikishe mpango wa siri
aliokuwa nao. Kati ya watu hao 20 watu watano walikuwa ni wawakilishi wa
ukoo wa Mafia wa usisili ( Sicilian Mafia) aliowaakika kutoka Italia.
Akiwa anafungua kikao hicho Spaggiari aliwaeleza kuwa amewaita hapo ili
awashirikishe kwenye tukio la wizi la kihistoria na ambalo anaamini
litakuwa na thamani kubwa sana kiasi kwamba hawataitaji kuiba tena
maishani mwao ili kuishi maisha ya hali ya juu waliyoyapenda.
Spaggiari akawaeleza kuwa amedhamiria kuiba katika Kuba (vault) ya benki
ya Société Générale. Ambayo ndiyo ilikuwa benki kubwa zaidi katika nchi
ya ufaransa kwa kipindi hicho na moja ya benki kubwa zaidi duniani.
Lakini kabla hajaendelea zaidi na 'hotuba' yake watu kadhaa waliokuwepo
kwenye kikao hicho waliangua kicheko cha dharau na kusema kwamba
walidhani kuwa wameitwa kwenye kikao hicho labda 'celebrity' Spaggiari
alikuwa ana ugomvi na 'celebrity' mwenzake kwahiyo alitaka awalipe
wakamfanyie 'umafia' lakini kamwe hawakutegemea mtu 'mboga saba' kama
Spaggiari ati atake kuwashirikisha wao kuhusu tukio la ujambazi kwani
wanaamini kuwa Spagiari hajui chochote kuhusu uhalifu wala hajui hata "a
e i o u" za matukio ya ujambazi.
Spaggiari aka kaa kimya kwa sekunde kadhaa huku macho yake yakiangaza
kwa wahudhuriaji wote wa kikao hicho na macho yake yakakutana na mzee
mmoja wa makamo aliyekuwepo pia kwenye kikao hicho ambaye walifahamiana
vyema na Spaggiari. Spaggiari akampa ishara kuwa awaeleze watu hao
waliohudhuria kikao hicho kuwa yeye ni nani, yeye Spaggiari halisi ni
nani, awaeleze kiundani wamfahamu Spaggiari zaidi ya yule wanayemsoma
kwenye magazeti, zaidi ya Spaggiari 'mboga saba' wanaye mjua.
UTAMBULISHO MFUPI WA "MPIGA PICHA" ALBERT SPAGGIARI
Albert Spaggiari alizaliwa Desemba 14, 1932 katika mji mdogo wa Hyerés
ambapo mama yake alimiliki duka kubwa la mavazi ya ndani ya wanawake
(lingerie).
Akiwa bado yuko katika shule ya upili, katika shule yao Spaggiari
alitokea kumpenda msichana ambaye alikuwa ni mtoto wa Mkuu wa shule.
Mara nyingi Spaggiari alijikuta anaingia kwenye matatizo na walimu
kutokana na kumshushia kipigo kijana mmoja wa kisenegali ambaye alipata
ufadhili wa kusoma shuleni hapo lakini naye alionyesha hisia za kumpenda
binti huyo. Kutokana na Spaggiari kuingia kwenye matatizo mara kwa mara
na walimu hakufanikiwa kumaliza shule kwani alifukuzwa baada ya walimu
kuchoshwa na tabia zake.
Licha ya kutokuwepo shuleni Spaggiari aliendeleza uhusiano wake na yule mtoto wa Mkuu wa shule
Katika juhudi za Kutaka kumuonyesha huyo binti kwamba yeye sio hoe hae
Spaggiari akamuahidi huyo binti kumnunulia pete ya almasi yenye thamani
kubwa sana. Uhalisia ni kwamba Spaggiari hakuwa na hela lakini kutoka
moyoni alipania kuitekeleza ahadi huyo ili azidi kumfanya mpenzi wake
ampende zaidi.
Hivyo basi Spaggiari akamshawishi rafiki yake mmoja kuwa usiku wa siku
moja ana mpango wa kuiba pete ya almasi katika duka mojawapo hapo mjini
kwao.. Rafiki yake akakubali na wakapanga siku wakatekeleza tukio lakini
kwa masikitiko makubwa wakakamatwa.
Baada ya kukamatwa na kushtakiwa mahakamani, Spagiarri alihukumiwa kwenda jela.
Lakini kutokana na umri wake mdogo wa miaka 17, serikaki na Spagiarri
wakakubaliana kuwa akajiunge na jeshi badala ya kukaa jela.
Hivyo basi Spaggiarri akajiunga na jeshi kitengo cha wanajeshi wa kutumia parashuti.
Mwaka 1953 Spaggiari alishiriki katika vita ambayo majeshi ya Ufaransa
yaliivamia koloni lao la Indochina (Vietnam ya sasa na maeneo
yanayoizunguka). Spaggiari alikuwa ni mwanajeshi hodari na aliwahi
kujeruhiwa mara mbili katika mapambano na kutokana na uhodari wake
alitunukiwa nishani ya heshima.
Lakini ni kana kwamba wizi ulikuwa ndani ya vinasaba vya Spaggiari kwani
akiwa huko huko Vietnam na kabla vita haijaisha yeye pamoja na rafiki
yake walivamia duka moja mjini Hanoi na baada ya upelelezi walibainika.
Hii ilipelekea Spaggiari kufukuzwa jeshini na kurudishwa ufaransa na kufunguliwa mashtaka na akahukumiwa miaka mitano.
Spaggiarri akatumikia kifungo na mnamo mwaka 1957 akarudi uraiani.
Baada ya kurudi uraiani Spaggiari akajihusisha na kufanya kazi katika
viwanda vya kutengeneza makabati ya kuhifadhi vitu vya siri (Safes) na
pia akafanikiwa kupata msichana mrembo aliyeitwa Marcelle Audi ambaye
kwa kipindi hicho alikuwa anafanya kazi kama Nesi na akafanikiwa kumuoa.
Baada ya kumuoa waliondoka ufaransa na kuelekea nchini Senegal ambapo
kwa kipindi hicho bado lilikuwa ni koloni la Ufaransa na wakaishi mjini
Dakar. Kwa bahati mbaya hawakufanikiwa kukaa sana Senegal kwani mwaka
1960 Senegal ilipata Uhuru na ikawalazimu warejee tena Ufaransa.
Baada ya kurejea Ufaransa Spaggiarri akaanza kujihusisha na vikundi vya
uzalendo vya nchi za ulaya ambavyo vilikuwa vinapinga wazungu kuachia
makoloni ya Africa.
Kikundi ambacho kilimvutia sana Spaggiarri kiliitwa OAS (Organisation de
al'rmée Secrète). Kikundi hiki kilijihusisha na shughuli za kishushushu
kusaidia kushawishi serikali ya ufaransa isiachie koloni la Algeria na
pia kilifanya shughuli zake kudhoofisha harakati za watu wa Algeria
kudai Uhuru. Spaggiari akajiunga na kikundi hiki mwaka 1961.
Rais wa ufarasa wa kipindi hicho (Rais De Gaulle) mwanzoni alikiunga
mkono kikundi hiki lakini kadiri muda ulivyoenda na kuonekana wazi kuwa
suala la kuipatia Uhuru Algeria haliepukiki, Rais De Gaulle akakipiga
marufuku kikundi cha OAS na vikundi vingine vyote vyenye mlengo huo.
Baada ya harakati zao za OAS kupigwa marufuku Spaggiari akabakia na
kinyongo kikubwa sana dhidi ya Rais De Gaulle. Hivyo basi mwaka huo huo
wa 1961 akasafiri mpaka nchini Hispania kwenda kuonana na mmoja wa
waanzilishi wa kikundi cha OAS mzee aliyeitwa Jenerali Pierre
Lagaillarde. Sababu kubwa ya kumfuata ni kwamba Spaggiari alikuwa
anahitaji apewe ruhusu ya kumdungua kwa risasi Rais De Gaulle ili
kulipiza kisasi kwa
"kuwasaliti" OAS na 'raia' wa Ufaransa kwa kuunga mkono Algeria kupewa Uhuru.
Jenerali Pierre akamwambia kuwa ampe 'ramani' yake jinsi alivyopanga ni namna gani atampiga risasi Rais De Gaulle.
Bila kusita Spaggiari akamueleza mpango wake, kuwa msafara wa Rais De
Gaulle huwa unapita katika mji mdogo wa Hyerès na huwa wanapita mbele ya
duka la mama yake Spaggiari (mama yake Spaggiari alikuwa ni
mfanyabiashara wa mavazi ya ndani ya akina mama (langarie)). Hivyo
Spaggiari akamueleza Jenerali Pierre kuwa atakaa juu ya paa la duka la
mama yake na atakaa na bunduki ya wadunguaji na Msafara wa Rais ukupita
atampiga risasi Rais De Guelle.
Jenerali Pierre akakubaliana naye kuwa arudi ufaransa na akatekeleze
mpango huo lakini akampa onyo kuwa siku hiyo atayotakaa juu ya paa la
duka la mama yake, asifyatue risasi kabla hajapata amri ya moja kwa moja
kutoka kwake (direct command). Spaggiari akakubali na kurejea ufaransa.
Siku ya siku ikafika, Spaggiari akakaa juu ya paa la duka la mama yake,
msafara wa Rais ukapita mbele ya duka, Spaggiari akasubiri 'direct
command' kutoka kwa Jenereli Pierre ili amfyatulie risasi Rais De
Guelle, akasubiri na kusubiri, amri haikuja na msafara wa Rais
ulitokomea mbali na macho yake.
Wiki chache baadae Spaggiarri akakamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya
kujihusisha na vikundi vya 'kigaidi'. Spaggiarri akagundua kuwa Jenerali
Pierre 'alimuuza'.
Mahakama ikamuhukumu kifungo cha miaka minne jela. Spaggiari akatumikia miaka yote.
Siku ya kutoka jela ni mke wake Audi pekee aliyemkuta nje ya geti la
jela akimsubiri waende nyumbani. Spaggiari akamuapia mkewe kuwa hataki
tena kujihusisha na harakati zozote wala siasa. Kuanzia sasa kitu pekee
anachokitaka ni kuwa mume bora kwake.
Spaggiarri hakuwa anatania, akafungua ofisi yake ya upigaji picha katika
jiji la Nice. Akafanya kazi kwa bidii usiku na mchana na ndani ya miaka
michache akaibukia kuwa ndiye mpiga picha bora zaidi katika jiji la
Nice, na harusi zote za hadhi ya juu ni Spaggiari ndiye alipiga picha,
matukio yote muhimu ya kiserikali na binafsi, tenda ya kupiga picha
alipewa Spaggiari. Punde si punde Spaggiari akawa moja ya watu mashuhuri
zaidi katika jiji la Nice, na akafahamiana na kila mtu muhimu kwenye
jiji la Nice. Mpiga picha Spaggiari akawa moja ya raia wanaoheshimika
zaidi jijini Nice.
Lakini licha ya mafanikio na heshima yote, kana kwamba uhalifu
umeandikwa kwenye vinasaba vyake, roho ya Spaggiari ilitaka zaidi! Sio
pesa zaidi, sio umaarufu zaidi, hapana roho ya Spaggiari ilitamani
kuiba! Kufanya tukio moja kubwa kuudhihirishia ulimwengu umahiri wake
katika wizi.
Roho ya Spaggiari iliwasha kwa kiu ya kutaka kuiba, na alijua bayana
roho yake haitotulia mpaka pale atakapo tekeleza walau tukio moja
maridadi la wizi. Na ili kujiridhisha Spaggiari akaamua kuwa atafanya
tukio la wizi ambalo litasimuliwa vizazi na vizazi.
Turejee kwenye Kikao cha "Mpiga Picha" Spaggiari na wenzake
Baada ya wote waliokuwepo kwenye kikao hicho kusikia historia hiyo ya
Spaggiari walishikwa na bumbuwazi. Wote waliduwaa kwani baadhi yao
waliwahi kusikia minong'oni mtaani kuwa mpiga picha Spaggiari ni 'mtundu
mtundu' lakini hawakutegemea kama huo 'utundu' wake aliwahi kuhusika
kwenye maisha ya hatari kama jinsi ambavyo wamesimuliwa kwenye kikao
hicho.
Kwa ufupi kwa historia hiyo fupi, Spaggiari alivuna heshima kutoka kwa
watu wote ambao walikuwa wamehudhuria kikao hicho lakini swali moja
likabaki hewani, je mpango wake ni upi juu ya utekelezaji wa kuiba benki
hiyo ya Société Générale, naye Spaggiari akawajibu kuwa hicho ndicho
alichowaitia hapo kuwa wakae chini wote watoke na mpango kabambe wa
kuiba katika benki hiyo na yeye yuko tayari kusikia mawazo yao kwanza.
Baadhi ya waliokuwepo kwenye kikao kile hasa wale wanachama watano
kutoka ukoo wa Mafia wa usisili, wakatoa maoni yao. Wakasema kuwa kama
anaweza kuwapa uhakika kuwa katika tarehe fulani mahususi benki hiyo
itakuwa na kiwango kikubwa cha fedha basi wao wanaweza wakasaidia wapate
silaha na kuweka mpango madhubuti wa kuivamia hiyo bank na kupora hela.
Baada ya wanachama hao wa Mafia kutoa maoni hayo Spaggiari akawapa jibu
la kuwashangaza sana, kuwa hakubaliani na mkakati huo kwasababu anataka
kwamba tukio hilo watakalotekeleza anataka waweke mpango wa kutumia
akili zaidi badala ya kutumia mabavu na silaha.
Baada ya maoni hayo kukataliwa wengine nao wakatoa maoni kwamba labda
wamteke mtoto au mke wa meneja wa benki kisha watumie kigezo hicho
kumshawishi meneja awasaidie kuiba katika benki yake. Wazo hili nalo
lilipingwa na Spaggiari na akawaeleza kuwa hataki ukatili wowote utumike
katika kutekeleza tukio hili. Mzee mmoja veterani wa kikundi cha OAS
ambaye alikuwepo yeye akasema kuwa anatamani afahamu siku ambayo benki
yoyote kubwa inakuwa na kiwango kikubwa cha fedha kisha wailipue ili
kuikomesha serikali kwa 'kusaliti' kikundi chao cha OAS. Spaggiari
akamjibu kwa kifupi tu kuwa kama akitaka afanye tukio lolote kwa ufanisi
anatakiwa aweke hisia za chuki pembeni. Hivyo wazo lake hilo la kulipua
benki kwa kisasi alikuwa analipinga.
Wale jamaa watano wanachama wa ukoo wa kihalifu wa Mafia, ambao
walisafiri kutoka Itali kuja kuhudhuria kikao hicho wakainuka wote kwa
pamoja na kumwambia Spaggiari kuwa wanaondoka. Wanahisi kuwa licha ya
kuwa ni kweli kama walivyosikia kwenye kikao hicho kuwa amewahi
kushiriki katika mipango ya hatari katika maisha yake lakini wanahisi
kuwa kwasasa Spaggiari ana ndoto za mchana na hayuko kwenye uhalisia
kwasababu kama anakataa maoni yote yaliyotolewa hawaoni uwezekano wowote
wa kikao hicho kuzaa mkakati wenye uhalisia wa kutekeleza tukio la
ujambazi.
Spaggiari akawasisitiza kuwa wakae chini wasikilize maoni mengine
yakiwemo maoni yake lakini wanachama hao wa Mafia wakamwambaia kuwa
hawako tayari kuendelea na kikao hicho kwani wanadhani mkakati wowote
utakaowekwa hapo utakuwa ni kana kwamba wanaenda kujitoa sadaka kwani
haiingii akilini watu muwe na dhamira ya kuiba benki alafu msitumie
silaha. Mafia hao wakainuka, wakaaga na kuondoka.
Kwahiyo Spaggiari akabakia na watu 15 pekee kwenye kikao hicho wengi wao
wakiwa ni wanachama wa zamani wa kikundi cha OAS. Na alivyowaangalia
nyuso zao aligundua dhahiri kuwa ndani ya dakika chache kama hatowapa
mpango wowote wa kuwashawishi kuhusu hilo tukio nao wangeweza kuinuka na
kuondoka.
Spaggiari akaenda mpaka kwenye kabati la pembeni lililopo kwenye sebule
hiyo na kutoka na boksi dogo la saizi ya kati na kulibeba kwa mikono
miwili mpaka kwenye meza iliyokuwepo katikati ya sebule na kisha
akawaomba wote wainuke na kusogea karibu na meza.
Baada ya wote kusogea karibu na meza Spaggiari akatoa makaratasi kadhaa kutoka kwenye lile box na kayatandaza juu ya meza.
Makaratasi yale yalionyesha ramani na mpango mji wa jiji la Nice. Kuna
makaratasi yalionyesha nyumba kwa nyumba na jengo kwa jengo kwa jiji
lote la Nice. Makaratasi mengine yalionyesha juu ya mifumo ya barabara
ya jiji zima. Makaratasi mengine yalionyesha juu ya mfumo ya maji taka
ya jiji zima na hapa katika karatasi hizi za mifumo ya maji taka ndipo
hasa Spaggiari aliwataka awaeleze kuhusu mpango wake anao ufikiria.
Katika karatasi hiyo inayoonyesha mfumo wa maji taka, Spaggiari
akawaonyesha mahali ambapo benki ilipo na akaweka alama kwenye karatasi
kisha akawaonyesha mfereji wa maji taka wa chini kwa chini ( Sewer)
ambao unapita karibu kabisa na benki hiyo na pia akaweka alama kwenye
mfereji huo kisha akawafafanulia zaidi. Akawaeleza kuwa upande ambapo
mfereji huo unapita na kupakana na benki ni takribani mita 5 tu kutoka
kwenye mfereji mpaka kwenye Kuba (Vault) ya benki. Hivyo basi kama
wataweza kuchimba shimo la chini kwa chini (tunnel) lenye urefu wa mita 8
kutoka kwenye mtaro huo wa maji taka kuelekea upande wa benki basi
watakuwa wamefika katikati ya sakafu ya vault ya benki ya Société
Générale na kitu pekee kitakachobaki ni kutoboa tundu dogo kwa kwenda
juu na watakalolitumia kuingilia ndani ya vault kutoka kwenye tunnel
walilochimba kutoka mtaroni. Huo ndio ulikuwa mkakati wake.
Spaggiari aliwaangalia nyuso za wale waliokuwepo kwenye hicho kikao na
alikuwa na uhakika kuwa wamevutiwa na mkakati huo ingawa walikuwa na
maswali kadhaa.
Spaggiari akatoa fursa waulize maswali na swali la kwanza lililokuwepo
kwenye vichwa vya wengi lilikuwa je, watakapokuwa chini wanachimba hilo
shimo (tunnel) hawatashtukiwa kutokana na makelele na mitetemo watakayo
sababisha. Spaggiari akawajibu kuwa japokuwa tunnel la urefu wa mita 8
wanaume kama wao 15 wana uwezo wa kulichimba ndani ya siku hata 3 lakini
ili kuzuia kusababisha kelele na mitetemo amepanga kuwa shimo hilo
litachimbwa taratibu kana kwamba wanakula chakula kwenye sahani kwa
kutumia kijiko. Haijalishi itachukua wiki au miezi mingapi.
Swali lingine lilikuwa je itakuwaje kama vault ina 'sensors' za kuhisi
mitetemo au sauti? Spaggiari akawajibu kuwa kuhusu hilo wampe kama siku
tatu atafahamu hiyo vault ina 'sensors' zipi na ni namna gani watakavyo
jiahami nazo.
Spaggiari akauliza kama kuna swali lingine. Hakukuwa na swali. Kisha
akawaukiza, "who is in?" ("Nani atashiriki nami kwenye hili?") wote 15
waliobakia kwenye kikao hicho walikubali kushiriki katika tukio hilo.
Spaggiari akawaeleza kuwa anawapa wiki moja kila mtu akamalize ratiba
zake alizokuwa nazo, mwenye familia akaage na kudanganya anavyoweza
kwani wakikutana baada ya hiyo wiki moja watakuwa na wiki kadhaa au
pengine miezi kadhaa ya kutekeleza tukio hilo ambalo halijawahi
kufanyika kabla.
Wakaagana, wakatawanyika.
SPAGGIARI NA GENGE LAKE WANAINGIA 'KAZINI'
Wakati wenzake wakiwa wamerudi makwao kuaga familia zao ili warejee
baada ya wiki moja kwa ajili ya 'kazi', yeye Spaggiari kesho yake
alifika mpaka kwenye benki ya Société Générale na akaomba kuwa mteja
afunguliwe sanduki jipya kwa ajili ya kuhifadhi vitu vyake vya
faragha/siri ( safe deposit box) katika vault. Baada ya kukamilisha
taratibu zote za kujaza nyaraka za maandishi na kulipia gharama za
huduma hiyo hatimaye akapelekwa na muhudumu wa benki mpaka kwenye vault
na kuonyeshwa kisanduku ambacho kitakuwa chake. Kisha muhudumu akatoka
nje ya mlango ili kumpa faragha Spaggiari ahifadhi vitu vyake. Baada ya
kuachwa peke yake Spaggiari akatoa saa kubwa ya muito (alarm clock)
ambayo ilikuwa kwenye kibegi kidogo alichokuja nacho. Saa hii ilikuwa na
ukubwa wa kufanana kabisa na saa kubwa ya ukutani. Lakini ilikuwa nzito
zaidi. Na ilitengenezwa kuwa saa ya muito ambayo muda uliotegeshwa
ukifika Saa inaita na kutetema (vibration). Spaggiari akaitegesha saa
hiyo iwe inaita usiku wa manane. Kisha akaiweka kwenye kisanduku chake
alichoonyeshwa. Kisha akakifunga kisanduku, akatoka nje akakabidhi
funguo ya kisanduku kwa muhudumu na kurudi nyumbani.
Baada ya wiki moja kupita na wenzake kurudi kwa ajili yakuanza kazi,
kwanza kabisa Spaggiari akawapa muhtasari juu ya alichofanikisha mpaka
mda huo. Akawaeleza kuwa hawahitaji kuhofu kuhusu 'sensor' za mitetemo
au sauti kwakuwa ameng'amua kuwa vault hiyo haina 'sensor' zozote zile.
Walipo muuliza amejuaje, akawaeleza kuhusu Saa ya muito aliyoiweka
kwenye hiyo vault na kuitegesha iwe inaita muda wa usiku. Na akawaeleza
kuwa kwa siku kadhaa amekuwa akichunguza na hajaona taharuki yoyote
kutoka kwa walinzi au alarm za ulinzi za benki zikilia hivyo ana uhakika
kabisa hakuna 'sensors' zozote kwenye hiyo vault.
Spaggiari alikuwa sahihi kabisa kwani vault hiyo ni kweli haikuwa na
sensor zozote, wenyewe wenye benki waliamini kuwa vault hiyo ilikuwa
haiingiliki kwa namna yoyote (utterly impregnable) kwasababu mlango wake
wa chuma ulikuwa mnene zaidi ya kuta tatu za nyumba ya tofali
zikiunganishwa pamoja na mtu alihitajika kuingiza namba maalumu
(combination) na kutumia funguo kubwa mbili maalumu ili aweze kuufungua.
Pia kuta za hiyo vault zilikuwa haiwezekani hata mtu kuzigusa akiwa nje
kwani vault ilikuwa kati kati ya jengo la benki na kuta zake zilikuwa
nene kiasi kwamba zinazidi hata unene wa kuta tatu za nyumba ya kawaida.
Baada ya Spaggiari kuwapa wenzake muhtasari huo, kawaeleza kuwa hivyo
basi saa hiyo ya muito watakuwa wanaitumia kama muongozo wa ziada ili
wawe wanachimba kwa usahihi zaidi kuekekea chini ya sakafu ya vault
(pinpointing). Baada ya kupeana muhtasari, Spaggiari akaondoka na
wenzake ili akawaonyeshe eneo la kazi.
Walitumia boti ndogo kusafiri katika mto Rivera mpaka mahali ambapo
kiwango kidogo cha maji ya mto yanachepuka na kuingia katika mtaro
mkubwa wa maji taka unaokusanya maji na kupita karibu na benki
waliyotaka kuiba. Walipofika hapa walitumia maboya kuelea juu ya maji
machafu ya mtaro yaliyojaa kinyesi cha binadamu na uchafu mwingine,
walielea kuelekea mbele kwa takribani dakika ishirini wakiwa na ramani
zao mikononi mpaka walipofika sehemu waliyoihitaji.
Baada ya kufika hapo Spaggiari akawapa maelekezo kuwa wanatakiwa
wachimbe moja kwa moja bila kupindisha hata kidogo kwenda mita 8 ndani
na kama watakuwa sahihi baada ya kufikisha mita 8 hizo alarm aliyoiweka
kwenye vault ikilia basi wataisikia juu ya vichwa vyao, ikimaanisha
kwamba wako chini ya sakafu ya vault.
Pia Spaggiari akawagawanya wenzake kwenye shift za kufanya kazi.
Akawaambia kuwa kutakuwa na makundi mawili, kila kundi litafanya kazi
kwa masaa kumi wakati huo wengine watakuwa wamelala na akawasisitiza
kuwa ni lazima walale kwa masaa kumi. Kwahiyo shifti zilikuwa mbili,
masaa kumi kazini na masaa kumi kulala. Pia akawakataza wasiguse kabisa
pombe au kahawa kwa muda wote ambao watakuwa wanafanya hiyo kazi.
Siku iliyofuata kazi ilianza. Kazi ilifanyika bila papara, taratibu na
kwa umakini mkubwa. Kazi ikaendelea kwa siku kadhaa, wiki kadhaa na
baada ya miezi miwili hatimae walifikisha tanuru (tunnel) la urefu wa
mita 8. Baada ya kufikisha umbali huo Spaggiari akawaambia wasubiri
usiku wa manane kusikiliza saa ya muito ili wajue kama wako sahihi au
la. Ilipofika usiku wa manane alarm ya saa iliyowekwa kwenye vault na
Spaggiari iliita, na waliisikia juu ya vichwa vyao kabisa. Wakapongezana
kwani sasa walikuwa na uhakika asilimia mia moja kuwa wako sahihi,
walikuwa wako chini ya sakafu ya vault na kilichobakia ilikuwa ni
kutoboa hiyo sakafu na kuchukua 'mwali wao'.
Spaggiari akawaambia wenzake kuwa inabidi wapumzike kwa siku mbili
kuisubiria Bestille Day ndipo watoboe sakafu na kuchukua mwali wao.
Bastille Day (siku ya Uhuru wa Ufaransa) ambayo husheherekewa kila mwaka
tarehe 14 July na kwa mwaka huu 1976 ilikuwa inaangukia siku ya
alhamisi, hivyo hii ilifanya kuwe na siku nne za mapumziko (alhamisi na
ijumaa (sherehe za Bastille Day) Jumamosi na jumapili (mapumziko ya
mwisho wa juma)). Kwahiyo Spaggiari alitaka wapate muda wa kutosha kwa
siku nne ili wachukue fedha na vitu vingi kadiri wawezavyo.
Hatimaye alhamisi ikawadia na Spaggiari na genge lake wakamalizia
kutoboa sakafu ya vault na kuingia ndani. Jambo la kwanza walilolifanya
baada kufanikiwa kuingia ndani ya vault ni kuchomelea mlango wa vault
kwa ndani ili mtu aliyepo nje asiweze kuufungua.
Kazi ikaanza na Spaggiari kwa kutumia uzoefu aliokuwa nao wa kufanya
kazi kwenye viwanda vya kutengeneza 'safes' akawaongoza wenzake katika
zoezi la kufungua visanduku. Kazi ilifanyika mchana na usiku kwa siku ya
kwanza ya alhamisi na kesho yake siku ya Ijumaa Spaggiari akawaambia
wenzake wapumzike kwa masaa machache ili nao washerehekee sikukuu ya
Bastille kama wenzao walioko huko mitaani. Hivyo basi Spaggiari akatoka
kwenye vault na kurudi mtaani kununua mvinyo pamoja na vyakula vya anasa
na kurudi navyo kwenye vault kwa ajili ya kusheherekea. Baada ya
kumaliza kula na kunywa kazi iliendelea usiku na mchana siku hiyo ya
ijumaa, jumamosi na ilipofika jumapili mchana walikuwa wamefanikiwa
kufungua yapata visanduku 400 vilivyokuwa na fedha taslimu, vito vya
thamani, hati fungani na vitu vinginevyo vya thamani kubwa. Inakadiriwa
kuwa thamani ya 'mzigo' wote ambao Spaggiari na genge lake walipata
unafikia Faranga Milioni 60 za ufaransa (60 million French Frans).
Ilipofika muda wa mchana siku ya Jumapili mvua ilianza kunyesha na
Spaggiari akahisi mitaro waliyotumia kuingilia inaweza kujaa maji na
hivyo kufanya zoezi la kutoka kuwa gumu hivyo basi akawaamuru wenzake
waondoke kabla mvua haijawa kubwa. Lakini kabla hawaondoka aliwaambia
wenzake kuwa anahitaji kufanya jambo moja la muhimu la mwisho. Huku
akionekana akiwa na hisia na msisimko wa hali ya juu, spaggiari
alichukua kopo la rangi alilokuwa amekuja nalo pamoja na brashi ndogo ya
kapakia rangi, kisha akausogelea ukuta mmoja ndani ya vault na kuandika
maandishi makubwa yaliyo someka;
"SANS ARMES, NI HAINE, NI VIOLENCE" ("Without weapons, nor hatred, nor violence" ("Pasipo silaha, wala chuki, wala ukatili")).
Hiyo ndio 'falsafa' aliyotaka kuifikisha kwa ulimwengu mzima kujitambulisha yeye ni 'mwizi daraja la kwanza' wa dizaini gani.
Baada ya hapo wakafungasha mizigo yao, wakatokomea.
'Maisha' Baada ya Tukio..
Siku ya jumatatu benki ya Société Générale ilifunguliwa na shughuli
ziliendelea kama kawaida pasipo yeyote kung'amua kuwa kuna jambo
lilitokea ndani ya vault. Na kama ilivyo ada ilipofika majira saa Tatu
na nusu asubuhi wafanyakazi wawili walielekea kwenye chumba cha Vault
kukifungua ili kuruhusu wateja kuhifadhi vitu na wengine kuchukua vitu
walivyohifadhi. Walipofika mlangoni wakaingiza namba maalumu na kisha
kama ilivyo utaratibu wakaingiza funguo mbili katika matundu mawili juu
ya mlango na kuzungusha funguo lakini jambo la ajabu mlango
haukufunguka. Walihangaika kuzungusha funguo karibia nusu saa lakini
mlango haukufunguka.
Baada ya juhudi zote hizo bila mafanikio wakaamua watoe taarifa kwa
meneja msaidizi wa benki aliyeitwa Pierre Bigou. Bw. Pierre baada na
yeye kuhakikisha kuwa mlango ulikuwa haufunguki ikabidi aagize aitwe
muhunzi ili aje kuwasaidia. Dakika chache baadae muhunzi alifika na
akaanza kuukagua mlango, na ndani ya dakika kumi na tano akawa
ameng'amua kuwa mlango umechomelewa kwa ndani na hakuna namna ambayo
wanaweza kuufungua wakiwa nje.
Sehemu ya mapokezi baadhi ya wateja walikuja kwa ajili ya kutumia
visanduku vyao vya kwenye vault walianza kupaniki na ilimbidi meneja
mwenyewe wa benki ahusike kuwatuliza na kuwaondoa wasiwasi. Meneja
alitumia maarifa yake yote ya huduma kwa wateja kuwaondoa hofu wateja
wake na kuwataka wawe watulivu,
" Nothing to worry about monsieur. A
minor technical problem madame. Your valuables are quite safe but there
may be a slight delay" ("ondoa hofu muheshimiwa. Ni tatizo dogo tu
la kiufundi. Vitu vyenu viko salama ila itachukua muda kidogo
kurekebisha.") Meneja wa benki Bw. Jacques Guenet alisikika akiwatuliza
wateja wake.
Baada ya muhunzi kugundua kuwa mlango huo hautaweza kufunguka kwa nje
akapendekeza kuwa watoboe ukuta ili kuingia ndani. Viongozi wa benki
wakakubali na kazi kutoboa ukuta ikaanza. Kutokana na unene wa ukuta na
kutoboa kwa makini ili wasisababishe hasara nyingine, ilichukua
takribani masaa matatu kutoboa tundu kubwa kiasi la kumuwezesha mtu
kupita. Yule muhunzi ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuchungulia ndani na
alipochungulia alipatwa na mshangao kana kwamba amepoteza fahamu kwa
sekunde kadhaa. Hakuamini alichokuwa anakiona ndani ya vault. Huku bado
akiwa na mshangao alimgeukia Meneja wa Benki aliyekuwa amesimama nyuma
yake na kumwambia kwa mshangao,
"Merde de putain" ("you have been robbed" ("Mmeibiwa")).
Baada ya wote bumbuwazi kuwaisha kutokana na kutoamini macho yao
walichokuwa wanakiona mbele ya macho yao, hatimae wakapiga simu polisi
na haraka sana polisi wakawasili. Baada ya Polisi kuwasili na kuingia
ndani ya vault nao pia hawakuamini kile walichokuwa wanakiona mbele ya
macho yao. Wote kwa pamoja macho yao yaliganda kwenye Ujumbe ulioandikwa
kwenye ukuta, "sans armes, ni haine, ni violence" (Pasipo silaha, chuki
wala ukatili).
KUKAMATWA, KUSHTAKIWA NA KUWA 'HURU' TENA
Ndani ya miezi miwili polisi walifanikiwa kugundua kuwa Spaggiari ndiye
muhusika mkuu wa tukio lile. Haijulikana hasa ni namna gani polisi
walifanikiwa kugundua kuwa Spaggiari ndiye alikuwa 'mastermind' wa tukio
lile, kwani kumekuwa na maelezo mengi sana yanayokinzana lakini angalau
ufafanuzi unaoonyesha uhalisia kidogo ni kwamba mmoja wapo wa watu
walioshiriki tukio lile alipopewa mgao wake wa fedha pia alipewa na
miche kadhaa ya dhahabu (gold bars) na bila kutumia akili au kuwa na
subira akauza mche mmoja ndani ya wiki chache baada ya tukio. Baada ya
siku kadhaa mtu aliyeununua mche huo aliripoti polisi kuwa ameuziwa mche
wa dhahabu unaofanana kabisa na moja ya miche inayoripotiwa kuwa
imeibiwa kwenye vault ya benki ya Société Générale.
Polisi wakamfatilia huyo mtu na wakafanikiwa kumtia nguvuni na baada ya
kumuhoji kwa siku kadhaa akawataja wenzake wote akiwemo Albert
Spaggiari.
Polisi waliposikia kuwa Spaggiari ndiye alikuwa kiongozi wa tukio hilo,
walishikwa na butwaa kwani Spaggiari alikuwa ni moja ya watu mashuhuri
na anayeheshimika zaidi jijini Nice. Na kipindi wanapata taarifa hii
alikuwa yuko safarini mashariki ya mbali akiwa amemsindikiza rafiki yake
Meya wa jiji Bw. Jacques Médecin, katika ziara ya kiserikali.
Siku ambayo Meya na Spaggiari wanarejea Nice kutoka mashariki ya mbali,
Spaggiari alikamatwa hapo hapo uwanja wa ndege na kufunguliwa mashtaka
ya kuhusika kupanga na kushiriki tukio la ujambazi katika benki ya
Société Générale.
Kesi hii ilitikisa vyombo vya habati ulimwengu mzima na umaarufu wa
Spaggiari ukaongezeka maradufu na mwenyewe alionekana kufurahia haswa
jinsi alivyokuwa anazungumziwa kila kona ya Dunia.
Wakati kesi ikiwa inaendelea Spaggiari akatunga hadithi ambayo kwa
bahati mbaya Jaji aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo aliiamini na akawa
anatamani kujua kiundani. Spaggiari aliwaeleza kuwa alifanya tukio hilo
ili kukiwezesha kiuchumi kikundi cha siri cha wazalendo kilichoitwa
'Catena' (neno la kifaransa linalomaanisha 'Chain' (mnyororo)).
Spaggiari akawaeleza kuwa hayuko tayari kuwapa taarifa za kikundi hicho
Polisi kwani hawaamini bali yuko tayari kutoa taarifa kwa Jaji huyo peke
yake. Hivyo basi ikawekwa ratiba maalumu ambayo Spaggiari alikuwa
anapelekwa ofisini kwa Jaji na kila walipokutana alikuwa anampa
kikaratasi alichokiandika kwa mafumbo (coded message) na ilikuwa
inamlazimu Jaji akune kichwa haswa ili kung'amua kilichoandikwa na
Spaggiari kuhusu siri za hicho kikundi cha 'Catena'.
Katika moja ya vikao vyao na Jaji, Jaji akiwa 'bize' kung'amua Ujumbe
huo wa mafumbo Spaggiari aliinuka kutoka kwenye kiti kana kwamba anataka
kumkaribia Jaji ili ampe ufafanuzi. Lakini jambo la ajabu alikimbia kwa
spidi ya ajabu mpaka dirishani na kujirusha nje kwa uhodari wa hali ya
juu (kumbuka aliwahi kuwa mwanajeshi kitengo cha Parashuti). Ofisi ya
Jaji ilikuwa juu ghorofa ya Tatu katika hilo Jengo la mahakama, lakini
kutokana na Spaggiari kujirusha kwa uhodari alitua chini juu ya paa la
gari bila kudhurika. Kisha akakimbia kuvuka barabara na kulikuwa na piki
piki inamsubiri.
Baada ya kukwea juu pikipiki akageuka kuwaangalia juu dirishani maaskari
pamoja na Jaji waliokuwa wanachungulia wakiwa hawaamini kilichotokea
ndani ya sekunde chache. Spaggiari akapayuka kwa nguvu
"Au revoir"
(kwaherini). Kisha akatabasamu kwa dharau na inasemekana akawaonesha
kidole cha kati. Kisha kwa mwendo wa kasi na uhodari pikipiki ikapotea
mbele ya upeo wa macho yao. Hiyo ndio ilikuwa mara ya mwisho kwa mamlaka
za serikali za ufaransa kumuona Spaggiari.
Wiki mbili baadae mtu mwenye gari ambalo Spaggiari alitua alipo ruka
kutoka ghorofani alipokea cheki ya thamani ya faranga 5,000 pamoja na
kikaratasi kikisema ni kwaajili ya matengenezo ya paa la gari lake.
Pia kuna tetesi ambazo zimeenea mno toka kipindi hicho mpaka sasa kuwa
mtu aliyempakia Spaggiari kwenye pikipiki na kumtorosha alikuwa
Christian Estrosi bingwa wa Dunia wa mbio za pikipiki ambaye baadae
alikuja kuwa waziri katika serikali ya Ufaransa.
Baada ya kutoroka Spaggiari alielekea nchini Argentina na kuishi huko na
kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha muonekano (plastic surgery).
Inasemekana Spaggiari alikuwa anarudi mara kwa mara nchini Ufaransa
kumuona mkewe Audi na Mama yake.
Akiwa nchini Argentia inasemekana kuwa alikuwa karibu sana na CIA
akiwasaidia kufanikisha shughuli ambazo CIA hawakutaka kujihusisha nazo
moja kwa moja kwa kuhofia jina la idara yao kuchafuka ikitokea siri
kuvuja.
Mfano mzuri ni jinsi ambavyo Spaggiari (au daniel jina walilotumia CIA
kumtambua (code name)) alishirikiana na Michael Townley afisa wa DINA
(kitengo cha ushushushu cha nchi ya Chile) kuchora mchoro na kulipua
gari la balozi wa Chile nchini Marekani.
Skandali hii ilichangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha mahusiano ya
kidiplomasia kati ya marekani na Chile na hakuna aliyejua uhusika wa CIA
mpaka pale mwaka 2000 ambapo CIA waliweka hadharani nyaraka kadhaa za
siri baada mda wake wa usiri kupita.
Albert Spaggiari alifariki June 8, 1989 kwa kansa ya koo kutokana na matumizi ya sigara.
Fedha, Vito vya thamani, hati fungani na nyaraka nyingine za siri
zilizoibwa na Albert Spagiari na Genge lake havijapatika mpaka leo hii.
Tukio hili limebakia katika vichwa vya Wafaransa kama tukio kubwa pekee
la wizi wa vitu vya thamani ya juu zaidi na lililotekelezwa kwa
umaridadi na akili nyingi au kama Spaggiari mwenyewe alivyolielezea;
"Sans armes, ni haine, ni violence" (Pasipo silaha, chuki wala ukatili").